Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Emmanuel John Khambay (2 total)

MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY aliuliza: -

Je, lini Serikali itafanya maboresho ya makazi ya askari pamoja na kununua magari mapya Gereza la Babati Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Emmanuel John Khambay, Mbunge wa Babati Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Gereza la Babati ni miongoni mwa Magereza yaliyojengwa miaka mingi tangu mwaka 1974 hali iliyosababisha uchakavu wa miundombinu ya gereza pamoja na majengo ya makazi ya Askari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Magereza limeanza kutekeleza mpango mkakati wa muda mfupi na muda mrefu ambapo kwa Gereza Babati ziko nyumba tatu zinaendelea na ujenzi kwa kutumia mapato ya vyanzo vya ndani vya ubunifu. Aidha, katika mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali imetenga shilingi 5,380,000,000/= kwa ajili ya ununuzi wa magari 31 kwa shughuli za Utawala na kusafirisha Mahabusu. Pindi magari hayo yatakapofika, Gereza la Babati litapatiwa gari moja mpya kwa matumizi ya kituo.

MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Barabara kilometa 24 kutoka Kona ya Mrara hadi Lango la Hifadhi ya Tarangire kwa upande wa Kijiji cha Mamire kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel John Khambay, Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa ujenzi wa barabara ya kutoka kona ya Mrara hadi Lango la hifadhi Tarangire kwa upande wa Kijiji cha Mamire yenye urefu wa kilometa 24 kwa kiwango cha lami ambayo itachochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wanaopitiwa na barabara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2025/2026, Serikali imeanza uboreshaji wa barabara hii yenye urefu wa kilometa 24 kwa kufanya usanifu wa kilometa 0.8 na kujenga kwa tabaka la lami pamoja na ujenzi wa daraja la Mrara kwa gharama ya shilingi milioni 944.88 ambapo mkandarasi amepatikana ili kuanza ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara hii kwa tabaka la lami pamoja na ujenzi na matengenezo ya Barabara za Jimbo la Babati Mjini kwa kutenga bajeti kwa awamu, ahsante.