Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. George Venance Lugomela (2 total)

MHE. DKT. GEORGE V. LUGOMELA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa tuna Kata ya Ipililo, kimejengwa kituo cha afya katika Kata ile na Kata ya Ipililo ndiyo Kata yenye wakazi wengi katika Jimbo la Maswa Mashariki. Ninaomba kuuliza, je, kituo cha afya hiki kitaanza kufanya kazi lini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge aliuliza swali la nyongeza kuhusu kituo cha afya Kata ya Maswa. Kwanza tumejielekeza kutoa katika vile vituo ambavyo havijakamilika kwanza viweze kutoa huduma zile za OPD. Kwa hiyo, mimi na Mheshimiwa Mbunge tutakaa chini baada ya Bunge hili leo, ili tuone namna gani katika kituo chetu hiki cha afya kitaanza kutoa huduma za msingi kwa ajili ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. DKT. GEORGE V. LUGOMELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa vile barabara hii ilikuwa na changamoto ya kupitika kabla ya mvua za mwaka huu na mvua za mwaka huu zimenyesha kwa wingi na kuiharibu zaidi. Je, ni ipi tathmini mpya ya Serikali ya kuhakikisha kwamba ule uharibifu ambao umetokea mwaka huu unafanyiwa kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kuambatana nami kwenye jimbo ili kujionea hali halisi ya barabara hii, lakini pia na barabara nyingine katika Wilaya ya Jimbo la Maswa Mashariki?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. George Venance Lugomela, Mbunge wa Maswa Mashariki amefuatilia sana barabara hii Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI na sisi tunamhakikishia kwamba tutahakikisha barabara hii inaendelea kujengwa. Tunafahamu kwamba kumekuwa na mvua nyingi na uharibifu umeendelea kutokea, hasa msimu huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ujenzi ambao umekuwa ukifanyika, tunaendelea kufanya tathmini ya uharibifu mwingine ulioongezeka kwa ajili ya kutenga bajeti kwa ajili ya kwenda kufanya ukarabati huo. Kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Lugomela kwamba, tutafanya tathmini na kazi hiyo inaendelea na taarifa tunaendelea kuzipokea, Ofisi wa Waziri Mkuu, TAMISEMI kwa barabara hiyo, lakini na barabara nyingine zote kote nchini kwa ajili ya kutenga fedha kwa ajili ya matengenezo ya dharura, lakini na matengenezo ya mara kwa mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, niko tayari kuambatana na Mheshimiwa Dkt. Lugomela kwenda Maswa Mashariki. Tutakaa mimi na wewe Mheshimiwa Mbunge tupange ratiba na tuone lini tutapata fursa twende tukakague barabara hii na barabara nyingine kwa lengo la kuhakikisha kwamba tunaboresha usafiri na usafirishaji kwa wananchi. ahsante sana.