Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Josephine Joseph Kapoma (6 total)

MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Je, Wizara ina mkakati gani wa kuja na solution ya kudumu, na hata kama siyo ya kudumu japokuwa ya muda mrefu kwa zile barabara zinazozibwa viraka? Kwa mfano, kuna baadhi ya barabara unakuta zina mashimo, lakini zinazibwa mara kwa mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa ninataka kujua kama tunaweza tukapata solution ya kuziba viraka ambavyo vitakaa kwa muda mrefu kwa ajili ya ku-save pesa ambazo zinatumika. (Makofi)



NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mbunge wa Mkoa mzima wa Morogoro aliyetoka kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupa maelekezo sisi TARURA ndani ya Serikali kwa ajili ya kuanza mkakati wa kutumia teknolojia mpya ambayo itajenga barabara zetu kwa gharama nafuu na hivyo tutaweza kuyafikia maeneo mengi na kujenga barabara zinazodumu kwa muda mrefu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa huu Mkoa wa Morogoro ambao Wabunge wake wameuliza maswali mengi hapa, Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana, tumejenga mtandao wa barabara kwa kiwango cha lami na sasa tumefikisha karibia kilometa 125. Mradi wa TACTIC ambao tulitekeleza kwa awamu ya kwanza tulipeleka zaidi ya shilingi bilioni 19. Mheshimiwa Rais lengo lake ni kutaka kuona anaufungua Mkoa huu mkubwa ambao ni muhimu kwa uchumi ndani ya nchi yetu. (Makofi)
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nina swali dogo la nyongeza. Kama ikimpendeza Mheshimiwa Naibu Waziri atalijibu au atalichukuwa. Wilaya yetu ya Malinyi tumekuwa tuna shida ya gereza la mahabusu kwa muda mrefu sana. Eneo limepatikana lakini kumekuwa kuna ucheleweshwaji wa kukamilisha ambayo inawafanya wahusika kusafiri umbali mrefu sana kwenda Wilaya ya Ulanga. Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha suala hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimfahamu ili niweze kujibu vizuri; amekusudia mahabusu ya polisi au ya gereza?NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge.

MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, mahabusu ya gereza.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunaongelea kuhusu suala la Jeshi la Polisi lakini kwa sababu Magereza na yenyewe ni sehemu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, lakini ninaomba tu nimjibu Mheshimiwa Kapoma kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli yapo baadhi ya magereza yamekuwa na changamoto ya uchakavu wa majengo. Hata hivyo, moja ya eneo ambalo amelitaja la jimbo lake kwamba wilaya nzima ya Malinyi hakuna gereza na kupeleka eneo la pili; tunakuja na mpango na tutaueleza kwenye bajeti ya mwaka huu kwamba ni mpango gani kwa upande wa Jeshi la Magereza, tutaenda kuboresha magereza katika maeneo ambayo yana uhaba likiwepo eneo lake la Malinyi.
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakazi wa Kata ya Boma Mlimani Luhungo wa Wilaya ya Morogoro Mjini wamekuwa na mgogoro wa muda mrefu na Serikali kwa ajili ya uharibifu wa mazingira. Je, Serikali ina mpango gani wa kuja na mkakati wa kutoa elimu ya mbinu bora za kilimo zitakazozingatia uhifadhi wa mazingira?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimthibitishie tu Mheshimiwa Josephine kwamba, moja ya mkakati wa Serikali ili kuhakikisha kwamba wananchi hawaendelei kuharibu mazingira, ni pamoja na kuhakikisha tunajenga miundombinu bora na ya kisasa, kwa maana ya mabwawa na schemes ili wananchi wale tukishawapanga na kuonesha maeneo ambayo wanafaa kufanya kilimo chao, maana yake hawatakuwa na nafasi ya kwenda kuharibu mazingira katika maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tutaendelea kupeleka timu kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kutunza mazingira, kwa sababu sisi mazingira ndiyo ambayo yanatusaidia kupata vyanzo bora vya maji ambavyo sasa miradi yetu ndiyo maeneo ambayo tumekuwa tukitekeleza.
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, vijana wengi wamekuwa wanapata hizi fursa za mikopo na Serikali imejitahidi sana kufungua hizi fursa, lakini tumekuwa na shida kubwa sana kwa vijana kwa sababu wengi hawana nidhamu ya fedha (finance mistress), lakini sasa Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha Vyama vya Ushirika vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) ili waweze kujengewa uwezo wa kuwa na nidhamu ya fedha? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, Serikali imeendelea kujitathmini kila wakati kuona namna ambavyo mikopo inayotolewa hasa kwenye kundi la vijana inakuwa na ufanisi. Kama alivyoeleza Mheshimiwa Kapoma, ni kwamba kumekuwa na changamoto kubwa sana hasa katika urejeshaji, kwa mfano tukiangalia Mfuko wa Maendeleo wa Vijana, zaidi ya shilingi bilioni 3.9 zimeshindwa kurejeshwa. Tumefanya tathmini kuangalia changamoto ni nini, ikiwepo pia na asilimia nne zinazotolewa kupitia halmashauri zetu. Moja ya changamoto tuliyoiona, ni elimu ya kifedha na ndiyo maana kupitia awamu hii ya mikopo tuliyoitoa, tumeingia utaratibu wa makubaliano rasmi na taasisi ya kifedha hasa CRDB, ambayo kabla kijana hajapata mkopo, huwa anapata fursa ya kupewa mafunzo maalum yanayohusiana na usimamizi wa kifedha, nidhamu pamoja na biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafunzo haya yanakuwa endelevu pia, ili kuhakikisha kwamba wanaendelea kupata elimu hiyo kwa namna endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea wazo lako na ushauri wako juu ya kuwa na SACCOS za vijana, na kama ambavyo Serikali imeendelea kuwezesha kwenye vikundi, tutaendelea kuifanyia kazi ili kuhakikisha kwamba vijana wanafikiwa kwa wingi. Ahsante sana.
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali. Nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, wafanyabiashara hawa waliahidiwa soko hili kuanza tangu Julai, 2025 na mpaka sasa wanashindwa kufanya biashara zao kwa sababu hawajui hatima yao. Je, ni lini sasa Serikali inategemea kuanza mradi huu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tuna miradi kadhaa Mkoa wa Morogoro ambayo inatakiwa, iko chini ya TACTIC. Je, ni lini Serikali inajipanga kuanza kukamilisha kwa sababu mingi iliahidiwa tangu mwaka 2025?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali inatekeleza miradi hii ya TACTIC; tunayo makundi matatu. Kuna kundi la kwanza la miji 12, kundi la pili la miji 15 na kundi la tatu ambalo Ifakara imo ni miji 18.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari imeshaanza utekelezaji wa miradi hii katika makundi ya kwanza na ya pili na utekelezaji unaendelea. Ipo miradi iliyokamilika, ipo ambayo inaendelea na hatua mbalimbali. Baada ya kukamilisha usanifu wa miradi hii ya kundi la tatu, tutaanza utekelezaji wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo la Kilombero na Ifakara kwamba Serikali baada ya kukamilisha usanifu wake tutaanza mara moja utekelezaji wa mradi katika eneo la Ifakara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tunafahamu kuwa iko miji kadhaa ambayo iko kundi la tatu, la kwanza na la pili ambayo inaendelea na utekelezaji wa miradi ya TACTIC. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama ambavyo utekelezaji unaendelea, tutahakikisha inakamilika kwa wakati. Ile ambayo haijaanza, na ambayo iko tier three tutahakikisha nayo inaanza kwa ajili ya kuhakikisha kwamba inatekelezwa kwa wakati.
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa ninataka niulize swali dogo la nyongeza. Nchi nyingi kwa sasa zimeshapiga hatua kubwa sana katika kubadilisha taka kuwa fursa za kibiashara. Je, Serikali ina mkakati gani wa kujielekeza katika mlengo huu ili kutokomeza hili suala la uchafuzi wa mazingira? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana Mbunge wa Mkoa wa Morogoro kwa swali lake zuri, na amekuwa msemaji mzuri sana kuutetea Mkoa wa Morogoro pamoja na Tanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuweka jitihada kubwa katika kuhakikisha kwamba taka zinazozalishwa kwenye mazingira ya shughuli zetu za kiuchumi kwenye miji yetu, kwenye majiji na maeneo mbalimbali zinakuwa recycled, yaani zinarudishwa kutumika kwa ajili ya kuzalisha bidhaa ambazo zitatumika tena kwenye mzunguko wa uzalishaji kwenye maeneo mbalimbali ya kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Serikali inahakikisha kwenye majiji makubwa, mathalan kama ilivyo Dar es Salaam inajenga madampo makubwa na ambayo yataambatana na miundombinu ya viwanda vitakavyoendelea kufanya recycling, yaani marejeo na marejesho ya hizo taka ili ziweze kutumika tena kwa ajili ya kuzalisha bidhaa zitakazotumika kwenye maeneo yetu.