Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Tinnar Andrew Chenge

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

Je, kuna mpango gani kufikisha huduma ya Maji Safi na Salama kutoka Ziwa Victoria kwa Wananchi wanaoishi umbali zaidi ya Km 12 kutoka Bomba Kuu?

Supplementary Question 1

MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na niendelee kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mradi huu kubwa sana wa maji, na ninashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa jamii ya wananchi wa Mkoa wa Simiyu ni wafugaji na wakulima, je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga bomba lingine sambamba na hili la majighafi kwa ajili ya shughuli za mifugo pamoja na kilimo cha umwagiliaji ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Mkoa wa Simiyu una wilaya tano, na kati ya wilaya hizo wilaya yenye changamoto kubwa sana sana ya maji ni Wilaya ya Meatu. Je, Serikali haioni kwamba kuna sababu za msingi za kuingiza Wilaya ya Meatu kwenye awamu ya kwanza ya ujenzi wa Bomba la Ziwa Victoria? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana.

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tinnar Andrew Chenge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, ninamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza swali muhimu sana na la msingi linalobeba matamanio ya wananchi wa Mkoa wa Simiyu, lakini pia niendelee kumpongeza na kumshukuru kwa kutoa ushirikiano mzuri sana kwa Wabunge wa majimbo katika Mkoa wa Simiyu. Vilevile, ninampongeza kwa kutafsiri kwa uhalisia majukumu ya Kibunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu ni mkubwa sana. Ni mradi wa takribani shilingi bilioni 440 ambapo Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa kwa ajili ya wananchi wa Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza, katika kuhakikisha kwamba tunakabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kurejesha uoto wa asili, Serikali imepanga kupanda miti na nyasi katika maeneo ya wilaya zote tano za Bariadi, Busega, Itilima, Maswa na Meatu, lakini tunayo maeneo ambayo tuna ekari karibia 11,200 ambapo mpaka sasa tumeshafikia 30% ya utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tunao mpango wa kukarabati mabwawa ili kuhakikisha sasa kwenye suala la umwagiliaji, basi iweze kufanyika bila kuwa na changamoto yoyote. Upande wa Meatu, ni kweli kabisa katika wilaya ambazo zina ukame, Meatu kwa Mkoa wa Simiyu inaongoza.


Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha huo, usanifu wa mradi huu ambapo tunajenga tanki letu kwenye intake yetu pale Nyashimo, pia tunajenga mtambo wa kutibu maji na kuyasafisha. Pia, tuna ujenzi wa matanki karibia sita ambayo yamebeba kwa upana wake mahitaji ya wilaya zote tano ikiwemo Meatu. Kwa kile kilima kilichoko Ibumba pale Itilima, kuna tanki la lita milioni 10 ambalo ndilo litakalochukua maji kutoka pale Itilima kupeleka katika Wilaya za Meatu pamoja na Maswa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, tunaamini kwamba phase ya kwanza itakapokamilika, phase ya pili itabaki sasa ni kusambaza maji katika Wilaya ya Meatu pamoja na Maswa na mradi utakuwa umekamilika kwa 100%, ahsante sana. (Makofi)

Name

Adonis Alfred Bitegeko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Primary Question

Je, kuna mpango gani kufikisha huduma ya Maji Safi na Salama kutoka Ziwa Victoria kwa Wananchi wanaoishi umbali zaidi ya Km 12 kutoka Bomba Kuu?

Supplementary Question 2

MHE. ADONIS A. BITEGEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Ningependa kufahamu Serikali ina mpango gani wa kutekeleza ahadi yake ya muda mrefu ya kufikisha huduma ya majisafi na salama katika Kata za Mayondwe na Muhutwe katika Wilaya ya Muleba?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni ahadi ambayo imetolewa na Serikali ya Awamu ya Tano, na utekelezaji ulishafanyika katika Kata za Kemondo na Kanazi kwa Wilaya ya Bukoba. Kwa hiyo, ilikuwa inasubiriwa kwamba mradi huu utafika katika Wilaya ya Muleba katika kata hizo.

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Muleba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi za Serikali, sambamba na ahadi kutokana na Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, ndiyo msingi wa utekelezaji, ndiyo msingi wa mipango yetu; mpango wa mwaka mmoja, na miaka mitano. Ndiyo msingi wa kutenga bajeti kuhakikisha sasa ahadi hizo zinaenda kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe hofu, ahadi ya Serikali ambayo ilitolewa, aidha na viongozi wakuu wa Kiserikali, ama kwenye Ilani ya uchaguzi, ama kiongozi yeyote ambaye alifika katika eneo husika na kutoa hiyo ahadi, ahadi hizo zitatekelezwa na bila kuwa na changamoto yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna juhudi ambazo tayari zimeshafanyika katika jimbo la Mheshimiwa Mbunge, na tunaamini kwamba miradi iliyopo katika hatua mbalimbali, tutaikamilisha, na baada ya hapo, tutaangalia kama kutakuwa na changamoto nyingine. Ahsante sana.