Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. YOHANA S. MSITA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza jioni hii. Ninaomba nichukue nafasi hii tena kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia afya na uzima, lakini kuwashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Itigi kwa kuendelea kuniombea, ninawaahidi kuitenda kazi kama inavyotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya katika Sekta ya Maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza pia kijana mahiri kabisa Mheshimiwa Jumaa Aweso pamoja na Naibu wake na Katibu Mkuu. Kwa kweli Wizara hii ya Maji wanaitendea haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona ari na nguvu na moyo walionao wa kufanya kazi. Changamoto ambayo ninaiona ni upatikanaji wa fedha. Tunakubaliana sote hapa kwamba maji ni uhai; pasipo maji hakuna maisha. Sasa, kama ndivyo Wizara hii ya Maji lazima tuipe kipaumbele sana, tuhakikishe fedha zote ambazo zinatakiwa kufika ndani ya Wizara hii zinafika kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mkoa wa Singida bajeti iliyopita ilitengewa jumla ya shilingi 10,000,000,000 kwa ajili ya maji. Mpaka kufikia mwezi Machi ilishapokea jumla ya shilingi bilioni 1.6 tu pekee. Hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba, miradi mingi ya maji haijatekelezeka. Katika Jimbo la Itigi viko vijiji havijawahi kuonja ladha ya safi na salama, kwa maana ya maji ya bomba. Vijiji kama Ipangamasasi Kata ya Idodyandole, Mnazi Mmoja, Tulieni, Kalangali, Chabutwa, Ipalalyu na Mgandu, vijiji hivi havina miundombinu kabisa ya maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaomba Serikali, tunapoipitisha bajeti tujitahidi kutafuta vyanzo vya fedha ili miradi hii ya maji iweze kukamilika na miundombinu iweze kujengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Itigi lina changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa maji chini ya ardhi. Mitambo imekuja na ninawashukuru watu wa Wizara. Mitambo imekuja imechimbwa; vijiji ambavyo maji hayajapatikana, Vijiji kama vya Mtakuja, Makale, Kayui, Chagutwa, Kintanula, Itagata, Mwamagembe, vijiji hivi lazima tuje na njia mbadala tuone namna gani tunaweza kuwasaidia wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vimechimbwa visima vingi, lakini maji hakuna. Sasa, inawezekana labda mitambo yetu uwezo wake ni mdogo, aidha, tunachimba mita ni chache zaidi. Tuje na mkakati mahsusi tuhakikishe kwamba vijiji hivi vinapatiwa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo la Itigi upatikanaji wa maji safi na salama ni 66% bado tuko chini. Ninaomba watu wa Wizara watuangalie kwa macho mawili, tuna changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa maji katika Jimbo langu la Itigi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema tunayo mito, tunayo mabonde na kadhalika. Huu mpango wa kuchimba mabwawa, ninadhani kwenye Jimbo la Itigi uelekezwe kwa kasi kubwa sana, kwa sababu chini ya ardhi sehemu nyingi hatupati maji. Maeneo kama ya Mbugani, Doroto, Kitaraka, Itagata, Makale, maeneo ambayo maji hayapatikani, tuchimbe mabwawa yaweze kupunguza adha ya upatikanaji wa maji. Maji ya binadamu, lakini sisi Jimbo la Itigi pia ni wafugaji wazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninawaomba sana, suala la uchimbaji wa mbwawa katika Jimbo la Itigi lipewe kipaumbele ili tuweze kuwasaidia wananchi wetu pamoja na mifugo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la vitendea kazi; Jimbo la Itigi hivi ninavyozungumza watu wa Maji pale Itigi Mjini wanayo pikipiki moja. Ile ni halmashauri, angalau basi tuongezewe pikipiki angalu zifike hata nne, lakini tupatiwe na gari ili watendaji wetu waweze kufanya kazi zao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, ninaiomba sana Wizara watuangalie watu wa Jimbo la Itigi kwa macho mawili ili tuweze kufika zile asilimia ambazo kwa mujibu wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inatutaka tufike, hasa kwenye majimbo ya vijijini katika ile 85%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)