Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. ISAYA M. MOSES: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kuniona. Kwa sababu leo ni mara yangu ya kwanza kusimama, kwanza ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kufika kwenye Bunge hili, chumba hiki Tukufu. Ninashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumshukuru Mwenyekiti wangu wa Chama Cha Mapinduzi, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ninapenda kumpongeza Makamu wa Rais, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi. Ninapenda pia kumpongeza Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi. Ninampongeza vile vile Spika Wangu, Mussa Azzan Zungu. Ninapenda kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wote waliopata uteuzi, tuna Imani nao na tumeona kazi yenu wanayoifanya, tuna imani tutafika salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuwapongeza wananchi wangu wa Jimbo la Kongwa kwa kunichagua kuwa hapa, kwa kweli, sitawaacha. Wamenifanyia vizuri kumchagua Rais wangu kwa kumpa kura nyingi sana, hata alivyopita pale kwenye kampeni watu walijaa sana pale Kibaigwa, mpaka Rais mwenyewe alifurahi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, ninapenda sasa kuwashukuru hao Mawaziri wawili kwa kuwasilisha Mpango wao wa Maendeleo. Mpango wa Maendeleo wa Serikali ni mpango ulioshiba, maana mimi ni mdau ninafahamu haya mambo, kazi iliyofanyika ni kubwa na wanastahili pongezi. Kilichobaki ni kusimamia utekelezaji wa huu Mpango wa Maendeleo, ukisimamiwa vizuri tutafika salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru kwa kupanga 70% itatoka kwenye private sector na 30% itoke kwenye public sector. Huo ni ubunifu na ni mawazo makubwa ya kina profesa. Ninawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo machache tu ninataka niongezee, hayo tukiyafanya vizuri mpango wetu utakwenda vizuri sana. Kwanza ni kilimo cha umwagiliaji; pili, nitazungumzia ufugaji; tatu nikipata muda nitazungumzia viwanda na mwisho nitazungumzia suala la miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kilimo cha umwagiliaji. Hilo ndiyo utaratibu mzima, ili tufike salama kwenye mipango yetu hii; mpango mfupi, mpango wa kati na mpango mrefu. Kwanza ni lazima tuwe na uhakika wa chakula, Taifa lisipokuwa na chakula lina njaa, siyo Taifa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tu mmeona hali halisi, mvua imejaribu tu kufanya kidogo watu tukawa na wasiwasi kwamba, tutakwenda wapi. Lazima tuwe na uhakika wa chakula halafu tuwe na ziada, ziada ile sasa ni biashara. Tukifanya hivyo, tutakwenda vizuri, tukiwa na kilimo cha umwagiliaji maana yake ni tutatumia mito yetu vizuri, tutachimba mabwawa, tutachimba visima na tukishafanya hivyo, kilimo kitakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutafute mbegu bora za kuweza kuzalisha, maana sasa hivi wakulima wangu na wa sehemu zingine wanapanda mbegu kwa kutumia nafaka, wala siyo mbegu. Ni nafaka wanalima, hizo hizo wanaenda kupanda, lakini tukitumia utaratibu mzuri wa kilimo, ziko mbegu bora za kilimo. Sasa hivi wakulima wengi, hasa kule kwangu Kongwa, Sehemu za Ngomai, Mkoka na Mlali hao watu wanalima ekari moja inatoa magunia matatu, magunia mawili, gunia moja, wakati kuna mbegu bora ya mahindi; ukichukua ile DK ngapi sijui, 777 DK, mpaka 93, uwezo wa kuzalisha kwa ekari moja ni magunia 40 mpaka 45.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwa utaratibu huu wa kipato kikubwa, yaani tukaamua, kama Serikali sasa, tukaamua kwamba, sasa kilimo cha umwagiliaji na mbegu bora zitumike tutamtoa mtu, mkulima atabadilika. Hata lile walikuwa wanasema pato la mtu mmoja mmoja, per capita income ile Dola 7,000, nina imani tutapita kwa sababu, leo hii nina uhakika pale Soko la Kimataifa la Kibaigwa gunia la kilo 100 linauzwa shilingi laki moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mtu akilima eka moja anapata magunia 40. Wako wakulima kule Ngomai, Mkoka, wanalima, mtu ana ekari 1,000 anapata magunia 1,000; maana yake ni average ya eka moja gunia moja. Ukienda kwake utakuta quantity ya mahindi imejaa pale utasema huyu ni tajiri, lakini ukiangalia uhalisia kamili huyu mtu anapata gunia moja kwa eka moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukimtengeneza huyu mtu na wale watu wako vizuri mtu mmoja unaweza ukakuta ana ma-tractor 10 ya kwake binafsi, yako pale 10. Sasa tukimwezesha kilimo cha umwagiliaji huyu mtu, akatengenezewa mazingira mazuri, maana yake ni kwamba, badala ya kupata magunia 1,000 huyu mtu atapata magunia 40,000 ukizidisha kwa shilingi 100,000 kwa bei ya Kibaigwa ya leo, ambayo mimi juzi nimeuza, huyu mtu wa ekari 1,000 atapata magunia 40,000 ambayo income yake itakuwa ni shilingi bilioni nne. Sasa kwa nini asifike huko tunakosema kwenye Dola 7,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama tutawawezesha hawa wakulima vizuri kabisa tutatoka. Tujitahidi sasa tufumbe macho, Serikali tuingize hela kwenye kilimo. Mfano pale Kongwa, maji yako jirani ni kuchimba kidogo tu yanapatikana. Dodoma kwa ujumla hali ya maji ipo vizuri, wakituwezesha; mfano kama pale kwangu nikiwezeshwa mabwawa 10 na visima 12 maana yake ni kwamba, nitamhakikishia Mheshimiwa Profesa nitafika kwenye per capita income ya 8,000 sio 7,000. Hebu wajaribu tuone, wafanye majaribio tu, tuamue tufanye eneo ambalo ni la mfano, tuweke mahali, uchumi utapanda sana, tukifanya hivi tutakwenda vizuri. Ninawaomba sana tufanye vitu kwa vitendo tutafika mahali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninazungumzia ufugaji. Kwenye jambo letu hili, Mpango wa Maendeleo, wamezungumzia ufugaji, lakini hawakuingia in detail. Wafugaji ni watu muhimu sana na ni wawekezaji wakubwa, hii sekta tukiitumia vizuri, ya wafugaji, tutakwenda mbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi nilikuwa ninaongea na Katibu Mkuu wa Chama cha Wafugaji Tanzania, hiyo ni private sector, ameniambia tunao mifugo, tukiacha mbuzi na kondoo, ng'ombe milioni 37, hawa tukiwatumia vizuri uchumi huu utakwenda vizuri, ila sasa hawa watu wana shida. Shida ya kwanza ni wana changamoto, maana ukifika wamejipanga wana salamu yao utasikia, ukifika tu pale, wanasalimiana ufugaji maisha yetu, maisha yetu ufugaji kwa hiyo, wanajua kwamba, ufugaji ni maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya kwanza ni ardhi. Ardhi inatakiwa ipimwe, tuwapimie hawa watu ardhi, ili wasiwe wanarukaruka tu. Pili ni maji, hawa watu wana shida ya maji, tuwatengenezee utaratibu wa kupata maji wasiwe wanahamahama. Tatu ni malisho, hawa watu wana shida ya malisho. Kama tutawatengenezea utaratibu mzuri wa malisho hawa watu tutapata kipato kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto yao nyingine ni masoko. Masoko yao kidogo ni magumu. Sasa hivi nilikuwa ninaongea na huyu Katibu Mkuu, Bwana Matayo Daniel ananiambia sasa hivi wanapeleka Comoro, lakini Comoro wana shida ya meli, ile meli ng'ombe wanakufa, lakini wakienda Comoro kilo moja ya nyama kwa hela ya Tanzania ni 30,000/=. Kwa hiyo, tukiwaboreshea watu, tukawatengenezea mazingira mazuri, tutapata income ya kutosha na mpango wetu utakwenda vizuri zaidi. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. ISAYA M. MOSES: Namalizia Mwenyekiti.
MWENYEKITI: Malizia.
MHE. ISAYA M. MOSES: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba suala la miundombinu iko shida pale. Kwenye bajeti hii, tunaenda na iliyopita, Ilani ya Uchaguzi ilituwekea barabara ya kutoka Kongwa Junction kwenda NARCO, kwenda Hogoro, kwenda Songambele mpaka Zoisa na barabara ya kwenda Zoisa – Kiteto mpaka Arusha. Hiyo ni barabara ya uchumi, ambayo mazao mengi yanatoka kule, lakini sasahivi haizungumzwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo barabara mpaka Mheshimiwa Rais alisimamia mikataba yake, kusaini mikataba, lakini mpaka leo hii haijulikani kinachoendelea. Huko watu wanauliza, hivi Rais inawezekana akasimama akasema ni mikataba ya uongo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba Wizara ya Ujenzi wajiandae vizuri. Kama kuna mabadiliko yoyote ninaomba wakasimame kule watetee maana sisi tutakufa. Hiyo barabara inahitajiwa sana kwenye uchumi. Ninawaomba sana hicho kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, ninakushukuru. (Makofi)