Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Alan Thomas Mvano (3 total)

MHE. ALAN T. MVANO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wakulima wa zao la muhogo Kakonko wanapata soko la uhakika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeendelea kutekeleza mkakati wa kuendeleza zao la muhogo nchini kwa lengo la kuongeza tija na uzalishaji, kuimarisha upatikanaji wa masoko ya uhakika ya bidhaa za muhogo na kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya kuchakata muhogo ili kuongeza thamani ya zao hilo. Moja ya eneo la kimkakati katika kuendeleza muhogo ni Halmashauri za Wilaya ya Kakonko na Kibondo, Mkoani Kigoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2025/2026, imetenga fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu ya masoko, kukaushia, kuchakata na kuhifadhi muhogo katika Halmashauri ya Kakonko. Tayari Wizara imefanya tathmini ya eneo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo pamoja na kuandaa usanifu, michoro na gharama za awali kwa ajili ya kuanza kumtafuta mkandarasi wa ujenzi. Wizara inaamini taratibu zote zitakamilika mapema ili kuhakikisha wakulima wanaanza kuongeza thamani ya zao la muhogo, kupunguza upotevu baada ya mavuno na kuimarisha upatikanaji wa masoko kwa wakulima. Ahsante sana.
MHE. ALAN T. MVANO aliuliza: -

Je, lini Barabara ya Kakonko kwenda mpaka wa Muhange kupitia Gwarama kilometa 41.43 itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Alan Thomas Mvano, Mbunge wa Kakonko, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Kakonko – Gwarama – Muhange yenye urefu wa kilometa 41.43 ni barabara kuu inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kigoma. Kwa sasa Serikali ipo katika hatua ya kutafuta fedha ili kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, ikiwa ni hatua ya awali katika mchakato wa kuijenga kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usanifu utakapokamilika na gharama za ujenzi kujulikana, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami, ahsante. (Makofi)
MHE. ALAN T. MVANO aliuliza: -

Je, lini Mkandarasi atakamilisha kuchimba na kujenga kisima cha maji katika Kijiji cha Kihomoka kama ilivyo kwenye mkataba wake?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Alan Thomas Mvano, Mbunge wa Jimbo la Kakonko, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilipanga kuchimba visima vitano katika Wilaya ya Kakonko kupitia programu maalumu ya uchimbaji wa visima 900. Hadi sasa jumla ya visima vinne kati ya vitano vimechimbwa katika Kijiji cha Ruhuru viwili, Kihomoka kimoja, na Nyamtukuza kisima kimoja, ambapo kwa pamoja vina uwezo wa kuzalisha jumla ya maji lita 55,500 kwa saa.

Mheshimiwa Naibu Spika, visima hivyo baada ya kupata maji vimeendelezwa kwa kujengewa miundombinu rahisi ya kutolea huduma kwa wananchi (point source) na vinaendelea kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wakazi wa vijiji hivyo. Hata hivyo kisima kimoja kilichokuwa kimepangwa kuchimbwa katika Kitongoji cha Centre B kilichopo Kijiji cha Kihomoka hakikuweza kuchimbwa. Hivyo, Serikali imekiingiza kisima hicho kwenye mpango wa programu ya vijiji 1,575 visivyokuwa na huduma ya maji ambayo inaanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2026/2027.