MHE. ARIF S. PREMJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Serikali iliahidi kuboresha miundombinu ya maji kwa kuwajengea tenki la lita 1,000,000 Kijiji cha Likonde, Kata ya Mayanga na ahadi hiyo iitolewa tarehe 27 Septemba, 2022 ambalo litaenda kuwasaidia wakazi zaidi ya 24,000. Je, ahadi hiyo itatekelezwa lini? Ninaomba nisisitize neno “lini?”
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, samahani kidogo, ninaomba kujua ni jimbo gani.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge, ni jimbo gani tena?
MHE. ARIF S. PREMJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni Jimbo la Mtwara Vijijini.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza miradi nchini kote na nchi yetu ina vijiji takribani 12,318. Katika utekelezaji wa miradi ni vijiji 1,575 tu ambavyo vimebaki kutofikishiwa huduma rasmi ya maji. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, eneo hilo tunalichukua likiwemo ndani ya miradi 878 ambayo haijakamilika yenye gharama ya shilingi trilioni 1.3. Tunaamini kwamba miradi hii itakapokamilika yote kwa ujumla na eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge ameliongelea basi litakuwa limekamilika katika utekelezaji huo. (Makofi)