MHE. YANNICK I. NDOINYO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kabla sijauliza kwa kweli ninatoa shukrani nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza ile ahadi yake ya kutujengea Barabara ya Gamba Gumu kutoka Ngorongoro kwenda kule mbugani Serengeti kwa kuwa ile barabara imeanza. Kwa kweli tunamshukuru sana.
Mheshimiwa Spika, swali langu la nyongeza kwa Wizara hii ya Mifugo, kama ambavyo tunatambua, viwanda ni nyenzo muhimu sana ya kuongeza thamani ya mifugo na kuongeza masoko na kipato cha wananchi wafugaji. Wilaya yangu ya Ngorongoro wananchi wakazi karibu 98%…
SPIKA: Mheshimiwa nenda kwenye swali moja kwa moja.
MHE. YANNICK I. NDOINYO: Mheshimiwa Spika, je, Wizara hii ina mpango gani wa kutujengea kiwanda cha nyama cha kusindika mazao ya mifugo ili kuongeza kipato kama vile inafanya kwa samaki?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, Serikali iko katika utaratibu wa kufanya mambo yafuatayo ili kuhakikisha tunaongeza uwekezaji wa viwanda vya nyama na kuongeza tija kwa wafugaji wetu. Kwanza ni kuendelea kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ili waweze kuwekeza katika sekta hii ambayo kwa kiasi kikubwa ina uwezo wa kuchangia katika pato la Taifa.
Mheshimiwa Spika, pili, tunaendelea kuwahamasisha wafugaji wetu ili kuendelea kufanya ufugaji wa kisasa kuongeza tija na ubora wa mifugo yao ili pindi tunapofanya uwekezaji huu, basi mazao haya tunayoyapata katika mifugo yetu yaweze kuwa na ubora mzuri ili kukidhi soko la ndani na nje katika nchi yetu. Ninakushukuru sana.