Supplementary Questions from Hon. Alan Thomas Mvano (8 total)
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Kakonko Mkoa wa Kigoma tunao uchimbaji wa madini ya dhahabu Kata ya Nyamtukuza, Vijiji vya Nyamtukuza maeneo ya Nyamwilonge. Tarehe 10 Disemba tulikwenda na Mkuu wa Mkoa pale na akazuia shughuli za uchimbaji kwa sababu zilikuwa zinakiuka sheria za mazingira na zinaathiri wananchi wa Vijiji zaidi ya saba vya Kihomoka, Kumwiyando na Vijiji vingine vya Bwera mpaka Nyamwilonge. Je, ni hatua gani zimechukuliwa na Serikali ili kunusuru maisha ya wananchi hao kwa sababu mto ule haufai kabisa kwa matumizi ya binadamu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala la uchimbaji wa madini linaendeshwa kwa mujibu wa sheria na suala la uhifadhi wa mazingira linasimamiwa kwa mujibu wa Sheria, Sura ya 191.
Mheshimiwa Spika, ninaomba nitumie nafasi hii kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Kakonko kwamba kipaumbele cha kwanza ni kutunza mazingira, lakini Serikali itaendelea kuhakikisha inaweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji wa madini ili kunufaika na rasilimali za madini vilevile kutunza mazingira katika maeneo hayo. Tutawasiliana na Ofisi ya Wizara ya Madini ili tuweze kuliweka sawa na wananchi waweze kuendelea kuchimba madini.
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa nipongeze na nishukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa taarifa, Mkoa wa Kigoma umekuwa ukizalisha zaidi ya tani milioni moja za muhogo kwa mwaka. Wilaya ya Kakonko imekuwa ikizalisha zaidi ya tani 184,000 na Wilaya ya Kibondo mathalani zaidi ya tani 174,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza la nyongeza; je, Wizara ya Kilimo ina mpango gani wa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara ili kupanua wigo wa masoko ya zao hili la muhogo ndani ya Wilaya ya Kakonko na Mkoa wa Kigoma? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa bei ya zao la muhogo ilianguka sana, kutoka kuuzwa shilingi 800 hadi 1,000 kwa kila kilo moja kwenda kuuzwa shilingi 150 hadi shilingi 200. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwanusuru wananchi ambao ni wakulima wa zao la muhogo ambao hadi sasa wameshindwa kuvuna zao hilo, kwa sababu hata wakivuna hawawezi kuuza kwa bei iliyoko sokoni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze pia bwana Alan Mvano ameanza vizuri kuwafuatilia wananchi wake wa Jimbo la Kakonko na ninaomba nimjibu kwamba, moja sisi kama Serikali, Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara tumekuwa tukifanya kazi kwa ukaribu sana. Ndiyo maana utaona katika moja ya hatua ya awali sisi ambayo tunaifanya sasa hivi ni jukumu la kujenga soko katika Halmashauri ya Kakonko. Wizara ya Viwanda na Biashara itakuja ku-complement jambo hili kwa kujenga viwanda ambavyo vitasaidia wakulima katika eneo hilo. Kwa hiyo, huo ni mpango ambao upo na ni endelevu kwa muda wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mpango wa Serikali baada ya bei kushuka; mpango wa Serikali ndiyo huo ambao tumeainisha kwamba kwa nini tunajenga soko. Lengo ni kuhakikisha kwanza moja, tunaongeza thamani, ndiyo maana utaona tumeainisha hapa kwamba tunataka wananchi waongeze tija kwa kuchakata yale mazao yao yaweze kudumu kwa muda mrefu ambapo tunaamini kwamba ukishakausha muhogo badala ya kuuza katika bei ya chini unaweza ukakaa kwa muda mrefu na ukapata bei ambayo ni nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi kama Serikali, jambo hili tunalifahamu na tunalifanyia kazi kwa ukaribu kabisa. Kwa hiyo, tu nimthibitishie tu Mbunge kwamba moja ya kazi kubwa ambayo tutaendelea kuifanya katika eneo hili ni kuboresha haya mazingira ili bei ya muhogo isiweze kushuka kama ambavyo ameainisha hapa.
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru. Wilaya ya Kakonko ina mtandao wa barabara wa kilometa 391.24 na uwezo wa TARURA ni kufanya matengenezo kilometa 120 tu sawa na 30.6%. Je, ni lini Serikali itaongeza bajeti ya TARURA katika Wilaya ya Kakonko?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba bajeti ya TARURA kila mwaka, kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 imeendelea kuongezeka. Kwa mfano, kutoka shilingi bilioni 210 mwaka 2021/2022 mpaka mwaka huu wa fedha zaidi ya shilingi bilioni 870, ukiondoa fedha za dharura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tunatambua kwamba uhitaji wa fedha ni mkubwa zaidi, lakini tutaendelea kutenga fedha kwa awamu kujenga barabara za Kakonko ili wananchi waweze kusafiri na kusafirisha bidhaa zao kwa ufanisi mkubwa zaidi.
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ninaipongeza kazi kubwa inayofanywa na Serikali yetu hii inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara hii ya Ujenzi inafanya kazi kubwa sana katika nchi yetu. Pongezi kubwa sana na ushirikiano tunauona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa barabara hii ya kutokea Kakonko kwenda kwenye mpaka wa Burundi eneo la Muhange ni potential sana kwenye Wilaya yetu. Kwa sababu ya umuhimu wake jambo la kwanza ninamuomba Waziri utayari wake, twende Kakonko aone barabara hii, kwanza aone umuhimu wake vilevile aone hali ya barabara kwa sasa. Jambo la muhimu sana hilo ninaomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kwamba, barabara hii inategemewa na wananchi wa Kata za Nyamtukuza, Nyabibuye, Gwarama, Muhange, Kasuga, na Kakonko; wananchi zaidi ya 60,000 wanaitegemea barabara hii. Sasa kutokana na mvua zilizokuwa zikinyesha barabara hii imekwishapandishwa hadhi, sasa hivi ipo TANROADS.
Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kuhakikisha kuwa barabara hii inapitika vizuri kwa sababu siku chache zilizopita lori limeanguka, limepata ajali katika barabara hii kwa sababu ya ubovu wa barabara kwa ajili ya mvua …
MWENYEKITI: Swali, Mheshimiwa tunakushukuru.
MHE. ALAN T. MVANO: … sasa nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba barabara hii inapitika kwa viwango vya TANROADS wakati tukisubiria upembuzi yakinifu ufanyike? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mvano, Mbunge wa Kakonko, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa niaba ya Serikali na kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, tupokee pongezi zake kwa kazi kubwa ambazo zinafanyika katika shughuli ya miundombinu na hasa barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hii barabara kwanza ilikuwa ipo chini ya Wakala wa Barabara Vijijini; na kwa sababu ya umuhimu wake, tunajua ni barabara ya mpakani, ndiyo maana imepandishwa hadhi. Si hadhi tu, kwa sababu inaunganisha nchi na nchi, tunajua wenzetu wa Burundi wamesogeza makao yao makuu ndiyo maana hata imepandishwa kutoka hadhi ya barabara ya mkoa kuwa trunk road. Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba umuhimu huo tunautambua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimuhakikishie nipo tayari, tutakapopata muda wakati wowote tunaweza kwenda tukaiona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kupitika ni suala la kiutendaji. Ninaomba nimuagize Meneja wa Mkoa wa Kigoma ahakikishe kuwa tutakapomaliza Bunge hili apate muda wiki hii akaione na ahakikishe kwamba anafanyia ukarabati ili iweze kupitika na wananchi waweze kupata huduma bora za usafiri na usafirishaji katika barabara hiyo. (Makofi)
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Naibu Spika, Shule tatu za sekondari katika Jimbo la Kakonko hazina kabisa vyumba vya maabara, nazo ni Kambi Secondary, Dr. Mpango Secondary na Kakonko Boys Secondary School. Je, nini mpango wa Serikali kuhakikisha shule hizi tatu nazo zinapata maabara? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Alan Mvano, Mbunge wa Kakonko, alishaleta taarifa hiyo Ofisi ya Rais, TAMISEMI, na tayari Idara ya Elimu imeshaandaa mpango kwa ajili ya kuanza ujenzi wa maabara hizo katika shule za sekondari tatu. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itafanya shughuli hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia kumsisitiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko kwamba pamoja na fedha za Serikali Kuu, ni muhimu waanze hatua za awali za ujenzi kwa awamu kwa kutumia fedha za mapato ya ndani ili fedha za mapato ya Serikali Kuu zikienda zifanye umaliziaji wa majengo ya maabara hizo.
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Kakonko tunashukuru sana Serikali kwa kutujengea kilometa tatu za lami kuelekea hospitali ya wilaya, ukiacha barabara hiyo mtandao wa lami katika Mji wa Kakonko ambao ndiyo makao makuu ya wilaya tuna meta 950 peke yake. Kwa kuwa moja ya ahadi ya kiongozi wa nchi ilikuwa ni kuongeza mtandao wa barabara za lami, ni upi mpango wa Serikali kuhakikisha sasa Makao Makuu ya Wilaya ya Kakonko yanaongezewa barabara kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Alan, Mbunge wa Jimbo la Kakonko na nimpongeze kwa kuendelea kuwapambania wanajimbo la Kakonko na wanajimbo wanafahamu Mbunge wao kwa namna gani anavyowasilisha changamoto za jimbo na sisi kama Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kutenga bajeti na kuhakikisha tunafanya ujenzi katika barabara hizo ambazo Mheshimiwa Mbunge umeziainisha.
Mheshimiwa Spika, ni mpango wa Serikali kila halmashauri na makao makuu ya halmashauri kuendelea kujenga barabara hizi kwa kiwango cha lami angalau kwa awamu kwa kila mwaka ili kuhakikisha halmashauri zetu zinapata huduma hii na zinakuwa smart. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali itaendelea kumpa ushirikiano kuhakikisha kwamba tunajenga barabara hizo na zinatoa huduma iliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali na jitihada hizo, ninaamini Waziri atakuwa tayari kuongozana na mimi kwenda Kakonko ili aweze kujionea hali ya upatikanaji wa huduma ya maji ilivyo, lakini pamoja na hayo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Katika Kijiji cha Kihomoka wapo wananchi wanaishi eneo linaitwa Nabulilije na wanatembea kilometa 10 kufuata huduma ya majisafi na salama. Sasa ni upi mpango wa Serikali wa dharura kuhakikisha kwamba wananchi hawa sasa wanapata huduma hiyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Wafanyakazi wa Serikali, wa RUWASA pamoja na Mamlaka ya Maji wamekuwa wakipata shida sana kutembea katika Wilaya ya Kakonko katika kushughulikia changamoto za maji. Ni upi mpango wa Serikali kuhakikisha sasa wanapelekewa gari ili waweze kufanya shughuli zao vizuri na wananchi wapate huduma ya maji? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninakubaliana na ombi la Mheshimiwa Alan Thomas Mvano, Mbunge wa Kakonko. Niko tayari kuongozana naye kwenda Kakonko, ili kujionea hali ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Sana Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi na ufuatiliaji wa miradi, kwa ajili ya wananchi wake waliomtuma kuhakikisha kwamba, tunamtua mama ndoo kichwani. Sisi Serikali tunaahidi kumpa ushirikiano mzuri kabisa kuhakikisha kwamba anatimiza azma yake ya kuwatumikia Wanakakonko.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu ambao Mheshimiwa Mbunge amesema, ni kweli kabisa Kijiji cha Kihomoka kina centre mbili. Centre ya kwanza tulichimba kisima, tukajenga miundombinu na tayari wanapata huduma nzuri kabisa, lakini Centre B ambayo ni kilometa 10 kuna wafugaji zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, kama nilivyojibu katika jibu la msingi, tunaiingiza kwenye programu ya vijiji 1,575 katika mwaka wa fedha 2026/2027, ili sasa tuchimbe kisima kwa kutumia mitambo ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alinunua katika mikoa yote 26. Itaenda kufanya hiyo kazi bila kuwa na changamoto yoyote na wananchi wa Kakonko watapata huduma ya majisafi na salama, hasa katika eneo la Kihomoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kulitazama suala la vitendea kazi. Vitendea kazi hivi vinasaidia sana watendaji wetu katika utekelezaji wa miradi, katika usimamizi wa miradi na katika shughuli mbalimbali za kiofisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua umuhimu huu na Mheshimiwa Mbunge amefika mpaka kwa Mheshimiwa Waziri na ameongelea kuhusu hili suala. Ninataka nimpe Mheshimiwa Mbunge habari njema, kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupatia fedha kwa ajili ya kununua magari 29 mapya ili kwenda kuwasaidia watendaji wetu kutekeleza majukumu yao. Ninamtoa hofu DM wa Kakonko, yupo kwenye orodha hiyo ya kupatiwa gari, ili aweze kusimamia miradi vizuri na iwe na tija kwa wananchi.
MHE. ALAN T. MVANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, na mimi nipongeze jitihada hizi nzuri za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 Wilaya ya Kakonko 60% ilionesha kuwa na watoto, 30% vijana na 10% wazee. Sasa kwa muktadha huo katika Wilaya ya Kakonko hatuna shule ya amali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni upi sasa mpango wa Serikali kwa kuzingatia kundi hili kubwa la 60% ya wananchi wa Kakonko ambao bado ni watoto wa kujenga shule ya amali katika Wilaya ya Kakonko ili kuweza kuwajengea uwezo na kuhakikisha wanakuwa wakiwa na elimu bora katika mazingira yetu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, katika utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa shule za sekondari za amali kwanza Serikali ilitoa kipaumbele kwa halmashauri au wilaya ambazo hazina Vyuo vya VETA, lakini kwa sababu ya dhamira njema ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, sasa wilaya zote zinaendelea na ujenzi wa VETA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa muktadha huo tuna uhakika kwamba Wilaya ya Kakonko pia itapata Chuo cha VETA lakini wakati huo huo tutaangalia uwezekano wa kutenga fedha kwa ajili ya kujenga shule za amali katika Jimbo la Kakonko. (Makofi)