Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2025-2030 Session 3 Sitting 32 Regional Administration and Local Government Authorities Ofisi ya Waziri Mkuu-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) 373 2026-05-19

Name

Devotha Daniel Mburarugaba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DEVOTHA D. MBURARUGABA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha Wabunge wa Viti Maalum wanashirikishwa katika utoaji wa mikopo ya 10% kwenye halmashauri?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Daniel Mburarugaba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatatanrmbua umuhimu wa kuwashirikisha Waheshimiwa Wabunge wote wakiwemo wa Viti Maalum, katika utoaji na usimamizi wa mikopo ya 10% katika halmashauri. Kufuatia maboresho ya sheria, kanuni na mwongozo wa utoaji na usimamizi wa mikopo hiyo wa mwaka 2024, Serikali imeweka utaratibu wa ushirikishwaji wa Waheshimiwa Wabunge kuhusu hatua za utoaji mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chini ya utaratibu huo, Waheshimiwa Wabunge wanatakiwa washirikishwe kikamilifu kupitia vikao vya kisheria vya halmashauri, hususani Baraza la Madiwani na Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ambapo hupokea taarifa, kujadili na kutoa maoni kuhusu upangaji, ugawaji na usimamizi wa mikopo ya 10% kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Aidha, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI imewaelekeza Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwataarifu na kuwaalika Waheshimiwa Wabunge kushiriki kwenye shughuli za utoaji mikopo katika halmshauri zao ili kuwapa fursa ya kuhamasisha, kuelimisha na kufuatilia shughuli za vikundi kutokana na mikopo hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inazisistiza halmashauri zote nchini kuendelea kuimarisha utaratibu wa mawasiliano na kuwapa taarifa kwa wakati Waheshimiwa Wabunge kuhusu ratiba za vikao, orodha ya wanufaika na mwenendo wa urejeshaji wa mikopo ili kuongeza uwazi na uwajibikaji. Ahsante.