Supplementary Questions from Hon. Khalid Mussa Nsekela (3 total)
MHE. KHALID M. NSEKELA: Mheshimiwa Spika, kwanza ninaungana na wenzangu kumtakia heri ya kuzaliwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ninaishukuru Serikali kwa kutuletea mkandarasi wa kujenga Barabara ya lami kutoka Kyerwa kwenda Omurushaka, kilometa 50. Hata hivyo, speed yake ni ndogo sana. Je, Serikali ina mkakati na maelekezo gani ya kumsimamia mkandarasi huyu ili amalize barabara hii ili kukidhi kilio cha wananchi wa Kyerwa? Ninakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli mkandarasi huyu anakichofanya ni sanifu jenga Barabara ya Kyerwa kwenda Omurushaka. Nimwagize Meneja na Mhandisi Mshauri anayemsimamia ahakikishe kwamba huyu mkandarasi, kwa sababu alikwishalipwa fedha ya awali, aweze kwenda kwa kasi inayotakiwa kulingana na mpango wake wa kazi ambao ameupanga na tumeukubali. (Makofi)
MHE. KHALID M. NSEKELA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi ya kuuliza swali hili la nyongeza. Kwanza naishukuru Serikali sikivu ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia wahudumu 58 katika dirisha hili la ajira za afya kwa Wilaya ya Kyerwa.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, Kituo cha Afya cha Nkwenda ni kikubwa na kinatoa huduma zaidi ya Kata 19 na sometime kinatoa huduma nje ya Wilaya ya Kyerwa, lakini kituo hiki hakina gari ya uhakika ya wagonjwa (ambulance), je, ni lini Serikali itatupatia gari la uhakika kwa ajili ya kutoa huduma safi kwa kituo hicho? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT.JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, tunakumbuka sote humu ndani katika kipindi cha miaka mitano Serikali imenunua jumla ya magari ya kubebea wagonjwa 316, pamoja na magari ya wakaguzi 212 na ambulance za awamu ya kwanza tumeshazigawa katika Halmashauri ambazo ziliainishwa. Nimhakikishie kuwa, awamu ya pili kituo hiki kitakuwa wanufaika wa gari la ambulance.
MHE. KHALID M. NSEKELA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, je, kwa kuwa Wilaya ya Kyerwa imekuwa na changamoto ya muda mrefu ya huduma ya maji, Serikali haioni haja ya kuifanya Wilaya ya Kyerwa kuwa kanda maalum ya usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya maji?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuambatana na mimi na kufika Kyerwa kujionea changamoto ya maji iliyokuwa? Ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge. Kwa kweli moja ya ajenda yake katika Bunge hili ni kuhusu suala zima la Wanakyerwa kuweza kupata huduma ya majisafi na salama. Sisi kama Wizara ya Maji ni wilaya ambayo tumeiangalia kwa kina sana. Ni moja ya wilaya tulizoifanyia tathmini, hasa katika kipindi hiki kwamba ni wilaya ambayo ina vijiji takribani 99, tumeshafikisha zaidi ya vijiji 55. Ipo miradi ya kimkakati ambayo tunaitekeleza katika kuhakikisha wananchi wa Kyerwa wanapata huduma ya majisafi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunao mradi wa Runyinya-Chanya zaidi ya shilingi bilioni 3.7, Kimuli-Nyanga zaidi ya shilingi bilioni mbili, Kaisho-Isingiro zaidi ya shilingi bilioni 1.9. Ninataka niwahakikishie, tutaisimamia Wanakyerwa waweze kupata huduma ya majisafi na salama, na mimi baada ya Bunge nipo tayari kuongozana na wewe kufika katika jimbo lako la Kyerwa. Ahsante sana.