MHE. SAMIRA K. AMOUR: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali itaweka utaratibu wa kuwafikia wanawake wa vijijini, Mkoani Kagera, kwa kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo hiyo bila kikwazo cha mtandao? Ahsante, (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera na ninamhakikishia tu kwamba, Serikali inafahamu kwamba tuna maeneo ya vijijini na maeneo hayo mara nyingine vikundi hivi vinapata shida au ugumu wa kuwafikia Maafisa Maendeleo ya Jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo limefanyika, moja ni kuhakikisha kwamba Maafisa Maendeleo ya Jamii wanafanya outreach Huduma Mkoba, kwa maana ya kwenda kwenye vijiji na kwenye kata kwa ajili ya kutoa elimu, kuhamasisha na kuviwezesha vikundi maalum kupata mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tumeunda Kamati za Mikopo katika ngazi za kata na kamati hizi zinahusika kuwafikia wananchi katika vijiji. Kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kulisimamia hili, lakini tumelichukua kuongeza nguvu zaidi kwa Mkoa wa Kagera na mikoa mingine ili kuhakikisha kwamba vikundi hivi vinafikiwa na Maafisa Maendeleo ya Jamii na zile Kamati za Mikopo ili kutoa mikopo kwa ufanisi mkubwa zaidi.