Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Jafari Wambura Chege (2 total)

MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: -

Je, kwa nini Serikali isiyondoe mfumo wa wanafunzi kurudi mchana kula nyumbani na kurudi tena shuleni ili kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Jimbo la Rorya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa mitaala ya elimu msingi na sekondari, wanafunzi wanapaswa kusoma vipindi sita hadi nane kwa siku kwa shule za msingi, na saba hadi kumi kwa shule za sekondari, kutegemea na ratiba ya siku. Katika kutekeleza takwa hili, halmashauri zimekuwa na ratiba ya watoto kurudi nyumbani kupata chakula na kurudi shule kumalizia vipindi. Aidha, halmashauri nyingine wanafunzi hukamilisha idadi ya vipindi bila kurudi nyumbani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia Waraka Namba Tatu wa Mwaka 2016 kuhusu utekelezaji wa Elimu Bila Ada, Mwongozo wa Kitaifa wa Utoaji wa Huduma ya Chakula na Lishe Shuleni wa Mwaka 2021 na Mpango wa Utekelezaji wa Mwongozo wa Kitaifa wa Utoaji wa Huduma ya Chakula na Lishe Shuleni wa Mwaka 2023 Serikali kwa kushirikiana na wazazi imeweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba kila mtoto anapata chakula shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia kuwa hali ya upatikanaji wa huduma ya chakula shuleni inatofautiana kati ya halmashauri moja na nyingine, Makatibu Tawala wa Mikoa wanaelekezwa kufanya tathmini ya utekelezaji wa utoaji wa huduma ya chakula shuleni katika mikoa yao ili kuondoa ratiba ya wanafunzi kurudi mchana kula nyumbani na kurudi tena shuleni.
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:-

Je, lini Mradi wa Maji wa Miji 28 ya Rorya – Tarime utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Jimbo la Rorya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Miji 28 wa Rorya - Tarime uliopo Mkoa wa Mara kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 134.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi zinazotekelezwa kupitia mradi huo ni pamoja na ujenzi wa dakio (intake) katika Ziwa Victoria lenye uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 29 kwa siku, ujenzi wa mtambo wa kutibu maji (treatment plant) wenye uwezo wa kutibu maji lita milioni 28 kwa siku, ulazaji wa mabomba umbali wa kilometa 110, ujenzi wa matanki matatu yenye jumla ya ujazo wa lita milioni 10 sanjari na ujenzi wa kituo kimoja cha kusukuma maji (booster station).

Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa 16% na unatarajiwa kukamilika mwaka wa fedha 2026/2027 kulingana na upatikanaji wa fedha ambapo mradi huo utanufaisha wananchi wapatao 460,885 waishio katika Wilaya za Rorya na Tarime.