Supplementary Questions from Hon. Twaha Said Mwakioja (4 total)
MHE. TWAHA S. MWAIKOJA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; Taasisi zetu za Serikali za TANAPA, NCAA na TAWA zinabaki na mapato ili kuweza kutoa huduma mbalimbali. Pamoja na kubaki na mapato (retention) bado tumekuwa na changamoto ya kuwapa waathirika hawa wanaokumbana na majanga haya ya wanyamapori kifuta jasho ambacho ni kidogo na kiwango hiki ni cha muda mrefu sana. Je, Serikali haioni haja sasa ya kufanya mapitio juu ya viwango hivi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; utaratibu wa kufanya uthamini kwa wananchi wanaopata majanga umekuwa na urasimu mkubwa sana na kusababisha baadhi ya wananchi kushindwa kufuatilia na kuendelea kuilalamikia Serikali yetu. Je, Serikali haioni haja sasa ya kufanya mapitio juu ya mchakato huu ili uwe rahisi na kuwaletea tabasamu wananchi wetu na hususan wananchi wa Jimbo la Mkinga? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kabla ya kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Twaha Mbunge wa Mkinga, ninaomba nimpongeze sana pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuaminiwa na wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali ilishafanya marekebisho ya Kanuni ya Mwaka 2011, kanuni hiyo ilionekana ni kweli kifuta jasho ni kidogo imefanyiwa marekebisho mwaka 2024 kwa Tangazo la Serikali Na. 440, mwaka 2024, tarehe 31 Mei na imefanya marekebisho makubwa. Kwa sasa waathirika wale ambao watakuwa na ulemavu wa muda mfupi yaani majeraha ya muda mfupi watalipwa 50%, vifo vya mifugo 50%, uharibifu wa mazao 50%. Pia lipo ongezeko kubwa la vifo na ulemavu wa kudumu kwa 100%.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, Serikali tayari imeliona hilo suala la urasimu na kwa sasa tunatumia mfumo maalum unaotambulika kwa jina la PAIS yaani Problem Animal Management Information System ambao sasa urasimu hautopatikana, maana yake inarekodi moja kwa moja na kuhakiki taarifa zile na kupelekwa kwenye kanzidata. Nina imani kabisa kwamba urasimu huo sasa utakuwa umepata mwarobaini wake. Ahsante sana.
MHE. TWAHA S. MWAKIOJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kuishukuru Serikali kwa majibu yake mazuri. Pamoja na majibu hayo mazuri nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa mradi huu wa kihistoria ambao kwa Wilaya ya Mkinga haujawahi kutokea. Pamoja na hivyo mradi huu unatekelezwa kwa kusuasua sana. Wananchi wa Mkinga wameyasubiri maji haya kwa muda mrefu, tarehe za ukamilishwaji wa mradi huu zimekuwa zikibadilishwa kila mara. Pamoja na maelekezo ya Mheshimiwa Rais kuwa mradi huu tangu mwaka jana ukamilike pamoja na maelekezo ya Mheshimiwa Waziri wa Maji kwamba mradi ukamilike, lakini mradi huu haujakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufuatilia ni kwamba mkandarasi anaidai Serikali na alishasimama akaondoka eneo la mradi; je, Serikali ina kauli gani kuhusu kumlipa mkandarasi huyu ili tarehe iliyotajwa ya kukamilisha mradi huu mwezi Julai iweze kutimia na wananchi wenzangu wa Mkinga waweze kupata maji safi na salama waliyoahidiwa na Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Wilaya ya Mkinga inatarafa mbili, mradi huu wa kihistoria na mzuri unakwenda kuwapatia maji watu wa Tarafa moja ya Mkinga. Hali ya Tarafa ya pili ya Maramba katika upatikanaji wa maji ni mbaya mbaya kweli kweli. Wakati wa kiangazi walifikia hadi kununua dumu la maji kwa shilingi 3,000 mpaka shilingi 5,000.
Je, kaka yangu Waziri wa Maji yupo tayari kuambatana na mimi katika kipindi hiki cha bajeti ili tukaione hali ya Tarafa ya Maramba na ikiwezekana atafute vyanzo vipya vya maji na ikibidi basi atuunganishe na Gridi ya Maji ya Taifa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kaka yangu Mheshimiwa Twaha Said Mwakioja, Mbunge wa Mkinga kwa kazi nzuri kwanza kabisa ya ufuatiliaji wa miradi. Kwa namna alivyoongea inaonekana anafuatilia hatua kwa hatua na kujiridhisha changamoto iko wapi. Sisi Serikali kupitia Wizara ya Maji tumejipanga kuhakikisha miradi mingi ya maji inakamilika ukiwemo mradi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameongelea mradi huu ni wa kihistoria. Ni kweli kabisa Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza shilingi bilioni 35.4 kuhakikisha kwamba eneo la Mkinga linapata suluhisho la kudumu. Vilevile, Serikali imeshamlipa mkandarasi shilingi bilioni 1.5 lakini pia ndani ya mwezi huu mkandarasi tunaenda kumlipa shilingi bilioni 1.7 arejee na kuendelea na mradi ili uweze kukamilika kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua kiu ya Mheshimiwa Mbunge na Wana-Mkinga ni kuhakikisha kwamba maeneo mengi yanatatuliwa kuhakikisha kwamba wanapata huduma ya maji safi na salama, lakini tuangalie upatikanaji wa maji mpaka sasa kwa Wilaya ya Mkinga ni 72.9% na kuna vijiji 85.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vijiji 85, vijiji 52 vyote vina maji isipokuwa vijiji 23. Katika vijiji 23 Serikali tumejipanga kuendelea kutafuta fedha ili vijiji 23 vya Mheshimiwa Mbunge ikiwemo Maramba ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja tutaingiza kwenye mpango wa bajeti ili twende kuhakikisha kwamba Wana-Maramba kwa sauti ya Mbunge wao wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
MHE. TWAHA S. MWAKIOJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali japo kwa maoni yangu nayaona bado ni majibu mepesi. Hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mkinga na hususan tarafa ya Maramba imekuwa na miradi ambayo haijakamilika na ilipaswa kukamilika tangu mwaka 2023 na wakandarasi wameshaondoka maeneo ya mradi na sababu kuu ni kwamba wakandarasi hawa hawajalipwa; Kata ya Gombero mkandarasi ameondoka na anadai shilingi bilioni 1.2, Kata ya Mhinduro, mkandarasi ameondoka na anadai shilingi milioni 368, Kata ya Mapatano mkandarasi ameondoka na anadai shilingi milioni 196, Mradi wa Mkinga - Horohoro mkandarasi anadai zaidi ya shilingi bilioni 1.7.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, pamoja na fedha nyingi tunazopewa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, miradi hii imechelewa zaidi ya miaka minne wananchi hawapati maji. Je, sasa ni lini Serikali ituambie kwa uhakika kabisa wakandarasi hawa watalipwa ili wakandarasi warudi na wananchi waweze kupata maji safi na salama waliyoahidiwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; tarafa hii ya Maramba ina hali ngumu sana ya upatikanaji wa maji na hususan wakati wa kiangazi. Naomba Serikali ituambie, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuambatana nami mara tu baada ya Bunge hili la bajeti ili tutembee kata kwa kata tujionee hali halisi na ikiwezekana tupate vyanzo vya uhakika na ikibidi tarafa hii ya Maramba tuweze kuiunganisha na mtandao wa Gridi ya Maji ya Taifa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Twaha Said Mwakioja, Mbunge wa Mkinga kwa kazi nzuri, kubwa anayoifanya na kwa ufuatiliaji na kwa kata hii ya Maramba natambua kwamba Mheshimiwa Mbunge aliongea kwenye bajeti yetu ya maji, lakini pia amekuwa na mawasiliano ya karibu sana na Mheshimiwa Waziri wa Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na swali lake la kuhusu miradi iliyoko katika kata tatu; mradi wa kwanza ambao umesema upo Gombero ni kweli, lakini Mradi wa Mapatano pamoja na Mhinduro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Gombero umeshafikia 100% maana yake umeshakamilika, mkandarasi natambua anadai kiasi cha shilingi bilioni 1.2. Mradi wa Mapatano kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema upo katika hatua ya 35% ya utekelezaji na Mradi wa Mhinduro upo 46%. Tunatambua tulikuwa tunafanya uhakiki wa zile hati zake za madai ili tulipe fedha inayoendana na kazi ambayo kule imefanyika kwa sababu tumebaini kuna maeneo mengine hati zinazoletwa haziiendani na hali halisi ya kazi iliyofanyika site, hizi ni fedha za Watanzania za walipakodi wa Tanzania lazima tuzisimamie ili ziweze kutoa matokeo halisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nakuhakikishia kazi ya uhakiki tumeshaimaliza, sasa tunasubiri kuwalipa wakandarasi ili waweze kurudi site kwa upande wa Mapatano pamoja na Mhindiro waweze kufanya kazi nzuri.
Mheshimiwa Mweyekiti, lakini pia upande wa Mkinga Horohoro Mheshimiwa Rais amewekeza zaidi shilingi bilioni 35 katika mradi huu na mradi huu upo hatua nzuri kabisa sisi tunachokifanya hatupeleki fedha kwa kasi tunayotaka sisi, tunapeleka fedha baada ya hati ya madai kuja mezani.
Kwa hiyo, sisi tutahakikisha kwamba tunaongeza msukumo pale ambapo hati imeshafika mezani lazima mkandarasi alipwe na kuhakikisha kwamba mradi uweze kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hali ya upatikanaji wa maji Mheshimiwa Mbunge hata wewe unafahamu, hivi sasa ni zaidi ya 72.9% natambua changamoto ya kwenda kufanya utafiti. Mheshimiwa Waziri ulimuomba kwenda katika jimbo lako, nataka nikupe taarifa nzuri ni kwamba Mheshimiwa Waziri pamoja na wataalam wa Wizara pamoja na wewe, yupo tayari kuambatana nawe kwenda katika jimbo lako ili kwenda kufanya kazi hiyo, lakini lengo kubwa ni nini, lengo kubwa la kwenda Mkinga la kwanza ni kwenda kufanya tathmini ya vyanzo vya maji vilivyopo na la pili kwenda kubaini vyanzo vipya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, kama ambavyo umeomba kuangalia uwezekano wa Tarafa ya Maramba inaunganishwa kwenye Gridi ya Taifa ya Maji. Katika hili hatutosubiri Mheshimiwa Waziri aende, ninawaelekeza bonde waanze kufanya hii kazi kabla ya Mheshimiwa Waziri hajaenda ili anapofika wampatie taarifa ya tathmini ambayo watakuwa wameshaifanya na wewe Mheshimiwa Mbunge ukiwepo ili sasa tuanze kuchukua hatua ya kufanya feasibility study, baada ya hapo tupate fedha na baada ya hapo tuanze kutekeleza mradi bila kuwa na cha...
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu sauti yako ni sauti ya wananchi wa Mkinga na sisi kama Serikali tutaendelea kushirikiana na wewe ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji ndani ya Jimbo la Mkinga, ahsante sana.
MHE. TWAHA S. MWAKIOJA: Mheshimiwa Spika, kwanza niishukuru Serikali kwa majibu mazuri na juhudi ambazo imezionesha kwa kipindi chote.
Mheshimiwa Spika, nimepata bahati ya kuzitembelea takribani shule zote za sekondari na msingi katika jimbo ninaloliongoza la Mkinga, kwa kweli hali ya shule hizi haiko vizuri hususan shule za msingi. Zipo shule zinavuja, zipo shule sakafu ni tifutifu kama vile uwanja wa mpira; na zipo kuta zinataka kuanguka.
Je, kutokana na hali hii, ni upi sasa mkakati wa Serikali wa kuhakikisha inaongeza fedha ambazo inazitenga ili kuondokana na adha hii; kwa sababu kuna baadhi ya madarasa nimeingia, watoto wanajitenga, hawa darasa la tano, hawa darasa la sita. Darasa moja wapo humo humo wanasoma pamoja. Ni upi mkakati wa Serikali kuongeza fedha ili kuhakikisha kwamba inaondokana na adha hii na kuweza kutoa elimu iliyo bora?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; nimwombe Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI ikimpendeza tuongozane naye ili akaone adha ya shule na miundombinu iliyopo katika Jimbo la Mkinga. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Twaha Said Mwaikoja, Mbunge wa Jimbo la Mkinga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI tuliwasilisha katika bajeti katika Bunge lako hili Tukufu kwamba tunao mradi unaoitwa School Infrastructure Facelifting Programme (SIFA). Mradi huu unakwenda kuboresha shule hizi hasa zile kongwe na Bunge lako hili Tukufu lilipitisha bajeti ile na tutakwenda kuhakikisha kwamba tunaongeza fedha katika shule ambazo, kwanza ni chakavu na zile za muda mrefu na zile zenye mahitaji muhimu. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa tutahakikisha tunaongeza fedha katika maeneo yote aliyoyataja ili kuhakikisha tunaboresha miundombinu ya elimu katika jimbo lake.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu ziara; Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI tumeendelea kufanya ziara ambazo zinaongozwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu na tatatenga ratiba mimi na Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kufika jimboni kuangalia miundombinu, siyo tu ya elimu hata maeneo mengine mbalimbali ili kuhakikisha kwamba ile azma ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuacha tabasamu kwa Watanzania inakwenda kutekelezwa. Naomba kuwasilisha.