Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Naghenjwa Livingstone Kaboyoka
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza: - Je, lini lami itawekwa kwenye Barabara ya kutoka Mroyo hadi Ndungu, Wilayani Same.
Supplementary Question 1
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa, kupande hiki cha Mroyo – Ndungu kimetandazwa kokoto ambazo magari mengine yakipita, haya yaliyopo nyuma yanavuviwa vioo, kwa ajili ya zile kokoto zinarukaruka sana, na Kwa kuwa, pembezoni mwa hii barabara kwa mwaka wa nne huu kumewekwa udongo ambao naamini ulikuwa ni mchanga na umeota majani, je, Serikali ina mpango gani wa kuchukua hatua za dharura kusaidia kuondoa huu udongo kwa sababu hata gari lililopo nyuma ambapo kokoto zinarukaruka, haliwezi hata kukwepa zile kokoto?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa, Serikali imeshatoa malipo ya awali kwa kipande hiki cha Ndungu – Mkomazi kwa mkandarasi, na kwa kuwa, mkandarasi huyu ameshaweka kambi ile, je, Serikali inamsimamia mkandarasi kwamba, aanze hiyo kazi ya kuweka lami wakati gani au kipindi kipi kinachokuja? Ahsante sana.
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI K.n.y. WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Kaboyoka kwa jinsi ambavyo anasimamia eneo lake na kuhakikisha kwamba, tunatekeleza vizuri majukumu yetu. Natumia nafasi hii pia kumkumbusha Mheshimiwa Kaboyoka kwamba, awali wananchi wa Kilimanjaro, hususan Same, walikuwa wanaiomba Serikali ikamilishe au ianze ujenzi wa mradi huu, lakini huko nyuma hatukuweza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Sita imeamua rasmi kuijenga barabara hiyo kwa maslahi ya Taifa letu, lakini kwa sasa hivi mkandarasi hajalipwa, hivyo kazi imesimama kidogo kwa kuwa ni muhimu pale tunapokuwa na miradi, barabara hizo zipitike bila kuleta usumbufu kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamwelekeza Mkurugenzi Mkuu au Mtendaji wa TANROADS, kupitia Meneja wa Mkoa husika wa Kilimanjaro, aende katika eneo husika atazame changamoto inayozungumzwa na Mheshimiwa Mbunge. Kama kutakuwa na changamoto hiyo kwa ukubwa huo, waifanyie kazi, ili wananchi wapite bila changamoto yoyote katika eneo hilo kwa sababu, katika maeneo yote ambayo tunatekeleza miradi ya barabara au miradi mingine, barabara inapaswa kuwa passable, yaani iendelee kupitika wakati huo mradi unaendelea kutekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, amezungumza pia kuhusu uendelezaji wa barabara hiyo. Namkumbusha Mheshimiwa Kaboyoka kwamba, barabara hii yenye kilomita 98 Serikali imekamilisha usanifu mwaka 2018/2019 na ilifanya maamuzi ya kuanza kuijenga 2021 kwa awamu ya kwanza, ambapo zilikuwa ni kilomita 5.2.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyozungumza tunategemea mwishoni mwa mwaka huu, 2025, ikamilike awamu ya pili ya Ndungu – Mkomazi kilomita 36. Tumeshampata mkandarasi ambaye ameanza kufanya kazi na kipande cha tatu cha Same – Mahore, kilomita 56, tupo kwenye hatua ya manunuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia mara tu wakandarasi wanapolipwa advance payment au fedha za malipo ya awali wanaelekezwa waanze kufanya kazi. Hivyo basi, kwa maeneo yote ambayo wameshalipwa nawaelekeza wakandarasi waanze kufanya kazi mara moja, ili tuweze kuhakikisha miradi hiyo inakamilika.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved