Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Asha Juma Feruz (1 total)

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. ASHA J. FERUZ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii na mimi niweze kuchangia katika hoja iliyopo Mezani ya Mpango wa Serikali. Nachukue nafasi hii kwanza kabisa ikiwa ni mara yangu ya kwanza kusimama na kuchangia, nawashukuru sana wapigakura wangu, Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa UWT Taifa, kwa kunipa ridhaa kwa kura nyingi niweze kusimama hapa kuwa mwakilishi ninayewakilisha kundi la Vyuo na Vyuo Vikuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nakishukuru sana chama changu pendwa, Chama Cha Mapinduzi, kwa kuniteua kuwa mwakilishi katika nafasi hiyo ndani ya Bunge lako Tukufu. Ninachukua nafasi hii pia, kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa ushindi mkubwa alioupata katika Uchaguzi Mkuu tulioufanya Oktoba, 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nachukua nafasi hii pia, kuwapongeza Mawaziri wote tukiamini kwamba, sisi ni timu moja. Wao wako mbele kumsaidia Mheshimiwa Rais kutimiza malengo na mahitaji ya wananchi wanayoyatarajia katika Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najielekeza katika mchango wangu. Kama alivyowasilisha Waziri wa Mipango asubuhi, amesema kuwa, mpango huu umeandaliwa kutokana na Hotuba ya Rais, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na matamko ya viongozi ambayo ndiyo kiu ya wananchi ambao ndiyo tunawawakilisha humu ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupitia mpango huu mimi najielekeza katika maeneo matatu; eneo la kwanza ni ajira kwa vijana. Katika sensa tuliyoifanya, nguvu kazi ya Taifa ni watu 25,000,000 lakini katika watu 25,000,000 milioni 14,000,000 ni vijana, sawa na 55.6%. Nini mchango wangu sasa ninaotaka kuusema? Katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi, ukurasa wa 21, Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake ambayo imeundwa kimejielekeza kutengeneza ajira 8,500,000. Sasa Serikali kwa mpango huu mzuri waliotuletea ninaomba kutoa ushauri kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuwasaidia vijana katika maeneo yetu tunaowawakilisha hapa waweze kupata ajira rasmi na zisizo rasmi, tuisadie Wizara ya Ajira. Pamoja na Wizara ya Vijana kuweza kupata taasisi chache ambazo zitakuwa na kazi ya kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa vijana, ili vijana hawa watakapotoka kwenye hizo taasisi ama vyuo tupate positive impact kwa muda mfupi kwenye jamii zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, naishauri Serikali kutoa mafunzo mahsusi, ikiwemo ujuzi wa fani adimu (real skills) kwa vijana, ili kupata fursa za ajira ndani na nje ya nchi. Nchi yetu ina miradi mingi ya kimkakati, nikitoa mfano Mradi wa Bomba la Mafuta, zipo kazi tunasema kwa Kiswahili chepesi, mafundi mchundo. Hawa ni watu wanaohitajika sana. Hatuna sababu ya kwenda kuchukua watu hawa nje, ili waje wafanye kazi zile hali ya kuwa sisi tuna vijana wengi ambao bado hawajapata ajira. Kwa hiyo, tutumie ombwe hilo kuweza kuwapa vijana wetu ajira za ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nichangie kuendeleza kuzisaidia sekta binafsi, kuwawekea mazingira bora na mazuri ya kukuza mitaji yao, ili waweze kutoa ajira kwa vijana wetu. Kuwa na utaratibu maalumu wa knowledge transformation kutoka kwa wafanyakazi wa kigeni kwenda kwa wafanyakazi wa ndani, wazawa. Hii itatusaidia kupunguza kuajiri watu kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe na mkakati wa kuanzisha na kuendeleza viwanda vidogo vidogo vijijini na kukuza ongezeko la thamani katika sekta za kimkakati ikiwemo uvuvi, misitu, kilimo na mifugo. Kufuatia hayo niliyoyachangia kwenye eneo la vijana tutakuwa tunajielekeza katika kuongeza ajira kwa vijana wetu, ajira rasmi na zisizo rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili ni eneo la ubunifu na utafiti. Ninapenda kuipongeza Wizara ya Elimu, kupitia Chuo cha UDOM, kuwa washindi wa shindano la vyuo 29 nchini katika masuala ya cyber. Hapa chuo chetu cha UDOM kimetuonesha umahiri mkubwa na kimetuvisha nguo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nawaombe Serikali tutengeneze misingi au mpango wa kudumu kuelekea bajeti inayokuja kuimarisha ubunifu na matumizi ya teknolojia za kidigitali katika huduma za kijamii, Serikali iwekeze zaidi katika kuwaendeleza na kuwaongoza wataalamu wa Artifical Intelligence, kwa maana dunia ndiko inakojielekeza. Hii itasaidia kukidhi mahitaji ya matumizi ya AI na pia, kuendana na hali ya kiuchumi kupitia ushindani wa sekta mbalimbali zinazotumia teknolojia hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nawapongeza Serikali kwa kuanza kutumia teknolojia hii kwenye baadhi ya taasisi za umma, kwa mfano, Mfumo wa E-File. Tumeanza hivyo, tunavyoendelea tutaendelea kupunguza ajira za watu. Kwa hiyo, sisi hatuna budi kuweza kujikita katika eneo fulani la Artificial Intelligence. Kama tunajikita kwenye maintenance, tujikite hapo, tusibebe yote kwa wakati mmoja, tuangalie focus yetu sisi, kama Taifa, tunakwenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa mwisho ni katika eneo la elimu. Nawapongeza sana Wizara ya Elimu, tumeanza vizuri. Wiki iliyopita nimeona Mheshimiwa Rais akifungua mpango wa KKK wa kuhamasisha suala la Kusoma, Kuandika na Kuhesabu kwa watoto wetu na amesisitiza mtoto asifike darasa la tatu hajui kusoma na kuandika, lakini sasa katika bajeti nimeona inaelekea shilingi trilioni 8.19 kwa 2026/2027. Ninataka kusema nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi hapa najielekeza zaidi katika ongezeko la mikopo ya elimu ya juu. Ni kweli, udahili umeongezeka, 2020/2021 udahili ulikuwa 295,919; 2024/2025 udahili ukawa 361,257; bajeti ya mikopo ilikuwa shilingi bilioni 570 na sasa 2025/2026 shilingi bilioni 916.7; udahili wa 2024/2025 ulikuwa 248,331. Udahili huu umeweza kuwanufaisha wanafunzi 248,331. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaweza kuona hawa wanufaika wa mikopo ni wale ambao wanaendelea, kwa maana ya first year, second year, third year, fourth year na fifth year, kwa zile kozi zinazokwenda mpaka miaka mitano na wale wapya. Kwa hiyo, tunaweza kuona kwamba, bado uhitaji wa mikopo ya elimu ya juu ni mkubwa, fedha haitoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwasaidie Wizara ya Elimu na Bodi ya Mikopo kuweza kuongeza bajeti. Pili, tuweke mikakati thabiti ni namna gani tutakiongezea hiki chombo, bodi ya mikopo, kupata fedha. Kwa nini tusi-engage private sector ili hii fedha iongezeke?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wahitaji ni wengi, watoto wa maskini wengi wamekosa mikopo na waliomaliza chuo wengi hawajaweza kurudisha. Kutegemea source moja ambayo ni ruzuku ya Serikali, kuuchunga huu mfuko wa bodi ya mikopo, ni kazi ngumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuwaongezee bajeti ili mipango iweze kufikia malengo ambayo tunahitaji. Sasa wanafunzi wetu wafundishwe ujuzi pamoja na vitu ambavyo vitawasaidia kwenda kujiajiri moja kwa moja. Wakishaajiriwa au kujiajiri moja kwa moja wataweza kurudisha fedha hizi na wengine wakanufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba kuunga mkono hoja iliyowekwa Mezani. Mwenyezi Mungu atusaidie wote tufanye kazi vizuri. (Makofi)