Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Juma Ramadhani Mustafa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igalula
Primary Question
MHE. JUMA R. MUSTAFA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga maeneo ya malisho katika Jimbo la Igalula ili kupunguza migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji?
Supplementary Question 1
MHE. JUMA R. MUSTAFA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Wizara. Kwanza kabisa ninapenda kuwapongeza kwa kazi nzuri ambazo wanaendelea kuzifanya, lakini ninampongeza Mheshimiwa Rais, wananchi wa Jimbo la Igalula wanamshukuru kwenye chanjo ya ruzuku, kuondoa na utambuzi wa mifugo.
Mheshimiwa Spika, nina swali moja la nyongeza; je, Serikali ina utaratibu gani wa kisheria na kiutendaji, ili kuhakikisha sasa maeneo haya yaliyotengwa hayavamiwi na hayabadilishiwi matumizi ili kuweza kuepuka migogoro kati ya wakulima na wafugaji ndani ya Jimbo la Igalula?
Name
Dr. Jafar Rajab Seif
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busanda
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. RAJAB S. JAFAR): Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juma Mustafa Kawamba, Mbunge wa Igalula, Halmashauri ya Uyui, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na Sheria mbalimbali ambazo zimekuwa zikitu-guide na zimepitishwa na Bunge lako Tukufu. Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999, hii ilikuwa inatoa hati ya Hatimiliki ya Kimila, lakini kuna Sheria ya Ardhi Namba Sita ya Mwaka 2007, ambayo imeainisha mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji, lakini kuna maeneo ya kilimo na malisho ya mifugo, yote yameainishwa katika Sheria hii. Sambamba na sheria hizi pia, kuna Sheria Namba 287, ambayo imewezesha halmashauri kutunga Sheria Ndogo. Kwa hiyo, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaziagiza Halmashauri zote nchini zifuatishe Sheria hizi na kuona zinatatua migogoro ya ardhi katika maeneo yao.
Name
Amosy William Maganga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Primary Question
MHE. JUMA R. MUSTAFA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga maeneo ya malisho katika Jimbo la Igalula ili kupunguza migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji?
Supplementary Question 2
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, kwanza ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii kuweza kuuliza swali la nyongeza. Wananchi wa Wilaya ya Sikonge kwa hivi sasa wanakabiliwa sana na ufinyu wa maeneo, kwa ajili ya shughuli za kiuchumi. Wilaya ya Sikonge ina jumla ya mapori tisa na kati ya haya, yaliyo mengi ni mapori ya akiba. Je, Serikali, ni wakati gani sasa haya mapori ya akiba yataanza kutumika, kwa ajili ya hao wananchi, ukizingatia kwamba, kwa kweli wananchi wanahitaji kuendesha shughuli zao za kiuchumi na hasa kilimo, ufugaji, pamoja na urinaji wa asali na kwa hivi sasa, hata viashiria vya uvunjifu wa amani vinaanza kuonekana?
SPIKA: Mheshimiwa swali lako limeshaeleweka. Ahsante.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Name
Dr. Jafar Rajab Seif
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busanda
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. RAJAB S. JAFAR): Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa Sikonge, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI. Utakumbuka Bunge lako hili kipindi cha Mwaka 2021 mpaka 2025 iliundwa Kamati ya Mawaziri Nane, ambayo ilizunguka nchini kote kuainisha maeneo haya na kufanya tathmini. Hivyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge tathmini ikikamilika kwa wakati watatengewa maeneo ili wapate kufanya shughuli za uzalishaji mali, kilimo na ufugaji.
Name
Agnes Mathew Marwa
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JUMA R. MUSTAFA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga maeneo ya malisho katika Jimbo la Igalula ili kupunguza migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji?
Supplementary Question 3
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, Serikali iliahidi kuwatengea maeneo wananchi wa Wilaya ya Bunda, Nyatwali, kwa ajili ya ufugaji ambapo maeneo hayo yalitwaliwa na Serikali kurudishwa hifadhini. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka kuwatengea wananchi, hasa wananchi wa Mkoa wa Mara kwa ujumla, maeneo ya kulishia wanyama?
Name
Dr. Jafar Rajab Seif
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busanda
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. RAJAB S. JAFAR): Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu hapo awali, swali hilo linaenda sambamba na swali la Mbunge kutoka Sikonge kwa maana ya kwamba ile Kamati ya Mawaziri Nane bado wanafanya kazi na tathmini ili tuweze kuwatengea maeneo wananchi wetu waweze kuendelea na shughuli za uzalishaji.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved