MHE. YOHANA S. MSITA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, ni lini Serikali itapeleka wataalam kwenye Jimbo la Itigi kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wetu wa dengu ili waweze kuongeza tija zaidi kwenye zao la dengu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Waziri atakuwa tayari kuongozana na mimi kwa ajili ya kwenda kuongea na wale wakulima kwa sababu wana mambo mengi sana? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nami nimpongeze Mheshimiwa Yohana Msita, Mbunge wa Itigi, ameanza vizuri kazi yake ya Ubunge, ni Mbunge mpya lakini unauona umakini wake. Nimthibitishie tu kwamba, moja, Serikali tutaendelea kupeleka wataalamu, lakini wale waliopo sasa hivi maafisa ugani, tutaongeza msukumo ili kuhakikisha wanafanya hiyo kazi kama ambavyo imekusudiwa kwa sababu lengo letu ni kuongeza tija ya zao hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, mimi niko tayari kuongozana naye katika Jimbo la Itigi, uzuri hapa siyo mbali tunaweza tukaenda na kurudi. Kwa hiyo, niko tayari muda wowote ambao yeye Mheshimiwa Mbunge atakuwa na hiyo ratiba.