MHE. REGINA H. MIKENZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninapenda kuuliza swali. Ni lini Kituo cha Afya cha Kata ya Rwamgasa kitakamilishwa na kuanza kutoa huduma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifika katika Kituo cha Afya cha Rwamgasa na kiukweli kimeanza kutoa huduma za OPD na kuna majengo yanazidi kuongezwa pale kupitia mbia wetu wa Buckreef, na majengo haya yanakwenda kukamilika ndani ya mwezi wa tatu na kuanza kutoa huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshatoa maelekezo mahususi kwa Mkurugenzi kufuatilia kwa ukaribu katika ujenzi wa majengo haya ili akina mama wetu wanaojifungua zaidi ya 200 mpaka 250 kwa mwezi waweze kupata huduma hii ya afya ya msingi. (Makofi)
MHE. REGINA H. MIKENZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niulize swali la nyongeza. Wilaya ya Nyang’hwale ndiyo Wilaya pekee katika Mkoa wa Geita ambayo haina barabara yoyote ya kiwango cha lami inayounganisha Wilaya hiyo na Wilaya nyingine ikiwemo Makao Makuu ya Mkoa wa Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lini Serikali itatujengea barabara kwa kiwango cha lami katika Wilaya hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Mbunge na ninatambua kwamba hili swali tumelijibu mara kadhaa kuhusu barabara ya lami aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge. Barabara hii ipo kwenye utaratibu kwa sasa wa kuisanifu kuanzia Busisi – Ngoma - Nyang’hwale hadi Nyambura na pia kutoka Nyang’hwale kwenda Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilisha usanifu, gharama zitajulikana, na sasa ndiyo tutakuja na mpango wa kuijenga kwa kiwango cha lami, ahsante.