Supplementary Questions from Hon. Emmanuel John Khambay (5 total)
MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali, nina swali moja la nyongeza. Kama ambavyo amekiri mwenyewe kwamba Gereza la Babati ni miongoni mwa magereza yaliyojengwa kwa miaka ya zamani, je, ni nini mpango wa Serikali wa kujenga gereza lingine jipya ambalo pia litakuwa ni gereza la kisasa linaloendana na wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Emmanuel kwa swali lake la nyongeza ambalo ni la muhimu sana. Kwanza tukiri ni kweli tuna uhitaji mkubwa wa magereza nchini, kwani katika hali ya sasa nchi nzima tuna idadi ya magereza 129. Kati ya magereza hayo, magereza 10 yana hadhi ya magereza ya kanda, magereza 76 yana hadhi ya magereza ya mikoa na wilaya na magereza 43 ni magereza ya wazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali hiyo, tuna upungufu wa takribani wilaya 50 ambazo hazina magereza, lakini kazi inayoendelea sasa ya ujenzi wa magereza katika maeneo mbalimbali ambayo kwa kweli kwa baadhi ya maeneo imepiga hatua nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Wilaya ya Karatu gereza limekamilika, Wilaya ya Kilosa limeanza ujenzi, Wilaya ya Gairo linaendelea, Wilaya ya Kingurungundwa kule Mchinga nalo linaendelea. Ninaamini kwamba na maeneo mengine pia tutaendelea na hatua kama ambavyo nimetaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali kwenye ujenzi wa magereza haya ni kuendelea kuweka fedha kwenye bajeti, kwani tayari tumeshafanya tathmini ya uhitaji wa magereza hayo kwamba kila gereza moja linahitaji wastani wa shilingi bilioni nane kulijenga. Hivyo, kwa magereza 50 tunahitaji wastani wa shilingi bilioni 40 ili tuweze kujenga magereza hayo. Sambamba na hilo, tunafahamu pia ipo changamoto kubwa ya makazi ya Askari Magereza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jambo hilo, pia Serikali imeandaa mpango wa muda mrefu ambao utajenga wastani wa nyumba 6,368 za magereza zitakazoweza kukaliwa na wastani wa kata 21,187. Bajeti ya fedha hizo zinahitajika zaidi ya shilingi trilioni 2.88 kwa ajili ya kukamilisha mradi huo.
MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kituo cha Afya cha Nangara kimejengwa na nguvu za wananchi na ni jengo moja tu la OPD. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa fedha nyingine ili kuweza kumalizia majengo mengine ili wananchi hao ambao wanafuata huduma umbali mrefu waweze kupata huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo hiki cha afya, kwanza tunawashukuru sana wananchi kwa kutoa nguvu zao na kuweza kuunga mkono juhudi za Serikali, lakini pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nimeshaongea na Mkurugenzi, na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI niendelee kumwelekeza Mkurugenzi kutenga fedha za ndani ili kukamilisha baadhi ya majengo katika kituo hiki baada ya kutoa OPD waendelee kutoa na huduma nyingine ambazo zinatakiwa kwenye kituo cha afya. (Makofi)
MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, Ziwa Babati limevamiwa na magugu na linaenda kupotea. Nini mpango wa Serikali katika kulinusuru Ziwa hilo ambalo ni muhimu kwa wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Babati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, Serikali inao mpango endelevu wa kukabiliana na athari za mazingira ambazo zimetokea kwenye maziwa yetu, siyo tu Ziwa Babati, tunalo Ziwa Victoria, Ziwa Jipe pamoja na na maziwa mengine.
Mheshimiwa Spika, kwa Ziwa Babati, cha kwanza ambacho tumeweka mkakati ni kushirikiana na Wizara ya Maji ambao ndio wanaohusika na mabonde pamoja na maji ili kwanza tuweke mipaka kwa maana ya kuweka beacons za mipaka ambazo zitaonyesha ukomo wa eneo la shughuli za kibinadamu.
Mheshimiwa Spika, pili, Serikali itaendelea kuwatafutia wananchi wa maeneo yanayozunguka maziwa shughuli mbadala ambazo hazitaathiri maeneo haya ambayo tunalenga kuyahifadhi.
MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itakamilisha zoezi la upembuzi yakinifu juu ya ujenzi wa bwawa la umwagiliaji katika Kata ya Bagara, hususani eneo la Kijiji cha Nakwa ili wananchi wa eneo hilo waweze kunufaika na kilimo cha umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, napenda kujibu swali la nyongeza kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameweza kuuliza kwamba kama nilivyosema hapo awali, nimtoe mashaka Mheshimiwa Mbunge. Kasi ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba, wananchi wake wananufaika na nchi hii na ameamua kukifanya kilimo kuwa uti wa mgongo.
Mheshimiwa Spika, ili kukamilisha hoja hiyo, eneo la umwagiliaji, ambalo wakati anaingia yeye madarakani lilikuwa ni eneo dogo sana la kumwagilia, takribani eneo la hekta laki sita, wakati Mungu ametupa fursa ya eneo lenye ukubwa zaidi ya hekta milioni 40. Ninakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge na ukawaambie na wananchi, Waziri wa Kilimo anawaambia, atakwenda kuwafikia maeneo yote ambayo ni ya kimkakati ili wananchi waweze kuzalisha na tuweze kuuza nje ya nchi na ndani ya nchi chakula pamoja na mazao mbalimbali.
MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Nina maswali mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kutambua umuhimu wa machinjio iliyopo ndani ya Halmashauri ya Mji wa Babati, kuna kipande ambacho kinahitaji lami, kipande cha kutoka Junction ya kuelekea Ikulu mpaka Machinjioni na kwenye Machinjio kuelekea kwenye Junction ya Barabara ya Babati - Arusha. Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha kipande hicho cha barabara kwa kiwango cha lami kwa manufaa ya wananchi wa Jimbo la Babati Mjini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, ni lini Serikali itajenga barabara ya kutoka Hangoni mpaka Junction ya kuelekea Ikulu inayopitia Kwere kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Emmanuel John Khambay, Mbunge wa Jimbo la Babati, amekuwa mfuatiliaji wa mara kwa mara kuhusiana na miundombinu ya barabara katika Jimbo la Babati Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali imeweka mpango mkakati kwenye bajeti zake. Kwanza kuna bajeti za kawaida za TARURA katika Mji wa Babati, na pili, tuna Mradi wa TACTIC ambao pia itakwenda kuboresha barabara za lami na kujenga miundombinu mingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu barabara ambayo ameisema Mheshimiwa Mbunge, ya Junction kwenda Ikulu, Junction kwenda Babati. Nimhakikishie tu kwamba, Serikali kwa ujumla wake tumeainisha maeneo yote muhimu ambayo yanahitaji huduma za kijamii na maeneo kama ya kimasoko, stendi, vituo vya huduma, na shule. Maeneo haya yote yanapewa kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika mipango yetu ya bajeti tutahakikisha tunatenga fedha kwa ajili ya kujenga barabara hizo kwa kiwango cha lami au changarawe kwa kadiri itakavyowezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nimhakikishie tu kwamba hata hiyo barabara nyingine ambayo ameitaja tutaendelea kuitengea bajeti kwa awamu kuhakikisha kwamba Wananchi wa Jimbo la Babati Mjini wanapata barabara bora kwa shughuli za kiuchumi. (Makofi)