Contributions by Hon. Alan Thomas Mvano (3 total)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa nafasi hii. Awali ya yote kwa kuwa nami ni mara ya kwanza ninasimama mbele ya Bunge hili Tukufu, ninaomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye ameendelea kutujalia kheri na afya njema sisi wote ambao tuko hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii vilevile, kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwanza kabisa kwa kuaminiwa na Watanzania kwa kupigiwa kura nyingi za kishindo na kwa ushindi mkubwa alioupata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa kuniteua chini ya vikao alivyoviongoza yeye mwenyewe. Mimi ndugu yenu, kusimama na kuomba ridhaa kwa wananchi wa Kakonko na ninawashkuru sana wananchi wa Kakonko kwa kuniamini na kunichagua ili niweze kuwawakilisha katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ahadi yangu ni kwamba sitowaangusha, nitafanya kazi usiku na mchana kwa nguvu zangu zote na kwa akili yangu yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa vilevile, kupongeza kazi kubwa ambayo anaifanya Mheshimiwa Rais wetu. Sisi kule Kakonko na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla, niseme Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupatia heshima kubwa sana wananchi wa Mkoa wa Kigoma. Hii ni kwa sababu miaka ya nyuma watu walikuwa wanaichukulia Kigoma kama eneo ambalo halifai. Watu walikuwa wanaamini watumishi ambao wanafanya vibaya Serikalini wakipelekwa Kigoma maana yake wamepewa adhabu, lakini leo Mheshimiwa Rais huyu Dkt. Samia Suluhu Hassan ameionesha heshima ya wananchi wa Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayasema haya kwa sababu miaka ya nyuma hatukuwa tumeunganishwa na barabara za lami kuelekea mikoa mingine, lakini leo ukitoka Mwanza, ukitoka Dar es Salaam, ukitoka Tabora, ukitoka kona yoyote ya nchi hii ukienda Kigoma utafika kwa barabara za lami, huyo ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya Kakonko, kwa miaka minne ambayo Mheshimiwa Rais wetu aliongoza Taifa hili, kipindi kile cha kwanza alituletea fedha nyingi za maendeleo jumla ya fedha alizozileta ni shilingi 28,910,712,714.65. Ninaomba Mheshimiwa Rais huyu apokee shukurani nyingi sana kutoka kwa wananchi wa Kakonko. Ndiyo maana tuliona hospitali ya wilaya ilijengwa, stendi mpya ya kisasa ikajengwa, chuo cha VETA kikajengwa, barabara zikajengwa, shukrani nyingi sana na pongezi nyingi sana zimwendee Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitumie nafasi hii kuwapongeza viongozi wote wanaomsaidia Mheshimiwa Rais wetu. Kwa nafasi ya pekee nimpongeze sana Waziri Mkuu wetu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba anafanya kazi kubwa sana. Wasilisho aliloleta hapa kwetu linaonesha namba ambavyo tunaona matumaini makubwa katika Taifa letu na nimesimama hapa kwa kweli kumtia moyo na kuwaambia Watanzania kwamba, Serikali tuliyonayo na viongozi tulionao, Mawaziri tulionao na Naibu Mawaziri tulionao, wanafanya kazi kubwa sana, wanapaswa kutiwa moyo ili waendelee kufanya kazi kwa moyo wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi hiki kifupi, ninaendelea kutoa shukurani kwa Serikali yetu hii. Mwaka huu Wilaya yetu ya Kakonko imepokea jumla ya watumishi 142. Serikali yetu hii imefanya kazi kubwa sana, ninamshukuru sana na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo ametuletea mbegu ya ruzuku ya alizeti tani 10 kwa kipindi kifupi hiki. Vilevile, tunashuhudia ujenzi wa soko la kisasa katika Wilaya yetu ya Kakonko. Hayo ni mambo ambayo lazima niyaseme ili Watanzania wajue kazi kubwa ambayo Serikali yetu inafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo hayo, nimekuwa nikifuatilia michango ya Wabunge wengine na kwa kweli nimejifunza mengi na nimesimama hapa kusema kwamba, pamoja na mambo mengine yote, bajeti iliyowasilishwa kwetu na mipango iliyowasilishwa inaonesha namna ambavyo Taifa letu linakwenda kuzalisha kwa kiwango kikubwa mazao ya kilimo, mazao ya uvuvi, kwenye utalii na sekta nyingine za uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili tuweze kufika huko tunahitaji fedha. Kwanza kabisa lazima tukubali kwamba, fedha tunazozipata kutoka kwenye makusanyo lazima zitumike vizuri kwa uwazi na kwa uwajibikaji. Wale wote ambao hawatatumia fedha zetu vizuri lazima wachukuliwe hatua ili fedha zote zinazopatikana kutoka kwenye sekta zote ziweze kuelekezwa kwenye maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Wilaya ya Kakonko yapo mambo ambayo tunatamani kuona yanafanyika. Kwenye upande wa afya, tunatamani kuona kata saba ambazo hazina vituo vya afya nazo zinapata vituo vya afya, lakini vilevile, tunatamani kuona maeneo yale yaliyotengwa kwa ajili ya chuo cha uuguzi, basi chuo hicho kikaanzishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kilimo vilevile, tunatamani kuona tunakuwa na kiwanda cha kuchakata zao la muhogo. Vilevile, tuone kwamba ile miundombinu ya umwagiliaji ambayo imechakaa ifanyiwe kazi ili wakulima wetu waweze kuzalisha katika misimu yote. Vilevile, tumetenga ekari zaidi ya 1,000 kwa ajili ya kilimo cha parachichi, tunatamani kuona eneo hilo linaendelezwa ili mambo yaweze kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa barabara mvua zilizonyesha zimeathiri sana maeneo yetu, watu wa Itumbiko, Katanga na Njoomulole wanashindwa kufanya shughuli zao kwa sababu mvua zimeharibu miundombinu ya barabara. Kwa hiyo, maeneo yote hayo yanahitaji fedha ili wananchi wetu waweze kufanya shughuli zao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mkoa wa Kigoma yapo mambo tunatamani kuona yanafanyika. Kwanza kabisa, tuna reli ya kisasa ambayo mradi wa ujenzi unaendelea lot six, tunatamani kuona Serikali imeweka kipaumbele katika eneo hilo ili tuweze kukuza biashara na nchi za jirani zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Ziwa Tanganyika ni ziwa la kimkakati, tunahitaji kuona tunakuwa na meli nzuri kwa ajili ya kusafirisha watu wetu. Tumeshuhudia siku chache zilizopita watu nane wamepoteza maisha, lazima kama Taifa tuweke meli nzuri kule ili watu wetu waweze kusafiri vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba uniruhusu nitoe mapendekezo yangu kwa bajeti hii…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote, nimshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye anaendelea kutujalia afya sisi sote. Nitumie vilevile nafasi hii kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya na niwapongeze sana Waziri wetu wa Nishati, Naibu Waziri wa Nishati na timu yote ambayo inamsaidia majukumu. Kwa kweli, kazi kubwa inafanyika na mwenye macho haambiwi tazama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengine yote ninayoweza kuyasema ni kwamba lazima nianze na pongezi kwa sababu mimi ninatokea Kakonko katika Mkoa wa Kigoma, Mkoa wa Kigoma hapa tunavyozungumza tayari umekwishaunganishwa kwenye gridi ya Taifa. Ndiyo maana tunaona katika Mkoa wa Kigoma viwanda sasa vinajengwa. Ukienda Kigoma Mjini utaona Kiwanda cha Cement, utaona Kiwanda cha Nondo, utaona Kiwanda cha Kuchakata Asali, kuna Viwanda pale vya Kusindika na Kuchakata Samaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kwenye Wilaya ya Kasulu utaona Kiwanda cha Sukari. Tunaamini mpango mzuri wa Serikali hii kwamba Kiwanda cha Kuchakata Zao la Muhogo katika maeneo ya Kakonko na Kibondo tunaamini hili nalo litafanikiwa kwa sababu tayari tunao umeme wa uhakika. Hizi ni pongezi kubwa sana na lazima tuziseme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo Wilaya ya Kakonko ina vijiji 44 na vitongoji…
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Alan, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Festo Sanga.
TAARIFA
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa yangu ni fupi tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Mbunge anachangia hapa pia Watanzania wakumbuke kwamba Mkoa huu ulikuwa unatumia diesel ya takribani shilingi bilioni 21 kwa mwaka, lakini kwa juhudi ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kuunganisha gridi ya Taifa, tumeokoa shilingi bilioni 21 kwa mwaka kwa matumizi ya diesel. (Makofi)
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana na ninaipokea taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge subiri, taarifa ya Mheshimiwa Sanga, unaipokea? (Kicheko)
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na ninaipokea taarifa. Kimsingi Watanzania watambue kwamba Mkoa wa Kigoma unatambua sana jitihada kubwa zinazofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mengi ningeweza kuyasema, lakini kwa sababu ya muda niseme hivi, Wilaya ya Kakonko pekee vijiji vyote 44 hivi tunavyozungumza vina umeme, kati ya vitongoji 355, vimebakia vitongoji takribani 50 tu, vingine vyote vina umeme. Kwa hiyo, lazima nitoe shukrani nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona jitihada za Serikali, tarehe 17 ya mwezi Januari ulisainiwa mkataba wa shilingi trilioni 1.2 ambapo vitongoji 9,009 vilikuwa vinakwenda sasa kunufaika na umeme vijijini. Kwenye mpango ule Serikali hii njema imesema Mkoa wa Kigoma, Mkoa wa Kilimanjaro na Mkoa wa Katavi vitongoji vyote vinakwenda kupata umeme kupitia kwenye mkataba huo. Ninaomba kwa niaba ya wananchi wa mikoa hii nifikishe shukurani hizi nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na shukrani hizo, yapo mapendekezo. Jambo la kwanza ambalo ninapendekeza ni kwamba, tunatamani sana kuona kazi kubwa inaendelea na tayari mipango mizuri tumeiona, jambo la umuhimu ni kwamba umeme umeshakwishafika kwenye vitongoji vingi, hamu ya wananchi sasa ni kuona umeme unasambaa ndani ya vitongoji. Kwa hiyo, hili ni jambo muhimu na wananchi wanatamani sana kuliona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni vitendea kazi. Wakati Wizara inapeleka vitendea kazi katika maeneo yetu, ni muhimu sana kuangalia jiografia za maeneo yetu, maeneo ambayo yana milima mikubwa na mabonde, yapelekewe vitendea kazi kwa uharaka na yaangaliwe kwa jicho la pekee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mathalani, tunashukuru sana katika Wilaya ya Kakonko tumepata gari dogo jipya upande wa TANESCO, lakini tunaomba pia kupitia nafasi hii tuweze kupata lori kwa sababu ya jiografia tuliyonayo ili wananchi wetu waweze kupata huduma nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine muhimu sana, ni kwamba tutakubaliana kwamba umeme sasa tunao, lakini matumizi ya umeme tuliyonao walio wengi wanatumia umeme kuwasha taa majumbani na kuchaji simu. Sasa kama Taifa tunahitaji kufanya mageuzi ya matumizi ya umeme wetu, tunahitaji kuufanya umeme utumike kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kupendekeza kwamba Wizara itengeneze timu izunguke katika nchi hii kupitia viongozi na waliopo katika mikoa waangalie watu wanahitaji umeme ambao wanahitaji kuutumia kwa ajili ya kuzalisha ili watu hawa wapewe kipaumbele. Ninatoa mfano, Wilayani Kakonko kuna mwekezaji anafuga ng’ombe kisasa, anafanya uwekezaji mkubwa kabisa pale, lakini ili afikishiwe umeme kwenye eneo lake anatakiwa alipie shilingi 65,000,000. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji Wizara iliangalie eneo hili kwa jicho la pekee kwa sababu hawa watu wenye viwanda, taasisi za Serikali, shule, viwanda tunahitaji wafikishiwe umeme, hawa ndiyo watumiaji wakubwa. Huyu mtu akifikishiwa umeme kwenye kiwanda chake hiki kwenye biashara yake kama hii ataweza kuajiri watu. Unaona kwenye biashara kama hii ndugu yetu huyu analazimika kukamua ng’ombe kupata maziwa mara moja kwa siku, badala ya kupata lita 12,000 za maziwa analazimika kupata lita 6,000 pekee kumbe angekuwa na umeme angeweza kukamua mara mbili kwa siku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mchango wangu wa leo unajikita katika eneo hili, Wizara iangalie na itenge fedha, tuzunguke katika nchi hii ili kuona zile taasisi zote ambazo zinahitaji umeme, zifikishiwe umeme. Viwanda vyote vinavyohitaji umeme wafikishiwe umeme ili hawa watumiaji wakubwa waweze kuwa na manufaa makubwa na vilevile manufaa hayo yaweze kushuka katika jamii yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kutoa mchango huo, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye anaendelea kutujalia afya njema, vilevile niendelee kuwashukuru sana wananchi wa Kakonko kwa kuniamini na kunituma kuwawakilisha katika hili Bunge Tukufu. Ahadi yangu kwao ni kwamba, nitaendelea kufanya kazi hii kwa uaminifu na nitafanya kazi hii kwa maslahi mapana ya Wilaya ya Kakonko na Nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe vilevile pongezi kwa Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Katika Wilaya ya Kakonko yapo mambo ambayo tumeyaona yamefanyika kwa kipindi kifupi, ikiwa ni pamoja na kutuletea mbegu za alizeti za ruzuku. Kwa kweli wananchi wa Kakonko wanashukuru sana, tumepokea na kazi inaendelea ndani ya Wilaya ya Kakonko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili tunashukuru pia tumepata Kituo cha Utafiti wa Mazao katika Wilaya ya Kakonko na tumekwishatenga ekari 267 na kazi inaendelea. Jambo la tatu, tunashukuru pia wakulima wetu wa tumbaku wamekaa muda mrefu bila kulipwa na siku mbili zilizopita wamepokea malipo ya zaidi ya milioni 300. Tunaishukuru sana Serikali hii inaongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunaamini na fedha nyingine ambayo haijalipwa, italipwa ili wananchi wetu waendelee kufanya shughuli zao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kakonko ingependa kuona mambo kadhaa yanafanyika katika mwaka huu wa fedha. Jambo la kwanza ni kukarabati miundombinu ya umwagiliaji na kujenga ile ambayo haijajengwa. Kwanza kabisa tuna maeneo ya Itumbiko, Liwiti, Katengela, Mwiluzi na Bwaru. Maeneo hayo yote yanafaa kwa kilimo cha umwagiliaji, kwa hiyo tunaamini ili tuweze kuboresha uzalishaji katika sekta ya kilimo, basi Wizara ituangalie kwa jicho la pekee maeneo hayo ili miundombinu iweze kutengenezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tunaomba sana kiwanda cha kuchakata na kuongeza thamani zao la muhogo kama ilivyoahidiwa, basi jambo hili nalo lifanyike ili wananchi waweze kuona faida katika zao hilo. Jambo la tatu, tumetenga ekari zaidi 1,000 kwa ajili ya block farming ya zao ya parachichi, tunaiomba Serikali ilione pia eneo hilo ili tuweze kufanikiwa na wananchi wetu waweze kupata manufaa ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne, tunaomba pia zana za kisasa za kilimo ziweze kufika katika Wilaya ya Kakonko, kwa sababu bado wapo wananchi wengi ambao wanaendelea kulima kwa kutumia jembe la mkono. Jambo la mwisho katika mambo ambayo tungependa kuona yanafanyika, ni kuendelea kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa wakati ili wakulima wetu waweze kufanya vizuri na kuongeza uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo yote hayo nimetoa pongezi kwa Serikali na nimeona mpango mzuri wa Waziri na mpango mzuri wa Rais. Mambo haya yote yakifanyika maana yake ni kwamba, tunakwenda kuona mageuzi katika uzalishaji wa mazao yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa pendekezo langu mimi ninajikita katika eneo la masoko. Pamoja na mambo mengine yote yatakayofanyika tusipoliangalia vizuri eneo la masoko maana yake ni kwamba tunakwenda kuzalisha kitu kikubwa na mwisho wa siku tutakosa pakupeleka. Jambo la kwanza la kuangalia Wizara hii kwa kushirikiana na Wizara nyingine lazima ije na mpango mkakati wa namna ya kuendea masoko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, soko la kwanza la muhimu la kuangalia ni sisi wenyewe Watanzania tupo zaidi ya milioni 70 maana yake ni kwamba tukiwa na mkakati mzuri sisi wenyewe tutakuwa soko la kwanza kwa mazao tunayozalisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili soko la nchi za jirani yapo mambo yanapaswa kufanyika ili tuweze kuyaendea masoko hayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, tujenge maghala maeneo ya mipakani ili watu wanaotaka kupeleka mazao nje ya nchi yetu waweze kuwa na sehemu ya kuhifadhia mazao yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Serikali ijikite katika kuhakikisha kilimo kinachofanyika kinakuwa ni kilimo cha mkataba, watu wasilime bila kujua watapeleka wapi mazao yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, lazima Wizara ije na mpango wa kuhakikisha wananchi wetu wanapata elimu ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza wajue wanapolima wanatumia mbolea gani kwa ardhi gani? Vilevile masoko ya mazao yanapatikana wapi? Kwa hiyo ninashauri Wizara ije mpango wa kuandaa channel maalum kwa ajili ya television zetu kama walivyofanya wenzetu wa utalii Safari Channel inafanya vizuri, watu wakiangalia wanaona fursa zilizopo, tuangalie kwenye channel zetu na redio zetu, zitoe habari za elimu kwa ajili ya wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejikita katika eneo hili kwa sababu jukumu la kumi la Wizara ya Kilimo ni kutafuta masoko na kuratibu masoko, lakini eneo la tatu ni masoko ya kimataifa. Hapa ninapendekeza kwamba Wizara ije na mpango mkakati wa kuyaendea masoko ya kimataifa kwa kuwatumia Mabalozi wetu walioko katika nchi za mbali. Moja kati ya eneo la kupima performance ya Mabalozi wetu iwe ni pamoja na kuangalia exports wanazozifanya kutoka Tanzania kupeleka kwenye nchi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo haya yote muda hauwezi kutosha kuelezea haya, ninaomba sana Serikali iangalie eneo hili la masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, pendekezo langu kwa sababu lazima mambo haya yaende pamoja, unaona Wizara ya Uchukuzi inaingia lazima liweke vizuri miundombinu, unaona Wizara ya Viwanda na Biashara inaingia kwa sababu lazima tutafute masoko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapendekeza ikimpendeza Mheshimiwa Rais aunde Wizara maalum ya masoko ili sasa iende kufanya kazi moja kwa moja kwa kushirikiana na Wizara nyingine ili tuweze kuyatafuta masoko ndani, tutafute masoko ndani ya nchi jirani na tutafute masoko katika nchi za mbali
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa mchango huo ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)