MHE. IBRAHIM M. SHAYO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha au kujenga nyumba za kisasa za TBA Manispaa ya Moshi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI K.n.y. WAZIRI WA UJENZI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ibrahim Mohamed Shayo, Mbunge wa Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeandaa na kuanza utekelezaji wa mpango wa matengenezo wa nyumba wa miaka 10 kuanzia mwaka 2023/2024 hadi 2032/2033. Mpango huu una lengo la kufanya maboresho makubwa katika nyumba za Serikali pamoja na miundombinu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huu, Wakala umepanga kukarabati nyumba 3,340 kwa gharama ya shilingi 157,232,159,418.71, ambapo Mkoa wa Kilimanjaro umetengewa jumla ya shilingi 6,265,601,062.92. Kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kiasi cha shilingi 556,891,416.08 kitatumika kwa ajili ya ukarabati wa nyumba za majengo ya wakala mkoani humo.