Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Morris Joseph Makoi (10 total)

MHE. MORRIS J. MAKOI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Ninaomba niulize kwamba hapa Dodoma kuna kiwanda cha mbolea, na hivi karibuni na hapa ninapoongea katika Jimbo la Moshi Vijijini wananchi wanataabika sana kutafuta mbolea ya ruzuku na mbolea mpaka sasa haipatikani kwa ajili ya palizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali inatuambiaje kuhusiana na uzalishaji wa kiwanda cha mbolea hapa Dodoma na kama mbolea ile inaweza ikapelekwa katika Mikoa hususan Kilimanjaro na Jimbo la Moshi Vijijini ili kusaidia kupunguza taabu ya mbolea katika Jimbo lile wakati huu wa palizi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza sana Mbunge kutoka Moshi Vijijini kwa swali lake zuri la kuwatetea Wananchi wa Moshi ambao ni wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakubaliana kwamba tunacho kiwanda kikubwa cha ITRACOM cha hapa Dodoma ambacho kipo maeneo ya Nala. Ni mwekezaji mkubwa wa kimkakati ambaye kimsingi amesaidia sana kupunguza tatizo la mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakiri kwamba bado tuna changamoto katika suala la mbolea na ndiyo maana Serikali tumeweka mkazo kuvutia wawekezaji wa viwanda vya mbolea. Kwa hiyo, ninaomba Mbunge akubaliane nasi kwamba, wakati Serikali inajipanga kuvutia wawekezaji, tutaendelea kutumia viwanda vilivyopo kuhakikisha wakulima wanapata mbolea kwa ajili ya kilimo. Ninashukuru.
MHE. MORRIS J. MAKOI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Nilikuwa ninaomba kama Waziri wa TAMISEMI anaweza akatusaidia kuhakikisha kwamba shule zetu za msingi na sekondari zinatumia mashamba waliyonayo kulima chakula kwa ajili ya kuwapunguzia wazazi hizi gharama za kuchangia, hasa kwa kuzingatia umaskini ambao upo vijijini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri zetu kama Wakurugenzi wakielekezwa, wanaweza wakatenga fedha wakawasaidia wale walimu kununua mbegu na pembejeo nyingine, na wanafunzi wakashirikishwa, wakalima na mwishoni wakavuna chakula cha kutosha na pengine hili jambo la kila mara Serikali inatoa mwongozo, na mwongozo hauzingatiwi lingeweza likamalizika. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge wa Moshi Vijijini, ni ushauri mzuri, lakini nimhakikishie tu kwamba Serikali kupitia mapitio ya Sera ya Elimu ya 2014, Toleo la 2023, limeweka utaratibu mzuri sana wa kuboresha mfumo wetu wa elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakuwa na elimu ya kujitegemea iliyoboreshwa zaidi ambayo itahusisha maeneo ya ujasiriamali, uzalishaji, kilimo, ufugaji, lakini tutakuwa tuna maeneo ya elimu ya amali ya kihandisi na isiyo ya kihandisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tunapoelekea kutekeleza sera mpya ya elimu, haya mambo yote tutayachukua kwa maeneo ambayo wanaweza kufanya shughuli za uzalishaji, watafanya shughuli hizo kujenga uwezo wa watoto, pia kuwezesha kupunguza gharama za michango.
MHE. MORRIS J. MAKOI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Katika Jimbo la Moshi Vijijini, wananchi wamekuwa mstari wa mbele sana kujenga vituo vya Polisi kwa kujitolea na hapa tunapoongea vituo vingi vya Polisi vimekamilika kikiwemo Kituo cha Polisi cha Kata ya Okaoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, Serikali ina mpango gani kuongeza Askari katika vituo hivi katika Jimbo la Moshi Vijijini kwa kuwa vituo vyote ambavyo vimejengwa na wananchi vina Askari mmoja mmoja na wakati…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Makoi, jambo la kwanza unauliza swali la pili. Sasa ni sababu majina hatuyashiki vizuri, kwa hiyo, ungeuliza kifupi zaidi.

MHE. MORRIS J. MAKOI: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi ninaomba niulize moja. Serikali ina mpango gani kuongeza Askari katika vituo mbalimbali vya Polisi katika Jimbo la Moshi Vijijini ambavyo wananchi wamejenga kwa kujitolea?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Morris, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini kwa swali lake la msingi. Kwanza ninampongeza na kuwapongeza wananchi wa Moshi Vijijini kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuunga mkono Serikali kwa ujenzi wa vituo vya Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nimhakikishie kwamba maeneo yote nchini ambayo yatakuwa yamekamilika ujenzi wa vituo na vikawa vimefikia katika vile viwango ambavyo nimevieleza katika majibu ya awali, basi tutaendelea kupeleka Askari kwa mujibu wa uhitaji katika maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. MORRIS J. MAKOI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri na ya kutia moyo ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile barabara ya Rau Madukani - Mamboleo - Materuni - Shimbwe yenye urefu wa kilometa 16.7 ni barabara ambayo ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyowaahidi watu wa Uru Mashariki na Shimbwe kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami kwa maana ya mwendelezo, lakini hiyo barabara ndiyo ambayo inaenda kwenye maanguko makubwa ya maji katika Wilaya ya Moshi na maanguko haya yanachochea sana pato la utalii kwa Halmashauri ya Moshi na wanaingiza karibu shilingi milioni 25 kwa mwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mpango gani pamoja na kukamilisha ahadi ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ina mpango gani kuhakikisha basi barabara hii pamoja na kujenga lami kiwango cha meta 500, 500, ina mpango gani kuhakikisha sehemu inayobaki inapitika muda wote ili kusaidia watalii kufika kwenye maanguko hayo, kuwasaidia wananchi kusafirisha mazao yao, lakini kikubwa zaidi kuchochea uchumi wa wananchi na utalii kwa ujumla?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Wilaya ya Moshi ina vijiji 40 ambavyo vimezunguka Mlima Kilimanjaro. Hivi vijiji 40 ndivyo ambavyo vinabaki na madhila yote ya kuzima moto na mahangaiko yote panapotokea uharibifu ndani ya Mlima Kilimanjaro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mpango gani wa kutenga 20% mpaka 30% ya mapato ya KINAPA au utalii wa Mlima Kilimanjaro kusaidia maendeleo ya vijiji 40 vinavyozunguka mlima kama vile ujenzi wa barabara ambazo zimeharibika sana, lakini vilevile ujenzi wa vyoo katika taasisi za umma ambazo Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, anapigia upatu kwa kiwango kikubwa kuhakikisha kwamba hakuna ukosefu wa vyoo katika shule za sekondari na msingi, lakini pia kukarabati shule za sekondari na msingi katika maeneo hayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ndiyo swali langu la pili.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza, ninampongeza sana Mheshimiwa Morris Joseph Makoi, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini kwa namna ambavyo kwa kweli anafanya kazi kubwa ya kuwasemea Wananchi wa Moshi Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu kwamba Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, siku zote akitoa ahadi na maelekezo yanatekelezwa. Sisi Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, tulishachukua agizo la Mheshimiwa Rais la kujenga barabara hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja na tunafahamu tutakwenda kuijenga kwa awamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari hivi sasa tumeshaiweka kwenye vipaumbele vya Wizara yetu kupitia TARURA kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa awamu ili kuhakikisha kwanza wananchi wanapata huduma bora za usafiri na usafirishaji, lakini pili tunaendeleza na kuboresha huduma za utalii, lakini pia na huduma nyingine kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, ninakuhakikishia barabara hiyo ipo kwenye vipaumbele vya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, ni kweli kwamba Mlima Kilimanjaro unazungukwa na vijiji hivyo takribani 40 na tunafahamu kwamba kuna mashirikiano kati ya wananchi, lakini na taasisi za Serikali na taasisi binafsi. Tunaendelea kuhakikisha kwamba kupitia TANAPA na Wizara ya Maliasili na Utalii, tutaendelea kuongea nao na kuwasiliana nao kuona namna nzuri ya kushirikiana katika kuboresha mazingira ya huduma za jamii, barabara, lakini na mambo mengine kwa vijiji hivi ambavyo vinazunguka Mlima Kilimanjaro.
MHE. MORRIS J. MAKOI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Ninaomba kumwuliza Naibu Waziri atusaidie, Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kukarabati kituo kikongwe cha afya cha Umbwe ambacho kipo Kibosho Magharibi, kituo ambacho kinawanahudumia Tarafa yote ya Kibosho yenye Kata sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, tayari tuna mpango mkakati pale Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhakikisha vituo vya afya kongwe, na hospitali zile kongwe tumezitengea bajeti kwa ajili ya kwenda kuzikamilisha, ikiwa ni pamoja na kurekebisha miundombinu chakavu ili ziendelee kutoa huduma kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa tutaendelea kutenga bajeti ili kukamilisha vituo kongwe kama ambacho amekiongelea.
MHE. MORRIS J. MAKOI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Kagongwa – Igusule - Mwamara mpaka Nzega imeshajengwa mpaka tabaka la tatu kutoka Kagongwa kwenda Igusule kilometa 18.3 kilichobaki ni kuwekwa lami kipande hicho cha kilometa 18.3. tukikiacha kitaharibika.

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali ina mpango gani wa kukamilisha uwekaji wa lami kilometa 18.3 kutoka Igusule kwenda Kagongwa ili kuokoa thamani ya fedha iliyotumika hadi sasa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI K.n.y WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Morris kwa kukumbushia barabara yake muhimu kama ambavyo nimesema kwenye majibu ya msingi, Serikali inayo dhamira ya dhati na inawahakikishia Wabunge wote ikiwemo Mheshimiwa Mbunge huyu miradi yote ambayo tumekwisha kuianza tutakwenda kuikamilisha na ile ambayo tunakusudia kuianza Serikali inakwenda kuikamilisha.

Mheshimiwa Spika, naomba awe na subira kwa kuwa tumeshaonesha nia, Serikali imekwisha anza ujenzi hata kipande hicho Serikali itakwenda kukikukamilisha ili kuwaweza kusikiliza kilio na maombi ya wananchi wa eneo hilo kama ambavyo imewasilishwa na Mheshimiwa Mbunge leo.
MHE. MORRIS J. MAKOI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Mawasiliano kati ya Kata ya Kirima na Kindi yamekatika tangu mwezi wa Nane mwaka 2025. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha za dharura kurejesha daraja la kata hizo mbili ili mawasiliano yaendelee?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, tumepokea maombi ya Mheshimiwa Makoi, Mbunge wa Moshi Vijijini kupitia Meneja wa TARURA wa Wilaya ya Moshi na Mkoa Kilimanjaro na hivi sasa Serikali inaendelea na taratibu za kupata fedha ili kwenda kufanya matengenezo ya barabara hizo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hilo litatekelezwa.
MHE. MORRIS J. MAKOI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Ninaomba niungane na Mheshimiwa Mbunge wa Same, Mheshimiwa Anne Kilango. Mheshimiwa Rais alipokuja Kilimanjaro alitoa ahadi ya kumalizia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, barabara ya Rau Madukani - Materuni Shimbwe yenye kilometa 9.7. Ninaomba kauli ya Waziri ni lini Serikali itamalizia sehemu iliyobaki, kwa sababu sehemu hiyo inasaidia sana utalii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunafahamu hiyo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema. Kama nilivyosema, ninarejea kwamba ahadi za Rais ni kipaumbele namba moja katika utekelezaji wa miradi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba barabara hiyo ya kilometa tisa ipo kwenye mpango hivi sasa, na tutaendelea kuhakikisha tunatafuta fedha mapema iwezekanavyo kwa awamu kuendelea kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili iweze kutoa huduma ambayo inahitajika.
MHE. MORRIS J. MAKOI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Kama ambavyo swali la msingi limesimama, mikopo ya 10% ambayo inatolewa na Halmashauri, inalenga zaidi vijana na wanawake, lakini wakulima wa kahawa ni makundi mbalimbali. Je, Serikali ina kauli gani kwamba mikopo hiyo sasa ijumuishe wazee pamoja na makundi mengine ambayo hayajatajwa kwenye hiyo sheria ya mikopo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mikopo ya 10% ni ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, lakini hao pia ni moja ya makundi ambayo yanafanya shughuli za kilimo. Kwa hiyo, wanaweza wakanufaika kupitia dirisha hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ipo mikopo mingine ambayo haiendi specifically kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Kama ambavyo nimesema, mikopo ya kilimo yenye riba nafuu inakopeshwa kwa wakulima wote; mikopo ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo, Ushirika, na pia mikopo ya Mfuko wa Mikopo ya Pembejeo za Kilimo. Hizi ni fursa ambazo mkulima yeyote anaweza akapata mkopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitumie nafasi hii kuwashauri na kuwahamasisha wakulima ambao hawapo kwenye kundi la wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kutumia fursa za madirisha mengine haya ya mikopo.
MHE. MORRIS J. MAKOI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wakandarasi wa nchi hii wanadai fedha nyingi kama ambavyo ametamka Mheshimiwa Waziri, lakini wakandarasi wa ndani hawaruhusiwi kudai malipo yao pamoja na riba, kinyume na wakandarasi wa nje ambao hudai malipo ya madeni yao pamoja na riba.

Je, Waziri ana kauli gani kuhusiana na madeni ya wakandarasi wazawa wanaodai madeni yao pamoja na riba ili na wao wanufaike au waepuke hasara kama ambavyo wenzao wa nje wanavyoepuka?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nikiri kama Serikali tumeendelea kulipa madeni yakiwemo madeni ya wakandarasi wa kigeni na madeni ya wakandarasi ambao ni wazawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kusema kwenye swali langu la msingi, kwanza hakuna upendeleo wowote baina ya wakandarasi wa nje na wakandarasi wa ndani, kama Serikali tumekuwa tukishamaliza kufanya uhakiki wa madeni hayo tumekuwa tukilipa kwa wakati na hivyo Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini nipende kukuhakikishia kwamba kama Serikali tumejipanga kuhakikisha kwamba madeni yote ya wazawa na wa kigeni yanalipwa kwa wakati.