Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Hawa Subira Mwaifunga
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:- Je, lini changamoto ya Mawasiliano Jimbo la Tabora Mjini Kata za Ikomwa, Ndevelwa, Ntalikwa, Kabila, Kalunde na Itetemia itamalizika?
Supplementary Question 1
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; bado Jimbo la Tabora Mjini kwenye kata za pembezoni nilizozitaja hapo zina changamoto kubwa sana ya mawasiliano. Kuna baadhi ya maeneo walitoa maelekezo ikajengwe minara hiyo ya Halotel lakini haijajengwa. Nini mpango wa Serikali kwenda kujenga hata hiyo Minara ya Halotel wanayoisema ili wananchi wa kata hizi za pembezoni zilizoko kwenye Jimbo la Tabora Mjini waweze kupata mawasiliano ya uhakika?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; pamoja na sasa hivi kuwa tuko kwenye awamu ya uwezo wa mitandao yetu 5G lakini mpaka leo Tabora Mjini bado tunapokea mawasiliano kwa kutumia 2G. Nini mpango na mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba wanapeleka minara yenye nguvu ya uwezo wa kupeleka 5G ili wananchi wa Jimbo la Tabora Mjini ambalo linakua kwa kasi waweze kupata mawasiliano ya uhakika? (Makofi)
Name
Switbert Zacharia Mkama
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ukerewe
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ninaomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusu ujenzi wa minara kwenye maeneo aliyoyataja pembezoni mwa Mji wa Tabora, kama nilivyoeleza kwenye jibu la swali namba 74 nilieleza kwamba tunatambua changamoto ya mawasiliano katika maeneo mbalimbali nchini na tuna mkakati mahususi wa miaka mitano kuanzia mwaka huu 2025 mpaka 2030 ambapo tutayafikia maeneo yote yenye changamoto za mawasiliano ikiwemo ni pamoja na eneo lake la Tabora Mjini.
Mheshimiwa Spika, kwenye maeneo ambayo yana minara na ambayo bado yana changamoto ya mawasiliano, tutatuma wataalam wetu wakafanye tathmini na pale ambapo kutaonekana kuna uhitaji wa kuiongezea nguvu hiyo minara tutaiongezea nguvu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu changamoto ya kuwepo minara ya 2G katika maeneo ya mjini. Ni kweli bado kuna maeneo hapa nchini yanasoma minara ya 2G lakini kwa maeneo ya mjini mengi yameshafikiwa na minara ya 3G na 4G. Iwapo bado kuna maeneo ya Mjini Tabora yanasoma minara ya 2G, ninaomba kupitia Bunge lako Tukufu kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nimwelekeze Mkurugenzi Mkuu wa TCRA apeleke timu yake ya wataalam kufanya tathimini katika eneo la Jimbo la Tabora Mjini ili kutambua ni kwa nini bado kunasoma minara ya 2G ambayo katika maeneo ya mjini mengi hakuna changamoto kama hiyo.
Name
Shaffin Ahmedali Sumar
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uyui
Primary Question
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:- Je, lini changamoto ya Mawasiliano Jimbo la Tabora Mjini Kata za Ikomwa, Ndevelwa, Ntalikwa, Kabila, Kalunde na Itetemia itamalizika?
Supplementary Question 2
MHE. SHAFFIN A. SUMAR: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo. Kwa kuwa tatizo la mawasiliano ni la nchi nzima na katika Jimbo langu la Uyui tatizo kama hili lipo na linasumbua sana katika Kata ya Ibili, Ibelamirundi, Ndono, Makazi na Bukumbi. Je, ni lini Serikali itapeleka wataalam ili waangalie maeneo ambayo yanafaa kuweka mnara waweze kuweka haraka iwezekanavyo ili wananchi waache kupanda miti kutafuta mawasiliano? (Makofi)
Name
Switbert Zacharia Mkama
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ukerewe
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Uyui kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ninaomba nichukue nafasi hii pia kumwelekeza tena Mkurugenzi Mkuu wa TCRA kutuma timu ya wataalam katika Jimbo la Uyui kuweza kufanya tathmini na kutambua changamoto zilizopo za mawasiliano katika jimbo hilo.
Name
Ester Amos Bulaya
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:- Je, lini changamoto ya Mawasiliano Jimbo la Tabora Mjini Kata za Ikomwa, Ndevelwa, Ntalikwa, Kabila, Kalunde na Itetemia itamalizika?
Supplementary Question 3
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza. Katika Jimbo la Bunda Mjini kata za pembezoni pia kuna changamoto ya mawasiliano kama Kunzugu, Bukole, Nyamatoke na Mihali. Ni lini changamoto hiyo itatatuliwa?
Name
Switbert Zacharia Mkama
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ukerewe
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Mheshimiwa Bulaya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tuna mkakati maalum na mahususi ambao tunauandaa Wizarani na utakamilika hivi karibuni. Mkakati huu tunakusudia kuyafikia maeneo yote yenye changamoto za mawasiliano likiwemo Jimbo la Mheshimiwa Bulaya. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa kwamba katika mkakati wetu huu na siku si nyingi tutamfikia katika maeneo yake yenye changamoto na nimpongeze pia kwa jinsi anavyowapigania wapigakura wake wa Bunda Mjini. Kwa kweli wamechagua Mbunge mahiri. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved