Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Tinnar Andrew Chenge (10 total)

MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Chenge Sekondari iliyopo Kata ya Somanda pale Bariadi ilijengwa kwa nguvu za wananchi tangu mwaka 2016, na kuna maabara ambayo ni two in one, lakini tangu kipindi hicho shule hiyo na maabara hiyo bado haijakamilika. Je, ni lini Serikali itakwenda kukamilisha maabara hiyo ili kuunga mkono juhudi za wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwanza Serikali inatambua mchango mzuri wa wananchi wa Jimbo la Bariadi na Bariadi Mjini kwa kuchangia nguvu zao kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Secondari ya Chenge. Nakuhakikishia kwamba, Serikali ilishafanya tathmini, na tunayo orodha ya shule zote ambazo zimejengwa kwa nguvu za wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule zote ambazo zimejengwa kwa fedha ya Serikali, kwa maana ya Halmashauri, yaani Serikali Kuu, tayari tunafahamu upungufu wa majengo na miundombinu inayohitajika. Tunaendelea na taratibu za fedha, ili tuweze kupeleka kukamilisha shule hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Shule ya Sekondari ya Chenge itapewa kipaumbele. Itapelekewa fedha ili tuhakikishe miundombinu hiyo inakamilishwa.
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Kumekuwa na changamoto ya kukatikakatika umeme katika Mkoa wa Simiyu, na Serikali iliahidi kutoa fedha kwa ajili ya kujenga kituo cha kupozea umeme. Je, ujenzi huu umefikia hatua gani? Lini utakamilika ili kuondoa changamoto hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuendelea kufuatilia namna ambavyo Wizara ya Nishati inaendelea kutekeleza majukumu ya ujenzi wa substation katika eneo la Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi inaendelea na mpaka sasa ujenzi wa substation umefika zaidi ya 30%. Ninamwomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira. Ninamhakikishia mara baada ya substation hiyo kukamilika, Mkoa wa Simiyu utakuwa umeondokana na changamoto ya kukatikakatika kwa umeme. Ahsante.
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Shule ya Sekondari Busangwa iliyopo Kata ya Sakasaka katika Jimbo la Kisesa ina wanafunzi wa kike takribani 250, lakini hakuna mwalimu wa kike hata mmoja. Je, ni lini Serikali itapeleka walimu wa kike? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaomba nipokee hoja ya Mheshimiwa mama yangu, Mheshimiwa Mama Chenge, lakini nitoe tu ufafanuzi ili kuweka rekodi sawa kwamba tunafahamu umuhimu wa walimu wa kike katika shule zetu zote za wanafunzi wa kiume na wa kike. Tunafahamu pia kuna mahitaji maalum ambayo mara nyingine ni vizuri mwalimu wa kike akiwa katika shule hizo. Kwa hiyo, suala hilo tumelichukua na tutakwenda kulifanyia kazi. (Makofi)
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kuniona. Kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Simiyu, ninaomba kuulizwa swali la nyongeza. Ni lini Serikali ina mpango wa kujenga Kituo cha Afya cha Bunamhala Wilaya ya Bariadi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza kuhusu Kituo cha Afya Simiyu, Bariadi. Katika vile vituo vyetu vya kimkakati Majimbo 94 na yale Majimbo mapya pamoja na Halmashauri ya Wilaya Simiyu na wao ni wanufaika, watakwenda kupata kituo cha afya. (Makofi)
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni sera ya Serikali kuhakikisha kwamba kila makao makuu ya mkoa yanaunganishwa na mikoa jirani kwa barabara za lami. Je, ni lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Bariadi na Gangabilili – Mwanhuzi – Sibiti - Iguguno na Singida? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, hili swali linafanana na swali la msingi kwa sababu ndiyo barabara ambazo zinatakiwa zijengwe zote. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa kwa awamu hii tumepanga kujenga kiwango cha lami kilometa 50 katika hiyo barabara ya Bariadi – Sibiti kuja Singida.

Mheshimiwa Spika, tayari tuna mkandarasi, na tunachosubiri ni kulipa malipo ya awali ikiwa ni pamoja na kujenga barabara kwa kiwango cha lami katika lile daraja la Sibiti ambapo kutakuwa na upande wa Sibiti kwa maana ya Simiyu na upande wa Singida, ahsante.
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali italipa madeni ya wakandarasi wa Wilaya ya Meatu ambayo yameshafanyiwa uhakiki na kutumwa TAMISEMI na Hazina kwa ajili ya malipo? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. ENG. MSHAMU A. MUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nijibu kwa ujumla.

Mheshimiwa Tinnar Chenge ninashukuru sana kwa swali lako lakini niseme wazi kwamba amesema madeni ya Wilaya ya Meatu. Hayo ni madeni jumuishi ambayo haijulikani sasa ni wakandarasi wa Wizara ya Maji au miradi ya barabara au ni miradi gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongea naye nje ya forum hii ili kupata uhakika na specific hoja yake iko vipi ili tuweze kumjibu kiuhalisia kutokana na swali ambalo atakuwa ametupatia nje ya kikao hiki. (Makofi)
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ninakushukuru. Kwa kuwa ni Sera ya Serikali ya Kuwainua Wanawake Kiuchumi kupitia mikopo ya 10%, je, Serikali ina mpango gani wa kufikisha elimu juu ya mikopo yenye riba nafuu inayotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii kwa wanawake wa vijijini Mkoa wa Simiyu?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, majibu.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, sijasikia vizuri.

MWENYEKITI: Mheshimiwa, ni kuhusu mikopo ya wanawake Simiyu, majibu kwa ufupi.

MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango gani wa kufikisha elimu ya mikopo yenye riba nafuu inayotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii kwa wanawake wa vijijini wa Mkoa wa Simiyu? Ninashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii tunafanya kazi kwa pamoja katika maeneo ya makundi maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge Wizara ya Maendeleo ya Jamii inaendelea pia kuwafikia wanawake na makundi yale ambayo yanahitaji kupata mikopo hiyo kutoa elimu juu ya upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu. Kwa hiyo, Ofisi ya Waziri Mkuu tumelichukua hilo. Tutakaa kwa karibu zaidi na Wizara ya Maendeleo ya Jamii ili kuendelea kuboresha mbinu za kuwafikia akina mama na kujua kwamba kuna fursa za mikopo hiyo.
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa shule ya Sekondari ya Wasichana ya Simiyu ina wanafunzi ambao wana ulemavu, je, ni lini Serikali itatatua changamoto ya miundombinu wezeshi ili wanafunzi hawa, waweze kwenda darasani na hasa katika kipindi cha mvua?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Tinnar Chenge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza miundombinu ya shule na miundombinu inayotoa huduma katika jamii zetu, yote imejengwa ili iweze ku-accommodate walemavu katika jamii zetu. Kwa hiyo, nimwelekeze mkurugenzi, afike katika shule ambayo Mheshimiwa Mbunge ameiainisha, ili kwanza kujiridhisha kama kweli miundombinu haipo; na kama haipo achukue hatua za dharura kuweza kuweka miundombinu hii, ili vijana wetu walemavu wanaopata elimu katika shule hizi waweze kupata elimu bila changamoto yoyote. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Bariadi ni Makao Makuu ya Mkoa wa Simiyu, na kwa kuwa, mji huu unakua kwa haraka sana, je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga soko kwa maana ya Machinga Complex kwa ajili ya wajasiriamali wa Mkoa wa Simiyu?

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, mkipiga makofi kabla Mbunge hajauliza swali, Mheshimiwa Waziri hawezi kusikia. Kwa hiyo, Mheshimiwa Tinnar ninaomba urudie swali lako.

Waheshimiwa Wabunge tuwe wavumilivu. Tupige makofi baada ya majibu.

MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Bariadi ni Makao Makuu ya Mkoa wa Simiyu, na kwa kuwa mji huu unakua kwa kasi sana; je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga soko, kwa maana ya Machinga Complex, kwa ajili ya wajasiriamali wa Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Bariadi kwanza ni miongoni mwa halmashauri ambazo ziko kwenye Mpango wa TACTIC. Ninafahamu kwamba, soko la pale Mjini Bariadi limeingizwa kwenye Mpango wa TACTIC na hatua zimeanza kutekelezwa. Kwa hiyo, pale litajengwa soko la kisasa sana kwa ajili ya Halmashauri ya Mji wa Bariadi ambapo ni Makao Makuu ya Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumepokea ombi la Mheshimiwa Mbunge la kuhitaji kujenga Machinga Complex. Tutafanya tathmini na kuona uwezekano wa kufanya hivyo.
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Kwa kuwa Hospitali ya Mkoa wa Simiyu ni hospitali ya rufaa, na kwa kuwa hospitali hii haina daktari bingwa wa mifupa, je, ni lini Serikali itapeleka daktari bingwa wa mifupa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Mama yangu, Mheshimiwa Chenge kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuwapigania wananchi wa Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Simiyu ni moja ya hospitali inayotoa huduma za kibingwa, na hospitali hii inatoa huduma za kibingwa sita. Ninaomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa ajira za watumishi ili kukabiliana na changamoto za watumishi na hasa watumishi bingwa. Hivyo pindi watakapopatikana na kupata kibali cha ajira, basi hospitali hii ya Simiyu itapelekewa mtaalamu huyu wa mifupa ili wananchi waweze kupata huduma hizi za kibingwa za mifupa karibu na mkoa wao. Ninaomba kuwasilisha.