Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Chiku Athuman Issa (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. CHIKU A. ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kuniwezesha pia kusimama leo kuweza kuchangia katika Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa na political will yake iliyokuwa kubwa ya kuiangalia Wizara ya Kilimo. Tumeona tangu ameingia madarakani bajeti imekua kutoka shilingi bilioni 294 na sasa tunaenda shilingi trilioni 1.1. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana Mawaziri: Waziri Daniel Chongolo pamoja na Msaidizi wake Ndugu Silinde na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa mnayoendelea kuifanya. Mimi kwa sababu ya muda nitaongelea mambo mawili, na kama muda utaniruhusu nitaongelea benki ya ushirika ambayo inamiliki 51%. Pia, muda ukiniruhusu nitaendelea kuongelea Tume ya Maendeleo ya Ushirika zaidi kwenye taarifa za ukaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kuanzisha Benki ya Ushirika nchini. Benki hii inaenda kuwa mkombozi wa wakulima katika nchi yetu. Katika muda wa mwaka mmoja Benki hii imefanya mambo makubwa sana, lakini zaidi ya hayo Serikali yenyewe imewekeza kiasi cha 10% katika Benki hii, baada ya Serikali kuwekeza, wananchi kuwekeza pamoja na wanaushirika wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa wanaushirika, wamepewa 51% kwa makusudi makubwa ili waweze kuimiliki Benki yao wao wenyewe. Unapomiliki kitu chako, una uwezo wa kuhakikisha kwamba unakiendesha kwa jinsi ambavyo kinaenda kukusaidia zaidi kama mkulima. Tuna benki nyingi nchini, tukiongeza na Benki hii ya Ushirika tunaenda kupata mikopo. Ni Benki pekee sasa hivi ambayo inaweza kutoa riba ya single digit ya asilimia tisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki hii katika kipindi cha mwaka mmoja mizania yake imetoka shilingi bilioni 49 ikaenda shilingi bilioni 176. Amana zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 15 kwenda shilingi bilioni 114. Mikopo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 14 kwenda shilingi bilioni 104. Tunaiomba Serikali iishike mkono Benki hii. Pia, ningependa kutoa ushauri katika 51% ambayo Benki hii imepewa, wakulima pamoja na wanaushirika, wana deficit ya kufikia hiyo 51% kwa kiasi cha shilingi bilioni saba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri kupitia Tume ya Ushirika, tuwahimize wanaushirika wakamilishe mtaji wao uweze kufikia shilingi bilioni saba. Pia, ninamshukuru Rais, baada ya Benki kuanza kazi ilikuwa na deficit ya shilingi bilioni tano. Menejimenti, bodi pamoja na Tume ya Ushirika ilimfuata Rais na kuomba iwaongezee wanaushirika shilingi bilioni tano, Rais amefanya hivyo. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kuona umuhimu wa chombo hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na Benki ya Ushirika ambayo imebadilika, na sasa inaitwa CRDB. Makosa yale yaliyofanyika kipindi kile yasirudiwe. Tunaomba watendaji, usimamizi, ukaguzi na bodi iweze kuisimamia hii benki kwa weledi. Ninaishukuru Benki ya CRDB ambayo imewekeza pia 20% katika benki hii. Ukiona benki kubwa kama CRDB inawekeza katika benki ya namna hii, jua kuna jambo kubwa na wana maono makubwa na wanatoa support kubwa kuhakikisha benki yetu hii inaenda kusimama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali, katika ile 10% kulibakia fedha kidogo ambayo Serikali ilikuwa haijaimalizia ya shilingi milioni 800. Tunaiomba Serikali basi imalizie ili kuweza kui-support benki yetu iweze kusimama na kufanya kazi vizuri na kwa weledi zaidi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)