Mkutano wa Tatu - Kikao cha Thelathini na Sita - Tarehe 25 Mei, 2026
MHE. LUCY D. S. KOMBANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Mchango wangu utajikita kwenye ustawi na mslahi ya watumishi, nikianza na watumishi wa ajira mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza sana Wizara kwa kasi wanayoenda nayo kwenye kuajiri. Ni kasi nzuri na hata ukiangalia kwenye mitandao ya kijamii feedback ni nzuri, watu wameridhika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea na mchango wangu ni kwamba, hili zoezi la kuajiri ni zoezi ambalo linaanza kwa hatua mbalimbali kwamba, tunaangalia sehemu ambayo ina uhitaji wa watumishi, tunatangaza hizi kazi, wanafanya interview na wanaenda kwenye vituo vyao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kumetokea sintofahamu moja kwamba, mtumishi anaenda kituo chake cha kazi, hela za kujikimu hana na kuna wengine wanalalamika mishahara inachelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara iangalie tatizo ni nini? Kwa sababu, mchakato wa kuajiri ni mrefu na unachukua miezi mingi kwa nini linapofika suala la watu kupata hizo hela iwe tatizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote hizi ajira, hasa za utumishi wa umma, kitu cha kwanza ni kutengeneza mindset yake. Sasa anafika eneo, kwa mfano kijijini kama kwetu Malinyi kule au Ulanga, hela ya kujikimu hana na majibu anayopewa atafute namna ya ku-survive. Jamani mtumishi huyu anakuja na nia nzuri ya kutenda kazi, kufanya kazi, kuhudumia jamii, lakini kwa kitendo tunachomtendea sisi waajiri mwisho wake anakuja kukengeuka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ninalotaka kuchangia ni kuhusu mashauri ya rufaa yanayoenda Wizarani. Ninapongeza Wizara, inafanya kazi nzuri, hasa pale inapochakata na kushughulikia mashauri ya rufaa hadi mtumishi ambaye anonekana ameonewa anapata haki yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ndiyo utu ambao Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anausema, lakini ikizungumzwa kwa upande mwingine, bado kuna malalamiko kwamba, kuna madai yanachukua muda mrefu sana. Tukumbuke, jamani Wizara, dai linapokuja huku mtumishi anakuwa tayari ameshapewa adhabu, aidha kapunguziwa mshahara au kashushwa cheo na wengine wanakuwa nje ya ofisi. Hii hali ina-frustrate sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunapozidi kuchelewesha haya madai, hizi rufaa, kwa kweli inakuwa si kitu kizuri. Ninaiomba Wizara sasa iangalie namna ya kukaa vikao ku-fast track hizi rufaa na haki zipatikane kwa watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia upande mwingine ni, kumekuwa na observation hizi rufaa zikifika utumishi kuna issue nyingine inaonekana mtumishi ameonewa, kwamba, wakati anahukumiwa huku chini Sheria za Utumishi wa Umma hazikuzingatiwa. Likifika huko, linarudishwa mtumishi ameshinda ile rufaa arudishwe kazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba Wizara iangalie, sometimes utumishi wa umma kuna watu tu na agenda zao binafsi wanawaumiza hawa watumishi. Tujiulize, je, ni watumishi wangapi hawajui utaratibu wa rufaa? Hawajaja kukata rufaa na wamefukuzwa kazi wapo nyumbani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Wizara iangalie na endapo kama ikithibitishwa, hizi rufaa, mtu amemhukumu mtu ndivyo sivyo, basi na huyo aliyehukumu achukuliwe hatua kutokana na miongozo ya utumishi wa umma. Uzuri utumishi wa umma tunaongozwa na miongozo, sheria pamoja na sera, siyo mtu tu ana maamuzi yake kichwani, anakuja anafanya vitu anavyojua mwenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu ninalotaka kuzungumzia, nitalitoa kwenye Sera ya Menejimenti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Toleo Na. 2 la Mwaka 2008. Nitajikita kwenye aya ya 4.11 na nitanukuu tamko namba nne na tamko namba tano. Tamko Na.4 linasema: “Waajiri wataweka utaratibu utakaowarahisishia watumishi wao kuwahi kazini na kurudi kazini.” Tamko Na.5 linasema: “Waajiri wawawezeshe watumishi kupata unafuu wa kupata makazi.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia Mkoa wangu wa Morogoro; ninashukuru Waziri ana-fast track hili suala la kujenga nyumba za watumishi, lakini niaomba watukumbuke Morogoro. Morogoro ni mkoa mkubwa sana na jiografia yake kwa kweli, kwa mgeni, inaweza ikamtia sonona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna wilaya zetu za mbali, Ulanga, Malinyi, kuna Wilaya kama Mvomero; mtumishi unaajiriwa unaenda kule haujui pa kukaa. Kwa kweli, utumishi wa mtu huyu unaanza vibaya kwa hiyo, tunaomba katika nyumba hizo, Mheshimiwa Waziri, atukumbuke Mkoa wa Morogoro, hasa kwenye majimbo haya ya mbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia taasisi zetu zina mipango ya motisha na mikataba ya hali bora. Hii mikataba ya hali bora imeleta sintofahamu mbalimbali kwamba, tasisi moja inapatiwa kitu fulani, taasisi nyingine haipatiwi kitu fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameongea hapa ndugu yangu, Mheshimiwa Nchimbi, amesema kuna tendency ya watu kukimbia taasisi moja kwenda nyingine kwa sababu ya maslahi, lakini chimbuko la hiki kitu linaanzia kwenye mikataba ya hali bora. Kwa hiyo, Wizara iangalie kwenye upitishaji wa mikataba ya hali bora kusiwe na double standard, kama taasisi inapatiwa kitu hiki na taasisi nyingine ipatiwe kitu hicho hicho, ili tupunguze hii ya watu kutaka kuhamia kwenye taasisi moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia ninapenda kuunga mkono hoja na ninashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. LUCY S. D. KOMBANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kuchangia. Kwanza ninawapongeza sana Wizara kwa harakati wanazoendelea kufanya kuhakikisha kwamba elimu ya Tanzania inazidi kukua siku hadi siku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ninapenda kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kufadhili walimu 150 kwenda India ili wakajifunze mafunzo ya ufundi stadi. Hili ni jambo kubwa sana kwa sababu tunajua kama tunataka kuendelea kwenye mambo haya ya sayansi na teknolojia, lazima tujifunze kwa nchi ambazo zimeendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda Waziri atakapotoa majibu yake atwambie uwiano wa kimkoa. Hawa watu 150 mikoa mingine imeshirikishwaje, kama yote imeshirikishwa ni walimu wangapi walioenda hususan Mkoa wangu wa Morogoro? Kwamba, kati ya walimu 150, hawa ni wangapi wamekwenda kupata haya mafunzo India? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuongezea kwenye hili, tunaelewa kwamba sayansi, teknolojia tunajifunza kwa nchi ambazo zimeendelea, ninamwomba Waziri ashirikiane na Mabalozi wa Tanzania wa nchi mbalimbali kutafuta exchange programmes. Tunajua programu hizi zinawawezesha walimu na wanafunzi waende nje ya nchi kujifunza vitu mbalimbali na mara nyingi hizi programu wanagharamia zile shule husika za nje ya nchi. Kwa hiyo, ili kupeleka hili zoezi kwa uharaka na kuokoa gharama, basi wasaidie kufanya hivyo. Pia, hili zoezi la exchange programme mara nyingi huwa motisha kwa walimu na wanafunzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nililokuwa ninataka kuchangia ni suala la msawazo wa walimu. Walimu wengi sasa hivi wako mijini wanakimbilia mjini. Hali za vijijini siyo nzuri kabisa, utakuta kuna mwalimu mmoja na mwalimu huyu labda kasomea Kiswahili na English, lakini kutokana na uhaba, huyu mwalimu analazimika afundishe hisabati au sayansi, hiki kitu siyo kizuri kwa ustawi wa mwanafunzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kinaleta stress kwa mwanafunzi kinaleta stress kwa Mwalimu, Mwalimu ili afiche ile weakness yake sasa ana-develop ego defence mechanism. Utakuta likifika somo la hesabu anaingia na fimbo nyingi mno, kwa hiyo, yule mtoto akiona zile fimbo hata kuelewa kwenyewe inakuwa ngumu. Tuangalie huu msawazo wa walimu, walimu wapelekwe vijijini ili kila mwalimu afundishe somo alilolisomea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sula lingine ninalotaka kuongelea ni ustawi katika elimu kwa mtoto wa kijijini. Tunahimiza udahili wazazi wanaandikisha watoto, lakini kwa hali ilivyo kwa kijijini kwa kweli inakatisha tamaa. Utakuta mtoto kaanzishwa darasa la kwanza, inaanza kwanza mzazi hana hata uwezo wa kumnunulia viatu, lakini huyu mtoto utakuta anatembea umbali mrefu kwenda shuleni, akifika shuleni anakaa chini, hajamaliza kukaa chini anashinda na njaa siku nzima. Tujiulize je, huyu mtoto ndiyo mtu mzima ambaye atafikia vizuri hii dira tunayoiongelea ya 2050? Wizara iangalie namna ya kumrahisishia maisha huyu mtoto wa kijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo ninataka kumaliza nalo na kushauri Wizara, Profesa ninatamani sana, katika mitaala yetu ifike mahali mitaala iendane na mazingira ya shughuli za kiuchumi za jamii husika. Ninatokea Ulanga, kule tunayo madini mbalimbali tunachimba, lakini leo hii ukichukua rubi ukanichanganyia na chupa ninashindwa kutofautisha na Ulanga ni kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatamani sana, kwa mfano sisi Ulanga tunachimba madini, basi mtoto kuanzia elimu ya msingi afundishwe vile vitu vya pale. Ninatamani sana mkulima wa mpunga Malinyi, huyu mtoto aanze kufundishwa kuanzia umri mdogo. Mimi siyoni haja ya kuendelea kulisoma sikio na sehemu zake zote za ndani ambalo hadi leo hii halijawahi kunisaidia, hicho kitu basi tungejifunza kwenye kutambua labda mbegu ya mpunga imekaaje na inafanyaje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sehemu za wafugaji hivyo hivo, watoto wajifunze kuanzia wadogo, kwamba ufugaji unakuwaje, ng’ombe huyu anatoa vitu gani, anatoa nyama. Ng’ombe huyu hatakiwi kuchapwa sana ngozi itaharibika na hizi ngozi tunatumia kwenye kutengeneza mabegi. Huyu mtoto afundishwe kwamba ng’ombe huyu hatakiwi kwenda kumlisha kwenye shamba la mtu mtatafuta ugomvi. Hivi vitu vingetusaidia sana zaidi ya kusoma vitu ambavyo ni vya sehemu ambazo hazituhusu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ifikie mahali tusiwe na wananchi ambao vichwani tumelishwa vitu vya kigeni, halafu wale wageni wanatoka kule wanakuja kutumia rasilimali zetu ili kuendelea kimaisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufikia hapo, ninaomba niunge mkono hoja. (Makofi)