Primary Questions from Hon. Ester Edwin Malleko (4 total)
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha fedha za TASAF zinawafikia walengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu. Kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani yake kubwa kwangu kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Ahadi yangu kwake ni kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa kujituma, na kwa uzalendo, ili malengo yaliyopangwa yafikiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, sasa naomba nijibu swali la Mheshimiwa Esther Malleko, Mbunge wa Viti Maalum.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia program ya TASAF, imeweka mkakati mahususi wa kuhakikisha fedha/ruzuku zinawafikia walengwa kupitia matumizi ya mfumo wa malipo ya kielektroniki (e-payments) unaolenga kuongeza uwazi, usalama na ufanisi katika utoaji wa ruzuku kwa walengwa. Mkakati huo unatekelezwa kwa kutumia watoa huduma za kifedha walioidhinishwa ambao hulipa fedha moja kwa moja kwenda kwa walengwa kupitia akaunti zao za benki na mitandao ya simu.
Mheshimiwa Spika, mfumo huu huondoa utaratibu wa kutuma fedha taslimu, na hivyo kupunguza mianya ya upotevu, ucheleweshaji au matumizi yasiyo sahihi ya fedha. Pili, malipo yote hufanyika kwa kuzingatia taarifa za walengwa zilizohakikiwa katika mfumo wa usimamizi wa walengwa, Management Information System (MIS), ambapo kila mlengwa hulipwa kulingana na utambulisho wake wa kipekee, ahsante.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa hoteli katika Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha uandaaji wa pembuzi yakinifu ya ujenzi wa Hoteli ya Nyota Nne katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro. Kwa sasa taratibu za kutafuta mwekezaji wa ujenzi wa hoteli zinaendelea.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza upatikanaji wa mbegu bora na kwa bei nafuu nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuongeza uzalishaji wa mbegu nchini kwa kutenga maeneo kwa ajili ya kuanzisha mashamba mapya ya kuzalisha mbegu, kuhamasisha kampuni binafsi za mbegu kuingia mikataba maalum na ASA ili kuzalisha mbegu bora kwa kutumia mashamba ya Serikali, na kuhamasisha uzalishaji wa mbegu za daraja la kuazimiwa ubora kwa maana ya Quality Declared Seeds – QDS kwa wakulima wadogo ili kuwaruhusu wakulima kuzalisha na kuuza mbegu zinazofaa kwenye maeneo husika kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuimarika kwa uzalishaji wa mbegu nchini kutasababisha kupungua kwa ongezeko la bei linalotokana na uagizaji wa mbegu nje ya nchi. Vilevile, Wizara inaendelea kutekeleza azma ya Serikali ya kutoa ruzuku ya mbegu bora ya mazao ya kimkakati.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza skimu za umwagiliaji katika Mkoa wa Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Maleko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuchukua jitihada mbalimbali za kuendeleza sekta ya umwagiliaji nchini ikiwemo katika Mkoa wa Kilimanjaro. Katika kutekeleza hilo, mwaka 2025/2026, miradi 42 ya umwagiliaji inatekelezwa katika Mkoa wa Kilimanjaro ikijumuisha ujenzi na ukarabati wa skimu 15 zenye jumla ya hekta 18,154.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya skimu hizo, skimu nane ni za ujenzi zenye jumla ya hekta 9,514 ambapo utekelazaji wake umefikia wastani wa 28%. Aidha, miradi ya ukarabati ni saba ambapo utekelezaji wake umefikia wastani wa 45%. Kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa miradi hiyo kutawezesha kumwagilia eneo lenye ukubwa wa hekta 18,154 na kunufaisha wakulima 283,877.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa miradi ikiwemo Bonde la Mtambo lenye miradi ya Kikavu chini, Mapacha, Mtambo, Ismail na Ngosero (Mpenda Roho na Longoi) yenye jumla ya hekta 8,500. Aidha, miradi 18 ya skimu zenye zaidi ya hekta 29,000 usanifu wake unaendelea.