MHE. COSMAS M. BULALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa Wizara ya TAMISEMI. Mji wa Ng’hungumalwa ni wa kibiashara katika Wilaya ya Kwimba. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza ujenzi wa soko la kisasa katika kata hii na Mji wa Ng’hungumalwa, ambapo mwaka 2025 iliidhinishwa shilingi bilioni 3.9, kwa ajili ya kujenga stendi katika Mji wetu wa Ng’hungumalwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, miundombinu hiyo ni kipaumbele cha Serikali. Serikali inatambua uhitaji wa miundombinu hiyo, kwa hiyo, tutaendelea kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge na halmashauri kuhakikisha tunaanza kutenga fedha kwa awamu na kuhakikisha kwamba, tunajenga miundombinu hiyo.
MHE. COSMAS M. BULALA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Hungumalwa Jimbo la Kwimba ni kitovu cha biashara ya ukusanyaji, usafirishaji na usambazaji wa mazao kwenye Mkoa wa Mwanza ambao unategemewa na wilaya jirani za Kishapu, Shinyanga Vijijini, Misungwi, Magu na Shinyanga Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini hasa tathmini hiyo itafanyika na kukamilika; na kwa sababu tayari wananchi wa Kijiji cha Hungumalwa wameshatenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa ghala ili utekelezaji wa mradi huo uanze?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Wiki iliyopita kumetokea janga katika Vijiji vya Buyogo na Mwang’ombe kwenye Kata ya Hungumalwa ambapo mvua kali ya mawe imenyesha na kuharibu mazao kama mtama, viazi pamoja na mpunga uliopo mashambani. Je, Serikali ina mpango gani wa dharura kwenda kusaidia wananchi walioathirika na mafuriko haya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza Mheshimiwa Cosmas Bulala, Mbunge wa Jimbo la Kwimba, kwanza, kwa maswali yake ya msingi, na pili, kwa ufuatiliaji ambao amekuwa akiufanya muda wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo maja, tunatambua umuhimu wa Mji wa Hungumalwa na tunatambua biashara kubwa inayofanyika pale na nimthibitishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika mwaka wa fedha huu tunaokwenda kuuanza, Serikali itafanya tathmini katika eneo hilo. Baada ya tathmini, tutatafuta fedha ambayo nimhakikishie kwamba tutajenga ghala ambalo litawasaidia wananchi wake katika eneo la Hungumalwa ambao wapo katika Jimbo la Kwimba. Kwa hilo, nina uhakika nalo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu changamoto ambayo imetokana na mvua, nimwambie tu kwamba Wizara ya Kilimo tutashirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu ambao ndio wana jukumu kubwa la kuratibu maafa na wakati wanafanya ule uratibu, kila Wizara ina jukumu lake. Kwa hiyo, tukishamaliza jukumu hilo ninaamini Serikali chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan itapeleka msaada katika eneo hilo kwa wananchi ambao wamekutwa na maafa hayo, ahsante sana.