Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Twaha Said Mwakioja (4 total)

MHE. TWAHA S. MWAKIOJA aliuliza:-

Je, ni lini Tembo wanaojeruhi na kuharibu mali majumbani na mashambani maeneo ya Mwakijembe, Bwiti, Daluni na Duga watadhibitiwa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninaomba kumshukuru sana sana Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na kuingia katika awamu hii tukiwa salama.

Mheshimiwa Spika, pili, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini. Ninatoa ahadi kwamba nitafanya kazi kwa weledi mkubwa, uadilifu pamoja na ufanisi mkubwa sana.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu katika Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga. Mkakati huu unajumuisha kuweka vikosi vya kudumu vya askari katika Kata za Bwita na Mwakijembe kwa ajili ya mwitikio wa haraka wa matukio ya wanyamapori katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea pia kutumia teknolojia za kisasa hasa visukuma mawimbi (GPS Collars, ndege nyuki pamoja na mabomu baridi katika kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo katika Wilaya ya Mkinga. Ahsante sana.
MHE. TWAHA S. MWAKIOJA aliuliza: -

Je, lini Serikali itawapatia maji safi na salama wananchi wa Wilaya ya Mkinga kupitia Mradi wa Tanga – Horohoro?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Twaha Said Mwakioja, Mbunge wa Jimbo la Mkinga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Maji Mkinga – Horohoro kwa gharama ya shilingi bilioni 35.4. Kazi zinazotekelezwa kupitia mradi huo ni pamoja na ujenzi wa matanki 10 yenye jumla ya ujazo wa lita 2,450,000, ulazaji wa mabomba yenye umbali wa kilometa 223.7 sanjari na ujenzi wa vituo 58 vya kuchotea maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa mradi wa Mkinga – Horohoro umefikia wastani wa 65% na umeanza kutoa huduma kwa wananchi wa Kijiji cha Mtimbwani. Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2026 na kunufaisha wananchi wapatao 57,334 waishio katika vijiji 37 katika Wilaya ya Mkinga, mkoani Tanga.
MHE. TWAHA S. MWAKIOJA aliuliza: -

Je, lini Serikali itafanya utafiti wa vyanzo vya uhakika vya maji Tarafa ya Maramba, Wilaya ya Mkinga ili kutatua changamoto ya maji kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji napenda kujibu swali la Mheshimiwa Twaha Said Mwakioja, Mbunge wa Jimbo la Mkinga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza utafiti wa maji chini ya ardhi katika maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa maji Wilayani Mkinga, mkoani Tanga ikiwemo baadhi ya maeneo ya Tarafa ya Maramba. Utafiti huo umeonesha uwepo wa maji chini ya ardhi katika vijiji vinne vya tarafa hiyo ambavyo ni Kichangani, Gombero, Maramba A na Matemboni, sanjali na Kijiji cha Mkota kilichopo Kata ya Mwakijembe wilayani humo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa taratibu za kuanza uchimbaji wa visima virefu katika maeneo yaliyobainishwa zinaendelea. Aidha, Serikali itaendelea na zoezi la utafiti wa vyanzo vingine vya maji katika maeneo yenye changamoto wilayani Mkinga ili kukidhi mahitaji ya wananchi wa wilaya nzima ikiwemo wale wa Tarafa ya Maramba.
MHE. TWAHA S. MWAKIOJA aliuliza:-

Je, lini Serikali itakarabati madarasa chakavu na kujenga madarasa mapya katika Shule za Msingi Jimbo la Mkinga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Twaha Said Mwakioja, Mbunge wa Jimbo la Mkinga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kufanya ukarabati wa shule katika Wilaya ya Mkinga ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022 mpaka kufikia mwaka 2025/2026, Serikali imepeleka jumla ya shilingi bilioni 2.78 katika Wilaya ya Mkinga kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili mpya za msingi, madarasa 82 katika shule 35 chakavu za msingi na ukarabati wa shule tatu chakavu za msingi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2026/2027 Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 275.2 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa matatu, matundu ya vyoo 94 katika shule 19 za msingi katika Jimbo la Mkinga.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kujenga madarasa na kukarabati shule za msingi chakavu nchini zikiwemo shule za Jimbo la Mkinga. Naomba kuwasilisha.