Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Jacqueline Chrisant Mzindakaya (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. JACQUELINE C. MZINDAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa fursa hii. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, aliyetuwezesha kufika hapa siku ya leo. Kipekee ninamshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzidi kuwekeza katika sekta ya kilimo. Pia, kipekee ninaomba nimshukuru Waziri wa Kilimo na Naibu Waziri wa Kilimo kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya ili kutimiza maono ya Serikali ya Awamu ya Sita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoka katika Mkoa wa Rukwa ambao kitovu cha uchumi wake ni kilimo. Mkoa wetu wa Rukwa una mchango katika uzalishaji wa mazao ya chakula kwa kiwango kikubwa na katika takwimu za mwaka jana, Mkoa wa Rukwa ulikuwa ni mkoa wa pili katika mchango kitaifa katika uzalishaji wa mazao ya chakula ikiwemo mahindi, mpunga, ulezi na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba nijikite katika mchango wangu. Kwanza kabisa ninaipongeza Serikali kwa kuendelea kutoa ruzuku katika pembejeo za kilimo. Vilevile, ninaomba pia niipongeze Serikali kwa kuendelea kununua mazao kutoka kwa wakulima kupitia NFRA. Ninakwenda kutoa ushauri ama ombi langu hususan katika Mkoa wangu wa Rukwa. Uzalishaji katika Mkoa wetu wa Rukwa ni mkubwa sana hivyo kiwango ambacho Serikali wanachukua mazao kwa wakulima wa Mkoa wa Rukwa bado hakikidhi uhitaji na kupelekea wakulima wengi kubaki na mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaishauri Serikali yetu sikivu ili iweze sasa kuongeza wigo wa masoko kwa kutujengea masoko ya mazao katika Mkoa wetu wa Rukwa na Tanzania nzima kwa ujumla wake. Vilevile, tunaomba pia mipaka iendelee kufunguliwa ili wakulima wetu waweze kupata sehemu ya uhakika wa masoko ya kuuza mazao yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, ninaomba pia niipongeze sana Serikali kwa kuendelea kujali kwa kutoa elimu ya kilimo kupitia Maafisa Ugani ili kuweza kuleta kilimo chenye tija. Kwa mkoa wetu wa Rukwa tuna upungufu wa Maafisa Ugani kwa 42%. Hivyo basi, ninaiomba pia Serikali yetu sikivu iweze kuhakikisha tunapata ongezeko la Maafisa Ugani hao ili waweze kufika maeneo yote na kwenda kutoa elimu ya kilimo ili hatimaye tukawe na kilimo chenye tija kwa kuwapa elimu bora wakulima wetu wa Mkoa wa Rukwa ili na uzalishaji uweze kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na hilo, ninaomba pia nichangie kupitia skimu za umwagiliaji. Tunaishukuru Serikali kwa kuelekeza pesa Mkoa wetu wa Rukwa kwa ajili ya kujenga skimu za umwagiliaji. Kuhusu skimu hizo za umwagiliaji, ninashauri kabla ya kuleta skimu mpya za umwagiliaji, tukamalize kwanza skimu ambazo hazijakamilika zikiwemo Skimu za Umwagiliaji za Singiwe, Sakalilo, Katongolo, Katuka na Ng’ongo. Kwa hiyo, tunaomba kukamilishwa kwa skimu hizo ili wakulima wa Rukwa wapate uhakika wa kuwa na kilimo endelevu na chenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia niongeze kwa kusema tunaipongeza pia Serikali kwa kuthamini kupitia ruzuku, lakini ruzuku zinatolewa tu katika pembejeo. Tunaomba ruzuku itolewe pia katika viuatilifu ambavyo ni dawa za wadudu. Mara kadhaa tunaona wakulima wanapata changamoto ya bei ambazo siyo rafiki katika viuatilifu. Kwa hiyo, tunaomba pia Serikali ielekeze kiwango cha ruzuku katika viuatilifu ili wakulima hao wawe na uhakika wa kupata dawa za kukabiliana na wadudu wanaovamia mazao na kupunguza uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho na la muhimu ni Programu ya BBT ambayo nimemsikia katika bajeti Mheshimiwa Waziri amezungumza, ambayo inawezesha wanawake na vijana katika kujinyanyua katika kilimo. Mkoa wetu wa Rukwa una maeneo makubwa lakini mpaka hivi leo tunakosa programu hiyo ambayo itakwenda kumnyanyua mwanamke wa Rukwa, itakwenda kumnyanyua kijana wa Rukwa kiuchumi kupitia kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaiomba Serikali yetu kupitia bajeti hii, katika hiyo Programu ya BBT, Mkoa wetu wa Rukwa nao uwepo miongoni mwa mikoa ambayo itakapelekewa programu hiyo. Vijana wetu wawezeshwe elimu, wawezeshwe pesa ili waweze kujikita katika kilimo endelevu ambacho kitatunyanyua katika kipato cha mtu mmoja mmoja kwa Wanarukwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninaunga mkono hoja kwa asilimia zote. Ninaomba nimalizie kwa falsafa ya Baba yetu wa Taifa aliyesema kilimo ni uti wa mgongo kwa sababu ndiyo msingi wa maendeleo ya uchumi na maendeleo ya jamii ya nchi yetu ya Tanzania. Hivyo basi, tupitishe bajeti hii na tuendelee kujikita katika kunyanyua sekta ya kilimo. Ahsante sana.