Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi ya kuchangia. Ninaanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, nimesimama hapa kwa mara ya kwanza kuchangia, ninaomba kuwashukuru sana Wanawake wa Mkoa wa Mara walionipa nafasi tena ya kuja kuwawakilisha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninaamini nitafanya kazi kwa weledi mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisema kilimo ni uti wa mgongo, ninamaanisha. Ninamaanisha kilimo ni uti wa mgongo kwa sababu, kilimo ni chakula, kilimo ni biashara, lakini kilimo ni ajira, hivyo ninaomba Serikali ipeleke fedha zote zilizoombwa na Wizara ya Kilimo, ili ziende zikatekeleze miradi hii ambayo Wizara ya Kilimo imeomba. Hapa ninampongeza sana Waziri wetu wa Kilimo, Mheshimiwa Daniel Chongolo, anafanya kazi kubwa, nzuri sana iliyo na mfano. Tunasema, Mheshimiwa Rais hakukosea kumpa nafasi hiyo kwa sababu, anaitendea haki. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajielekeza upande wa ushirika. Ninaipongeza sana Serikali yetu kwa namna ilivyowekeza kwa upande wa ushirika. Tumeona namna gani imewekeza kwenye Benki ya Ushirika, zaidi ya shilingi bilioni 50, leo Benki ya Ushirika inafanya kazi. Ombi letu ni kuhakikisha matawi yanaongezeka katika maeneo mengine, ili kufikisha huduma kwa wananchi kwa haraka, ili kusudi ushirika uendelee kuimarika. Ninaomba Serikali ihakikishe inafungua viwanda vile ambavyo ni vya ushirika, ili kuendelea kuongeza chachu ya mazao, ushindani ndani ya ushirika, mazao yetu yaweze kupata soko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, wamefungua Kiwanda cha Mbogwe kinafanya vizuri, Kiwanda cha KACU kinafanya vizuri na pale Simiyu kinafanya vizuri, lakini kuna viwanda vingine bado tunatamani viende vikafunguliwe. Kiwanda kama cha Nyanza Cooperative Union, Kiwanda cha Mara Cooperative Union, Kiwanda cha SHIRECU Cooperative Union ni viwanda vilivyokuwa vinafanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Mkoani Mara, Kiwanda cha Mara Cooperative Union kilikuwa kinafanya vizuri sana na pamba ile ilikuwa ni pamba safi, pamba iliyokuwa inapendeka Tanzania Bara na Afrika kwa ujumla. Kwa hiyo, ninamwomba Mheshimiwa Waziri Kiwanda kile cha Mara Cooperative Union aende akakifufue, ili kusudi wananchi wa Mkoa wa Mara na wenyewe waweze kupata ajira. Kaka zetu na wananchi wa Mkoa wa Mara kwa ujumla waweze kuongeza pato katika mkoa wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ninamwomba Mheshimiwa Waziri, upande wa bei ya tumbaku. Bei ya tumbaku imekuwa sasa siyo bora kwa wakulima na hapa ninampongeza sana kaka yetu Stanley, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku, anaendelea kufanya vizuri, changamoto hizi za bei ya tumbaku aziangalie. Wakulima wa Serengeti wamekuwa wanapata changamoto ya bei hizo kwa sababu, kwa sasa wanauza kwa Dola 1.4 mpaka Dola 1.5, lakini wamezalisha kwa Dola 1.6. Hii siyo sahihi kwa sababu, wamekopa mikopo wanatamani warudishe, hii itaenda kuwaletea hasara kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba; wazo langu hapa na ushauri ni tuangalie namna bora ya kuziangalia pembejeo. Tukae, tuangalie bei za pembejeo, ili kusudi tuweze kuwasaidia hawa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini pia, ninaendelea kumpongeza Mheshimiwa Daniel Chongolo, Waziri wetu, katika hii stakabadhi ghalani. Stakabadhi ghalani ni maono ya Mheshimiwa Rais, ameenda vizuri na sasa wanaendelea kufanya vizuri katika kuwajali wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu hapa ni tupeleke elimu, ili wakulima waweze kujua namna bora ya kutumia mfumo huu wa stakabadhi ghalani kwa sababu, tunaenda kuwaondolea ile adha ya madalali waliokuwa wanawasumbua, ili kusudi wakulima waweze kupata bei nzuri na huu mfumo uendelee kufanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa mbolea.
MWENYEKITI: Muda wako umekwisha, Mheshimiwa.
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. GHATI Z. CHOMELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi ya kuchangia. Nami pia nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya katika nchi yetu na hasa kwa kuhakikisha anaendelea kumtua mwanamke wa Kitanzania ndoo kichwani kama dhamira yake inavyojieleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, kwa kazi nzuri anayoifanya katika kumsaidia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Wizara hii ya Maji yeye pamoja na Naibu Waziri na Katibu Mkuu wetu wa Maji, dada yetu mahiri sana, mchapa kazi Eng. Mwajuma na Watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami pia sitaacha kuwapongeza sana Watendaji wa Wizara hii katika Mkoa wangu wa Mara kwa namna wanavyopambana kuhakikisha wanamtua ndoo mwanamke wa Mkoa wa Mara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, bado kuna changamoto katika Mkoa wetu wa Mara. Tunashukuru sana kwa miradi ambayo imeletwa katika Mkoa wetu wa Mara, tumepata miradi 77 ya maji lakini miradi hiyo ina thamani ya shilingi bilioni 265 ambayo itaenda kuwanufaisha wananchi 985 katika Mkoa wetu wa Mara. Pia, tumepata miradi sita mipya ya maji yenye thamani ya shilingi bilioni 1.6. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi tunapokea, tatizo kubwa tulilonalo katika Mkoa wetu wa Mara ni kutokukamilika kwa miradi. Mimi ninaomba Waziri utakapokuja kuhitimisha hoja yake atuambie miradi hii ambayo ametupatia Mkoa wa Mara itakamilika lini? Hili ni tatizo kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2024 tulisaini mradi wa maji wa miji 28 wa shilingi bilioni 134. Fedha hizo mpaka sasa mradi wa maji wa miji 28 haujakamilika, uko 15%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ambao tulisaini nao mradi huu, wao wako 80% na wengine 70%, lakini sisi 15%. Hii ni aibu kubwa sana. Tumezunguka kwa wananchi wa Mkoa wa Mara, akinamama wa Mkoa wa Mara tumewaambia dhamira njema ya Rais ya kuwatua ndoo kichwani, lakini mpaka sasa mradi ule mkandarasi hayupo site, mradi haujakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Wana-Mara tutaondoka na shilingi ya Mheshimiwa Waziri ili kusudi aje atuambie ule mradi utakamilika lini? Mkandarasi atalipwa lini? Mradi ule ukikamilika utaenda kuwasaidia mama zangu wa Wilaya ya Rorya, wa Wilaya ya Tarime Mjini na Jimbo la Tarime Vijijini baadaye na Serengeti. Hizi ni Wilaya ambazo zinateseka sana suala la upatikanaji wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vijiji vingi havina maji. Mheshimiwa Waziri, ametembelea Mkoa wa Mara, amejionea namna gani akina mama wanateseka, lakini kuna sehemu tunashukuru amezigusa, ninaomba atakapokuja hapa atuambie ni lini mkandarasi wa mradi ule atapewa fedha ili aweze kukamilisha ule mradi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuipongeza Wizara hii. Tuliwahi kupata shilingi bilioni 70 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Mgango - Kiabakari na sasa ule mradi unaendelea kufanya vizuri, ila kuna kata moja ambayo ndiyo ule mradi umepita, Kata ya Tegeruka. Jamani changamoto ya pale ni mabomba. Ninaomba mradi ule mabomba yapelekwe ili Kata na vijiji vile ambavyo viko pale viweze kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, ninaunga mkono hoja. (Makofi)