Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Isack Joseph Copriano (2 total)

MHE. ISACK J. COPRIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina swali dogo la nyongeza. Unajua fika Wilaya ya Monduli kwa sasa ni kame na ukizingatia mabwawa yote yamekwisha maji na wananchi wa Monduli wanapata maji Arusha. Je, Waziri haoni sasa ni wakati muafaka wa Serikali kuiangalia Monduli kwa jicho la huruma ili wananchi wale wapate huduma ya maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Isack Joseph.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Kaka yangu, nilifanya ziara katika Jimbo la Monduli mwaka jana na mwaka juzi akiwa Diwani na tuliweza kutembelea miradi mingi ikiwemo na bwawa lililokuwa linajengwa na tukachukua hatua kwa wakandarasi ambao walikuwa wanaleta uzembe katika utekelezaji wa miradi ndani ya Monduli.

Mheshimiwa Naibu Spika, upatikanaji pia wa huduma ya maji katika Wilaya ya Monduli na Jimbo la Monduli ni 77% mpaka sasa ambapo miradi zaidi ya mitano imekamilika yenye gharama ya shilingi bilioni 3.4 na kuna miradi mingine inayoendelea takribani miradi 10 yenye gharama ya shilingi bilioni 41 ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alituelekeza Wizara ya Maji kuhakikisha kwamba tunazipeleka Monduli.

Mheshimiwa Naibu Spika, huu mradi ambao unaendelea sasa ambao umefikia 15% wenye gharama ya shilingi bilioni 20.3. Kwa hiyo, tunaamini kabisa katika uwekezaji huu ndani ya Jimbo la Monduli miradi hii itakapokamilika, ongezeko la upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa Monduli hautakuwa na changamoto yoyote. Ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ISACK J. COPRIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Nataka kujua Mradi wa kutoka Monduli Mjini – Monduli Juu - Maerete hadi kwa Hayati Edward Moringe Sokoine, mradi ambao unafanywa kwa force account. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha ili mradi huo uendelee ambao umekwama pale msituni?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Isack Copriano, Mbunge kutoka Monduli, kama ifuatavyo. Namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji mzuri na ule mradi wako kutoka Ngaramtoni kuelekea Monduli wa vijiji 13 tunaendelea vizuri na mabomba yapo vizuri kabisa yanaendelea kuzalishwa, lakini nakutoa hofu, huu mradi ambao unatekelezwa kwa force account, huu hauna tatizo lolote, tunauweza kwa sababu unatekelezwa na wataalamu wetu wa ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimtoe hofu, Katibu Mkuu atapeleka fedha na wataalamu wetu ambao ni mainjinia mahiri kabisa kutoka Wizara ya Maji wataukamilisha huu mradi bila kuwa na changamoto yoyote. Ahsante sana. (Makofi)