Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Josephine Joseph Kapoma (2 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi hii niliyoipata ili na mimi niweze kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee ninapenda kumpongeza kaka yangu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Daniel Chongolo pamoja na timu yake Naibu Waziri, Katibu Mkuu kwa hotuba kubwa na nzuri ambayo imelenga na kuwapa matumaini makubwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ajili ya maslahi ya muda, ninaomba nijielekeze moja kwa moja. Mosi, nitaelekea kwenye zao la tumbaku. Kwa nini zao la tumbaku, zao la tumbaku mimi nikiwa kama mwakilishi wa watu wa Morogoro hili zao ni katika mazao ya kimkakati ambayo watu wa Morogoro linatuingizia kipato kikubwa kwa sababu viwanda vya kuchakata tumbaku viko Mkoani Morogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zao la tumbaku kwa takwimu tu, mwaka wa fedha 2020/2021 tulipata jumla ya mapato ya USD milioni 392, lakini kufika mwaka wa fedha 2024/2025 tumepata mapato ya zaidi ya USD bilioni 1.2, ni zaidi ya 187% ya ongezeko la pato.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sisi watu wa Morogoro, Kiwanda cha Mkwawa Tobacco mwezi Aprili, 2024 kufika Disemba, 2025 tumefanikiwa kupata zaidi ya ushuru wa Halmashauri levy bilioni 2.7, lakini viwanda hivi tu kwa Morogoro toka Rais alivyokuja na mapinduzi ya tumbaku, Morogoro viwanda hivi vimeweza kuajiri ajira za muda mrefu zaidi ya wafanyakazi 1,000 na ajira za msimu zaidi ya 5,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, pongezi hizi huwezi kuziongelea bila kumtaja Mkurugenzi wa Bodi ya Tumbaku Ndugu Stanley. Kazi kubwa aliyoifanya katika mapinduzi ya tumbaku watu wote tunaelewa. Pia, sisi kama watu wa tumbaku pongezi kubwa tunazipeleka na wachangiaji wengi wamelalamika kwamba mbolea zinachelewa, lakini wakulima wa tumbaku na wadau wa tumbaku kwa kweli kwenye suala la mbolea hilo hatuna malalamilko kwa sababu mbolea tumepata kwa wakati. Kwa hiyo pongezi nyingi sana ziende kwa kaka yangu Mshote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninajielekeza sasa kuishauri Serikali. Wachangiaji wengi waliopita wamelalamika kuhusu suala zima la bei. Kweli mwaka jana wastani tuliuza kwa dola 2.3, lakini mwaka huu tunaenda kuuza kwa dola 1.9. Sasa ninaishauri Serikali, soko la tumbaku linakuwa-controlled, ni soko la kidunia hatuna control na bei ya tumbaku. Sasa tufanye nini, nilikuwa ninaishauri Serikali kwa sababu soko la tumbaku liko-controlled, ni wakati sasa sisi kama Tanzania tukaangalia masoko mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano Tanzania hatufanyi biashara na China, lakini tunao Mabalozi kama Balozi ambayo iko China. Huu ni wakati sahihi wa kuona ni vipi tunaweza tukatanua wigo wa soko na kwa kifupi China kufanya biashara na sisi, kitu ambacho tunatakiwa kukifanya ni mikataba ya nchi kwa nchi ambayo ni bilateral agreement.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukitanua wigo wa soko na kuongeza watu wengine Wallah nakuapia, hili suala la bei ya tumbaku halitakuwa kero kwa sababu tutakuwa na wigo mpana sana wa soko. Kwa sababu sasa hivi tuna wanunuzi wachache ambao wanaweza wakapanga bei wanayoitaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kuishauri Wizara kwamba shida ya bei ya tumbaku kidunia pia inasababishwa na cost of production. Hata hivyo, Tanzania tuna uwezo wa kutengeneza viwanda vyetu, ambapo tutatengeneza vifungashio kama magunia na kamba, tunayo katani na hizi malighafi ambazo hivi vitu tunaweza tukavitengeneza katika nchi yetu. Kwa sababu bei ya tumbaku inaathirika kikubwa sana na cost of production.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tukipata nafasi ya kuweka mikakati katika kujenga viwanda vya mbolea, viwanda vya magunia na nyuzi zikapatikana hapa, tunaenda kupunguza cost of production, hivyo hata soko la dunia likiyumba kwenye bei ya tumbaku, sisi bado tutakuwa tumeuza tumbaku yetu kwa faida na soko likipanda maana yake tutauza kwa supper abnormal profit. Kwa hiyo ninatoa ushauri huu katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, soko la tumbaku sasa hivi tumekuwa na shida kubwa hasa katika mikutano ya kidunia, tumekuwa tunapigwa vita sana katika uzalishaji wa tumbaku.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge, ahsante sana.

MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, dakika moja ninamalizia.

NAIBU SPIKA: Unga mkono hoja, muda wako umekwisha.

MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kupata nafasi ya kusimama siku ya leo kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa ninapenda kumpa pongezi kaka yangu Mavunde na timu yake yote, Naibu Waziri, Katibu kwa kazi kubwa ambayo wameifanya. Tunapoongelea madini maana yake tunaongelea uchumi wa Tanzania na tunaongelea ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Kwa hiyo, kaka yangu Mavunde, kiatu alichokivaa kimemtosha sawasawa, akaze mwendo na ashikilie hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee ninafarijika sana. Nikiangalia jinsi tulikotoka na tunapoelekea. Ukiangalia takwimu zinaonesha mwaka wa fedha 2023/2024 tilipata maduhuli zaidi ya bilioni 750 na kadhaa, lakini mwaka unaofuata tulipata zaidi ya trilioni moja na mwaka 2026 hatujamaliza mwaka wa fedha, ndani ya miezi tisa tumeshazidi zaidi ya 114% katika ukusanyaji wa maduhuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii inamaanisha nini? Hii ina maana kwamba mikakati ambayo Waziri amejiwekea kama Wizara ya Madini, inaenda sawasawa siyo mikakati ya kwenye makaratasi. Kwa hiyo, ninaomba nimpongeze kwa sababu sisi ni Tomaso, tunataka kitu ambacho Waziri anakizungumza tukione. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitajikita moja kwa moja katika madini ambayo mchangiaji dada yangu Mheshimiwa Esther ametoka kuyasemea. Nimetoka Mkoa wa Morogoro, Mkoa wa Morogoro kila mtu anafahamu jinsi tulivyobahatika kuwa na madini ya kila aina, lakini sasa shida inayokuja ni kwamba haya madini hayajapewa thamani ambayo yanatakiwa kupewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Morogoro tu pale tuna madini kama limestone, tuna marble, tuna golden shine, amethyst, sand stone, kitenge, feldspar, just name it! Ninaweza nikataja mpaka asubuhi, lakini ukiangalia kwa takwimu mwaka 2023 mpaka mwaka 2025 tumefanikiwa kukusanya maduhuli ambayo ni kama bilioni 16 siyo kweli! Hii ni kwa sababu ninaona kama nguvu kubwa tumeiweka kwenye baadhi ya madini ambayo ni gold na Tanzanite.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni wakati wa kuyapa haya madini thamani na nini sasa kifanyike? Mimi binafsi ni mchimbaji mdogo na kumekuwa kuna shida ambayo wachimbaji wengi wa madini haya ambayo either siyo ya vito wanapitia, mojawapo ni kukosa masoko. Mfano, ninachukulia sasa hivi mtu anachimba sandstone, leo hii ukichimba sandstone ukimpelekea Mchina anakwambia shilingi laki tatu kwa kilo, kesho ukipeleka anakwambia shilingi laki tatu kwa kilo, baada ya wiki ukimpelekea anakwambia hii jiwe leo leta mbaya sana, mimi nitanunua kwa shilingi elfu nane, kwa sababu hakuna soko, I mean hakuna bei elekezi ambayo ipo manageable, unakuwa huna cha kufanya inabidi uuze.

Mheshimiwa Naibu Spika, imagine nimetoka na mzigo kutoka kwa baba yangu kule Profesa Kabudi, Kilosa mpaka Dar es Salaam, mzigo ambao ninaenda kuuza kwa kilo shilingi laki na hamsini, nikifika Dar es Salaam ananiambia shilingi elfu nane. Siwezi kurudi nao ule mzigo Kilosa! Kwa sababu nilipokwenda mara ya kwanza alinunua kwa kilo shilingi laki na hamsini nilivyorudi nimeenda kukopa na kufanya kila kitu ili niongeze kilo nyingi kwa sababu ninajua nikipeleka Dar es Salaam nitauza kwa shilingi laki na hamsini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikifika Dar es Salaam akisema kwa shilingi elfu nane na tena ukienda muda mbaya anakwambia fanya haraka mimi nataka funga ofisi. Kwa hiyo, ukiangalia sasa mimi ninafanyeje, inabidi uuze kwa bei hiyo hiyo. Sasa hii hatukuzi Uchumi. Haya madini ni kweli yanauhitaji ndiyo maana hawa ndugu zetu zamani walikuwa wanakaa Dar es Salaam lakini sasa hivi ukienda Gairo, ukienda Dutumi, ukienda Kisaki wamejenga mpaka na nyumba. Wanachosema wenyewe wanatupa technical assistance lakini technical assistance kwetu kule Morogoro hawa majamaa wanatupa digger na jenereta ndiyo technical assistance.

Mheshimiwa Naibu Spika, anatupa digger na jenereta, lakini yeye anachukua 85%, anakupa 15%, anaondoka nayo. Kilichobakia kwamba vijana wetu wengi wamekuwa na stress na hawaoni thamani, mbaya zaidi haya madini wakiyauza wanaona kabisa hawa wanunuzi wanafaidika. Imefika sehemu sasa hivi unamwona Mchina anakuja kununua madini kijijini kule Kilosa amejenga na nyumba, lakini pesa anayonipa mimi siwezi hata kuezeka bati. Kwa hiyo, sasa hii kipekee kwa uchumi ambao tunataka kwenda nao kwa kweli, ni ngumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishauri Serikali hii technical support ambayo hawa wawekezaji wanakuja nayo kama kofia ya kuwekeza si kweli, hii technical support wanayoisema si kweli! Sisi ambao tupo chini tunajua, wanachokifanya wanachimba na likibaki shimo ambalo wanajua halina mwamba, halina mwendelezo anaondoka anaenda sehemu nyingine. Mbaya zaidi aina hizi za madini mchakato wake haufanyiki Tanzania, haya yanaondoka makinikia kama yalivyo, yanaenda kufanyika huko China.

Mheshimiwa Naibu Spika, at least hata tungekuwa tunachimba Tanzania, tunasema usafishaji wake labda kama dhahabu unafanyika Tanzania, watu wapate ajira, processing zingine zinafanyika Tanzania tungesema kweli at least hata kama unanunua kwa bei ndogo lakini some processes zinafanyika Tanzania na vijana wetu na ndugu zetu wanapata ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, akinunua sand stone na vumbi lake vilevile analibeba kupeleka China, akienda China anatengeneza ananiletea mimi tiles hapa, ananiletea vyoo, ananiletea taa. Kwa hiyo, ukiangalia kabisa ni kwamba thamani haipo, sisi wanatuachia mashimo, hawatuachii kitu na hizo CSR wanazosema hazipo. Kwa sababu, mtu anaahidi hizo CSR kama walivyotangulia wachangiaji wengine, ninaona sasa ni wakati ambao inabidi zifanyike kwa percentage. Kwa sababu mtu hawezi kuchimba madini, akapata thamani ya milioni 500 akajenga tundu moja la choo, hakuna kitu kama hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, hizi sehemu za uwekezaji wa madini, kaka yangu Mavunde anapoteza pesa nyingi.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, unga mkono hoja.

MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuunga mkono hoja, mengine kaka yangu nitakuja tuyaongee. Ahsante sana. (Makofi)