Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Sheila Edward Lukuba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SHEILA E. LUKUBA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga mfereji mkubwa kuelekeza maji Mto Ngerengere ili kunusuru Wakazi wa Kata ya Kihonda na Lukobe kwa mafuriko?
Supplementary Question 1
MHE. SHEILA E. LUKUBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majawabu mazuri ya Serikali, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; Kata za Kihonda na Lukobe hazikuwahi kupata mafuriko huko nyuma, lakini baada ya ujenzi mkubwa wa Reli ya Kisasa ya SGR kumeibuka makorongo makubwa yaliyopo Kwa Wagogo, Juhudi na Azimio. Makorongo haya kwa ujumla yamekuwa yakisababisha mafuriko makubwa na kuathiri mali na miundombinu ya wananchi. Je, lini Serikali itajenga miundombinu imara ili kudhibiti mafuriko na ili kunusuru maisha ya wananchi hawa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Mkoa wa Morogoro ni wanufaika wakubwa wa Mradi wa SGR na sisi sote ni mashahidi tumekuwa tukitumia, lakini kuna changamoto ya vivuko katika Kata ya Lukobe, Mtaa wa Tushikamane, karibu na Shule ya Sekondari Mji Mpya na Mtaa wa Kambi Tano ambao ni mpaka wa Mvomero na Morogoro Mjini. Nini kauli ya Serikali juu ya vivuko hivyo? Kwa sababu imekuwa ahadi ya muda mrefu kwamba wananchi hawa watatengenezewa, nini kauli ya Serikali? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Sheila Edward Lukuba, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Morogoro. Amekuwa mfuatiliaji wa karibu sana wa shughuli za ustawi wa wananchi wa Mkoa wa Morogoro, lakini na Watanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia tu Mheshimiwa Mbunge Lukuba kwamba, kwanza Serikali inatambua kwamba tuna changamoto ya mafuriko katika mitaa ya wananchi katika Kata ya Lukobe na Kihonda Morogoro Manispaa na tayari tumeshatuma wataalam. Timu ya wataalam inafanya tathmini maeneo gani yanahitaji miundombinu ya aina gani na gharama za fedha zinazohitajika ili baada ya kukamilisha tathmini ya mahitaji na design tutapeleka fedha kwa ajili ya kujenga mfereji wa kupeleka maji yale ya mafuriko kwenye Mto Ngerengere ili kuondoa mafuriko hayo. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Kihonda na Lukobe kwamba, Serikali inalifanyia kazi na tutakwenda kumaliza changamoto hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, tunafahamu kwamba viko vivuko ambavyo vinahitaji kujengwa na kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema, Kivuko cha eneo la Tushikamane lakini pia Kivuko cha Mtaa wa Kambi Tano. Ninaomba nimhakikishie tu kwamba, wakati wa ujenzi wa mfereji huo tutapeleka package ambayo pia itakwenda kujenga madaraja, lakini pia kujenga vivuko hivyo ili kuondoa changamoto hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha na ahsante sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved