Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Jafari Wambura Chege
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rorya
Primary Question
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:- Je, lini Mradi wa Maji wa Miji 28 ya Rorya – Tarime utakamilika?
Supplementary Question 1
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi kuuliza maswali ya nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri, pamoja na majibu ya kwamba mradi huu unatakiwa kukamilika ndani ya mwaka 2026/2027, lakini ninadhani wewe unafahamu kwamba mradi huu umesimama, mkandarasi hayuko site, na anadai zaidi ya shilingi bilioni saba ili aweze kurudi kuendelea kukamilisha kazi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni mara ya tatu sasa ninasimama ndani ya Bunge hili kuulizia kuhusu mradi huu na mkandarasi hayuko site mpaka sasa. Ninataka nijue Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini mkandarasi huyu atalipwa hiyo shilingi bilioni saba ili aweze kurudi site aweze kukamilisha mkataba huu kwa muda ambao amepewa kwa mujibu wa mkataba?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, ni kwamba Wilaya ya Rorya imezungukwa na maji zaidi ya 77%, nchi kavu ni sehemu ya 23% peke yake, lakini katika vijiji 86, vijiji vyenye miundombinu ya maji ni 47 pekee yake, vijiji 39 havina miundombinu, na havina maji yoyote. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba Wilaya ya Rorya kwa ujumla wake sasa inapata miradi ya maji ili kuwanufaisha wananchi kwa ujumla wake?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri na kwa kuwasemea wana Rorya, na kwa mradi huu atakuwa anawasemea Wanarorya na Wanatarime.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa mradi huu unatekelezwa kwa mfumo wa design and build. Maana yake ni kwamba, inapofikia upande wa ku-design, siyo lazima mkandarasi awe site, anaweza akaendelea ku-design wakati akiwa eneo lingine, baada ya kukamilisha kipande ambacho anaki-design anahamia site kwa ajili ya kutekeleza. Kinachofanyika mpaka sasa, Wizara ya Maji ndani ya wiki mbili hizi mkandarasi tumemlipa shilingi bilioni 1.6.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua umuhimu wa mradi huu na ndiyo maana tayari imeshatoa hizo fedha. Ninamwomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira ili mradi huu utekelezwe kwa ubora stahiki, lakini na thamani ya pesa. Tunafahamu kwamba kuna hamu na kiu ya wananchi wake kupata huduma hii ya majisafi na salama kutoka Ziwa Victoria. Tutahakikisha kwamba watapata hayo majisafi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa Vijiji vya Rorya kama ambavyo amesema kwamba 77% vimezungukwa na maji, ni kweli kabisa. Nimtoe hofu, tunavyo vijiji 1,575, vikiwemo hivi vijiji 39 na tumeshaanza kuweka mpango kuanza kuhakikisha kwamba vijiji hivi ambavyo viko katika mpango wa miaka mitano, kila mwaka tutakuwa tunapunguza vijiji kadhaa, mpaka tutakapofikia katika target yetu ya mwaka 2030, tutakuwa tumekamilisha vijiji vyote ambavyo vitakuwepo Rorya na nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana.
Name
Nuru Issa Kashakari
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Kusini
Primary Question
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:- Je, lini Mradi wa Maji wa Miji 28 ya Rorya – Tarime utakamilika?
Supplementary Question 2
MHE. NURU I. KASHAKARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wilaya ya Uvinza, Jimbo la Kigoma Kusini, kuna miradi mikubwa minne ambayo imegharimu kiasi cha shilingi bilioni 15 ambayo ni Kijiji cha Kazuramimba, Kijiji cha Makizega, Kijiji cha Ilagala, na Kalenge. Je, ni lini Serikali itakamilisha miradi hii? (Makofi)
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya majimbo yaliyokuwa na changamoto kubwa sana katika upande wa maji, Jimbo la Uvinza lilikuwa na changamoto kubwa sana. Kwa uwekezaji mkubwa katika jimbo hili na katika kijiji ambacho amekitaja, Kijiji cha Kazuramimba, ambapo mimi nilifika katika tanki ambalo lilikuwa limejengwa likaachia. Tukarejea tena kufanya design nyingine na tukajenga tanki ambalo mpaka sasa liko imara kabisa na limeshaanza kutoa huduma ya majisafi na salama katika eneo lile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzuri ni kwamba katika eneo la Kazuramimba nilizunguka katika ile mitaa yote, nikajionea mpaka kwenye zile shule, na ninafahamu namna hali ilivyokuwa na sasa ilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe hofu katika maeneo ambayo yamebaki hayana majisafi na salama, tunao mkakati wa kuhakikisha sasa tunaenda kuyafungua maji ya lile Tanki la Kazuramimba ili maeneo yote ya shule yanayozunguka pale yapate huduma ya majisafi na salama, na miradi mingine ambayo tayari tumeiingiza kwenye bajeti, itaenda kuhakikisha kwamba inapunguza kwa ukubwa sana changamoto ya majisafi na salama katika Jimbo la Uvinza. Ahsante sana.
Name
Ramadhani Hamza Singano
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bumbuli
Primary Question
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:- Je, lini Mradi wa Maji wa Miji 28 ya Rorya – Tarime utakamilika?
Supplementary Question 3
MHE. RAMADHANI H. SINGANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali langu ni kwamba, Mji wa Soni, Bumbuli, ni miongoni mwa miji yenye changamoto kubwa ya huduma ya maji, lakini kuna chanzo kikubwa cha uhakika cha Mto Mkuzu. Ni lini Serikali itaona umuhimu wa kumaliza changamoto hii kwa kutumia chanzo hiki cha uhakika?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Singano kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya, lakini pia kwa kuendelea kutushauri yeye akiwa mdau wa Wizara ya Maji. Akiwa mtumishi wa Wizara ya Maji ameendelea kutupatia ushirikiano mzuri sana hasa kutatua changamoto katika jimbo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe hofu katika eneo hili ambalo Mheshimiwa Mbunge ameligusia, tunayo mipango ya kuhakikisha kwamba tunaenda kutatua changamoto hiyo, lakini suala la lini, tutaenda kuingiza kwenye mpango wa bajeti ya mwaka 2026/2027 ili tuone namna ya kwenda kutatua tatizo hilo. Ahsante sana.
Name
Esther Nicholas Matiko
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tarime Mjini
Primary Question
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:- Je, lini Mradi wa Maji wa Miji 28 ya Rorya – Tarime utakamilika?
Supplementary Question 4
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Tarime una mahitaji wa lita za ujazo wa maji 4,830 lakini yaliyopo sasa hivi ni 2,175 tu, sawa na 45%. Hivyo, tulikuwa tunategemea kuna mradi wa muda mrefu wa Ziwa Victoria. Muda mfupi tuliomba, mwaka huu wa fedha milioni shilingi 140 ili kuweza kuongeza mtandao wa maji kwa Mtaa ya Saba Saba, Majengo na Ronsoti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wa kati tuliomba shilingi milioni 617 ili kuweza kuweka chujio kwenye chanzo cha Nyandurumo ambako mvua ikinyesha wale wanaopata maji, 45% maji ni machafu sana lakini mpaka sasa hivi wametuletea milioni 278 tu. Ile shilingi milioni 140 ya muda mfupi hawajaileta kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninauliza ni lini fedha hizi zitaenda, ili sasa huu mradi wa muda mfupi na muda wa kati uweze kukamilika, watu wa Mji wa Tarime wapate maji wakisubiria mradi huu wa Ziwa Victoria? (Makofi)
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Mheshimiwa Mbunge ni suala la kisera la kuhakikisha kwamba wananchi wanapata majisafi na salama. Ili wapate majisafi na salama ni lazima tuwe na mtambo wa kuchuja ili kuhakikisha kwamba maji yanatibiwa na kuwafikia wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba tunayo miradi mingi inayoendelea kutekelezwa. Tutahakikisha tunapeleka fedha awamu kwa awamu kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amekiri kwamba mpaka sasa Serikali imeshapeleka shilingi milioni 200 na kitu. Nimtoe hofu, kwa dhamira ya Serikali hii ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunafahamu kwamba wananchi wote na Wabunge wote wanayo mahitaji yao ya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kuweka vipaumbele katika miradi ambayo inaenda kugusa matokeo ya moja kwa moja ili iweze kutoa matokeo na kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma ya majisafi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba upatikanaji wa maji haya hasa kipindi cha masika turbidity inakuwa kubwa sana na hilo tunalitambua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo msingi huo huo tulioutumia kuhakikisha kwamba angalau tunapeleka fedha kwanza za kuanza mradi huo ili ukiwa unaendelea, na mkandarasi akiwa anatoa hati za madai, na sisi tutaendelea kulipa bila kuwa na changamoto yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuwa na imani na subira, wakati tunalifanyia kazi, na litakapokamilika wananchi wake watakuwa na furaha ya kutumia majisafi na salama. Ahsante sana. (Makofi)