Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Fatma Ally Rembo (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. FATMA A. REMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango Wangu. Awali ya yote, kwanza ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunipa afya njema, siku ya leo kwa mara ya kwanza kuchangia hoja, lakini pia, kuchangia Bajeti ya Wizara ya Elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda pia, kutoa pongezi kwa dhati ya moyo wangu kwa Jemedari wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi ya mageuzi makubwa anayofanya katika sekta ya elimu ya nchini. Pia, ninapenda kuwapongeza Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara ya Elimu nchini kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya kuendelea kuchagiza maendeleo ya elimu katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kwa kusema, elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa lolote duniani na sote tunafahamu hilo. Taifa lenye elimu bora hujenga uchumi imara, teknolojia, ajira na pia, ustawi wa wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kitabu cha Quran kinaanza kwa amri ya kusoma, Surah Al Ala, Aya ya 96, mstari wa kwanza. Unasema: “soma kwa jina la Mola wako mlezi aliye kuumba”, lakini pia, kwenye Biblia, Hosea 4:6 inasema: “watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa”. Tunaona kabisa hii inaonesha wazi kuwa, elimu ni msingi wa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujikita sasa moja kwa moja kwenye mchango wangu. Ninajikita zaidi kwenye mafunzo ya ufundi stadi na pia, elimu ya ufundi stadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuipongeza Serikali kwa kuongeza Vyuo vya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kutoka 1,414 mpaka 1,446 mwaka 2026. Pia, ninapenda kusema na kuongezea uzito kuwa, VETA imekuwa ni daraja kubwa sana la kuwavusha vijana na wanawake. Wanawake wengi wameweza kujiajiri kupitia VETA, wengi wamekuwa wakifungua biashara ambazo wamejiajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano ni karakana, kuna gereji, kuna wanaofungua saloon, kuna wengine ambao wanafungua catering, lakini wapo ambao wanafungua kampuni ndogo za TEHAMA. Tunashuhudia vijana wenzetu wakipambana katika kuchangia maendeleo ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shughuli mbalimbali za uzalishaji mali kupitia elimu ya ufundi stadi, kwa hakika tunaona VETA ni sehemu ambayo ni uwekezaji mkubwa wa moja kwa moja kumsadia kijana au mwanamke kuweza kujiajiri na kuchagia uchumi wa nchi hii, lakini bado tuna changamoto ambayo inatukabili ukiachana na haya maendeleo ambayo tunayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wetu wa elimu nchini umejikita katika nadharia kuliko vitendo; dunia ya sasa inahitaji watu wenye ujuzi mbalimbali na ubunifu. Zaidi ya kuwa na vyeti pekee ni lazima mtu awe na ujuzi na kwanza kujua kutumia teknolojia kwenye kuchagiza na kutatua changamoto za jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kutoa mfano, zipo nchi ambazo zimeendelea kiuchumi, kama Ujerumani, China, Singapore, South Korea; hizi nchi zimewekeza sana kwenye ufundi stadi, lakini pia, kwenye teknolojia na ubunifu pamoja na practical skills kwa wananchi wake, vijana na wanawake. Ninaomba kuishauri Serikali yangu kwa unyenyekevu mkubwa waweze kufanya maboresho yafuatayo, kwa ajili ya mustakabali wa maendeleo ya elimu katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, waendelee kubadilisha mfumo wa elimu kutoka kwenye nadharia kwenda kwenye vitendo, ili kuweza kusaidia wahitimu wetu wawe na uwezo na ujuzi. Wakitoka katika mafunzo waweze kwenda moja kwa moja kujiajiri au kuwa na utayari wa kuajirika kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuimarisha elimu ya sayansi, TEHAMA, coding, kwa maana ya programming na pia, ubunifu kuanzia elimu ya msingi. Yaani coding, TEHAMA na programming zianzie kwenye ngazi ya msingi na siyo tu kwenye vyuo vikuu, ili watu waweze kujifunza mapema nyanja hizi za teknolojia na tukizingatia sasa hivi tunaishi kwenye uwanda mkubwa wa teknolojia, ndiyo maisha ya sasa na ndiyo maisha ya baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, kuimarisha ushirikiano kati ya vyuo vya ufundi na viwanda, ili wahitimu watoke wakiwa tayari kwenye soko la ajira. Kwa maana ya kwamba, vyuo vya ufundi viweze ku-intergrate na viwanda, ili wahitimu wetu wawe tayari wamejiandaa wakiwa kwenye masomo, wakitoka wawe tayari kwenda kuajirika, lakini pia, kuajiri na wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda piakusisitiza vyuo vikuu na taasisi za utafiti zipewe fedha za kutosha, kwa ajili ya innovation. Zipewe fedha kwa ajili ya medicine, zipewe fedha kwa ajili ya scientific research, zipewe fedha kwa ajili ya agriculture technology na renewable energy. Vyuo hivi vina uhaba wa fedha za kufanya haya, kwa ajili ya kuleta maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na teknolojia na maarifa tunahitaji elimu inayojenga maadili. Tunaona Taifa letu sasa ambavyo limekuwa na mmong’onyoko mkubwa wa maadili. Vijana wengi wamekuwa wakifanya mambo mengi ya hovyo na wengine ni wanafunzi kwa hiyo, tunakumbushwa kwamba, tunatakiwa tuanze kuwapa elimu wakiwa huko huko shuleni, elimu ya maadili, uzalendo wa nchi yao, nidhamu, lakini pia, uwajibikaji na utu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi nilivyosema sasa ndiyo msingi wa maendeleo yote tunayoyatafuta kwa sababu, elimu bora siyo vyeti peke yake, bali kujenga Taifa lenye wananchi wenye maadili na maono katika nchi yao. Ninapenda kusema Tanzania ina vijana wengi sana wenye ujuzi mkubwa, lakini lazima tuendelee kuboresha mfumo wetu wa elimu, ili kuwekeza zaidi katika sayansi, teknolojia, ubunifu na ujuzi wa vitendo, ili Taifa letu liweze kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi mkubwa na pia, ushindani wa Kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ninapenda kwanza kunukuu quote ya Nelson Mandela. Alisema, “Education is the most powerful weapon which, you can use to change the World”, akimaanisha, elimu ni silaha yenye nguvu zaidi unayoweza kuitumia kubadilisha dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa quote hii tunaona ni namna gani elimu ndiyo msingi mkuu wa maendeleo katika nchi na Taifa lolote katika dunia hii. Namalizia kwa kusema, napenda pia kutoa pongezi tena na tena kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ndugu zangu tumeona ni namna gani ambavyo ameleta mageuzi makubwa, wananchi tuendelee kumpa moyo, lakini sisi kama Wabunge, tuendelee kumwombea Mheshimiwa Rais, ili aweze kuendelea kufanya mambo makubwa na mageuzi katika Taasisi hii ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba kusema ninaunga mkono hoja na ninashukuru sana. (Makofi)