Supplementary Questions from Hon. Benjamin Lukubha Ngayiwa (5 total)
MHE. BENJAMIN L. NGAYIWA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali kuhusu kuboresha huduma katika hospitali yetu ya Manispaa ya Kahama, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Mheshimiwa Naibu Waziri amesema Serikali inatenga bajeti kwa ajiili ya kuboresha huduma kwa kujenga jengo la dharura na kuweka vifaa vya uchunguzi kwa maana ya CT- Scan. Sasa ni lini Serikali ina mpango wa kupeleka CT- Scan kwenye hospitali hii ambayo inapokea wagonjwa wengi sana kutoka hospitali zingine?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni lini sasa Serikali ina mpango wa kuboresha na kukamilisha majengo ya zahanati ambayo yamefikia hatua za lenta kama vile Chalya, Nyandekwa na sehemu zingine za Wilaya yetu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ngayiwa. Kwanza, ninampongeza Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI anatoa michango mizuri kwa ajili ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kweli kwa idadi kubwa ya wagonjwa ambao tunawapokea katika hospitali hii ya Halmashauri ya Manispaa ya Kahama na uhitaji wa CT- Scan kwa ajili ya upimaji, uchunguzi wa mifupa kwa wagonjwa wetu, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa maana ya kwamba ndani ya muda mfupi Serikali imekwishafanya tathmini na uhitaji huo tumeshauona, tunaipeleka CT-Scan pale ili iende kutoa matibabu kuwahudumia wahitaji wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu zahanati nilikwishaeleza hapa kwamba zaidi ya zahanati 1,841 zinakwenda kufanyiwa ukarabati na kumaliziwa maboma, Serikali inajielekeza zaidi katika miradi hii ambayo tayari imekwishaanzishwa ili tuweze kuikamilisha kabla ya kuanza miradi mingine ya zahati na vituo vya afya. (Makofi)
MHE. BENJAMIN L. NGAYIWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkandarasi wa ujenzi wa barabara za TACTIC pale Kahama Mjini (Sichuan) alisitishiwa mkataba wake baada ya kusuasua na kuchelewa kukamilisha mradi huo ndani ya muda. Mchakato wa kuanza kutafuta mkandarasi mpya umeanza. Sasa swali langu kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini mchakato huo wa kumpata mkandarasi mpya utakamilika ili barabara za pale Kahama ambazo zimekuwa kero sana kipindi hiki cha mvua ziweze kuanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba pale Kahama palikuwa na mkandarasi huyu huyu ajulikanaye kama Sichuan. Baada ya kuwa amesuasua kwa muda mrefu, Serikali iliamua kusitisha, na kwa kweli iliamua kuvunja mkataba. Tulivunja mkataba huo na tumeelekeza kwamba mkandarasi apatikane ndani ya mwezi mmoja na nusu toka tarehe ya kuvunjwa kwa mkataba huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Benjamin, Mbunge wa Kahama, chini ya usimamizi wa Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan barabara hiyo itakwenda kujengwa na kukamilika ili wananchi wa Kahama waweze kutumia barabara hizo.
MHE. BENJAMIN L. NGAYIWA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kuniona. Ninaomba kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri, kwamba kutokana na kukua kwa shughuli za kibinadamu na kuongezeka kwa idadi ya watu katika Mji wa Kahama, je Serikali ina mpango gani wa kumega eneo dogo la Hifadhi ya Pori la Nkweni ambalo lipo kati ya Kahama na Wilaya ya Ushirombo ili kuwapatia wananchi waweze kufanya shughuli zao za kibinadamu kama ufugaji na kilimo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, eneo ambalo amelitaja kwa sasa, Serikali haina mpango wa kumega kwa ajili ya matumizi ya wanadamu, lakini, kama kuna haja kubwa ambayo anaiona yeye Mheshimiwa Mbunge, basi tukae tu mezani mimi na yeye, twende site tuone. Kama ipo haja ya kufanya hivyo, Serikali inaweza ikachukua hatua siku zijazo.
MHE. BENJAMIN L. NGAYIWA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Wizara, ninaomba sasa nipate uhakika wa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, je, yuko tayari kuambatana na mimi kwenye uzinduzi wa miradi hii ambayo amesema itakamilika mwezi Juni pamoja na kutembelea miradi mingine ya Kilago na Mondo ili kuwapatia wananchi wetu huduma ya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Lukubha kwa kazi nzuri na kuwa sauti imara ya Wanakahama Mjini kwa kuendelea kuwatetea na hasa katika sekta yetu ya maji.
Mheshimiwa Spika, Serikali dhamira yake ni kuendelea kushirikiana na Wabunge wote. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali kupitia Wizara ya Maji, tuko tayari kuambatana naye kwenda kukagua utekelezaji wa miradi; pili, kuhakikisha ubora wa mradi uliokamilika; tatu, kuangalia thamani halisi ya mradi uliotekelezwa. Baada ya hapo uzinduzi wa miradi utatokea katika jimbo lake.
Mheshimiwa Spika, sisi Serikali hasa Wizara ya Maji tutaendelea kushirikiana naye.
MHE. BENJAMIN L. NGAYIWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali lakini nipende tu kuweka swali la nyongeza kwamba Mji wetu wa Kahama umekuwa ni mji ambao unakuwa na changamoto kubwa sana ya kupitika kwa barabara hasa wakati wa masika, Kata ya Majengo, Kata ya Mhungula, Malunga, Nyahanga, Nyasubi, Mhungula na hasa ile barabara ya kuelekea kwenye machimbo kule Mwine ambayo inaingiza fedha nyingi sana Serikalini bado zinakuwa hazipitiki wakati wa mvua.
Sasa nini mpango wa Serikali kwenda kuongeza bajeti ya ujenzi wa barabara za lami kutoka kilometa moja kwa kila mwaka twende kilometa tatu kwa kila mwaka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Benjamin Lukubha Ngayiwa, Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini kwa namna ambavyo amekuwa mwakilishi madhubuti sana wa wananchi wa Jimbo la Kahama Mjini, na mimi nimhakikishie kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI tutahakikisha tunampa ushirikiano wa kutosha ili barabara za Jimbo la Kahama Mjini ziweze kupitika vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika majimbo na manispaa ambazo zimetengewa fedha nyingi kwa ajili ya uboreshaji wa barabara za changarawe na lami Jimbo la Kahama Mjini ni moja ya majimbo hayo. Kwa mfano, kupitia Mradi wa TACTIC hivi sasa ambao tayari tumeshasaini mkataba na kazi zinaanza kuendelea tayari tumetenga shilingi bilioni 22.31 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami Kahama Mjini, kilometa 16.58 ambazo zitajengwa katika maeneo ya eneo la mjini kilometa 12.13, eneo la viwanda Zongomera kilometa 3.08, eneo la kituo cha mabasi na soko kilometa 1.37. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 tumetenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami kilometa moja, lakini pia tumetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za changarawe zaidi ya kilometa 58.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imedhamiria kuhakikisha kwamba Manispaa ya Kahama inakuwa na barabara bora za lami na changarawe na tutaendelea kutenga fedha ili ziweze kujengwa na kuwa na huduma nzuri ya usafiri katika Jimbo la Kahama Mjini.