Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Fatma Ally Rembo (1 total)

MHE. FATMA A. REMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapomwezesha mtoto wa kike
tusimsahau pia mtoto wa kiume ambaye pia anakutana na changamoto nyingi za malezi. (Makofi)

Je, Serikali ina mpango gani maalum au mkakati gani
maalum wa kuhakikisha kijana wa kiume anajengwa na kulinda ili aweze kuja kuwa kiongozi bora na baba bora wa kesho? (Makofi)
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na nampongeza sana Mheshimiwa Fatma kwa swali lake la nyongeza zuri ambalo linapenda kujua ushiriki wa watoto wa kiume kwenye masuala haya ya malezi na makuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema kwamba watoto wote ambao wanasimamiwa chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maluum ni wa jinsia zote na katika mikakati yote tunapotamka neno mtoto, mtoto wa kiume anakuwa ni sehemu. Mfano tunatekeleza mkakati wa vikundi vya
malezi vya wazazi, wazazi hawa wanafundishwa jinsi ya kwenda kufanya malezi na makuzi ya watoto, ndani mle wanaume wapo ambao ni baba zao na hawa watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatekeleza elimu kwa jamii
inayohusu masuala yanasema Familia Bora Taifa Imara. Tayari wazazi ambao wameshiriki kwenye hii programu au hii kampeni ni kama 550,000 na nusu hivi lakini kati yao laki moja hamsini na saba na pointi ni wanaume.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunawafikia watoto hawa kupitia wazazi wao wa kike na kiume, lakini tukienda mashuleni tuna madawati ya ulinzi wa watoto, madawati ya ulinzi wa watoto ni watoto wote wa kike na kiume, na kwenye uongozi pale kiongozi ni mwanamke na mwanaume kwa pamoja. Kuna
mabaraza ya watoto tunayafanya. Haya mabaraza ya watoto yanaanzia kijijini, kwenye mitaa, kwenye kata. Haya nayo ni watoto wote wako mle ndani. Tumekuwa na watoto wa kutosha wa kiume wanakwenda kuwakilisha nje ya nchi wakitokea kwenye haya mabaraza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiiangalia sheria ya mtoto
ilivyojengwa, inamshughulikia mtoto wa kike na wa kiume. Kwa hiyo, ninapenda tu kusema kwa ufupi tunazingatia masuala haya na ili kuongeza nguvu zaidi tumesajili vyama vya wanaume mbalimbali na siku hiyo nilipowasilisha bajeti tarehe 01 Juni walikuwepo. Lengo ni kuuchukua mtandao wa wanaume uingie, ushike nafasi yake katika kuangalia maslahi ya wanaume, siyo
wakubwa tu bali na watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hapa Mheshimiwa Baba Levo tunatarajia kumteua awe Balozi wa Wanaume, lengo ni kwamba kupitia uwezo wake wa kuzungumza nao na kushirikiana nao watuletee zile hoja, wapi tuna-miss point katika kusuka mikakati yetu. Hili linakwenda sambamba na Mheshimiwa Kampala pia. Hawa tumewaona wanaweza wakatusaidia sana kwenda vizuri kwenye hii Wizara, ili hili suala mwishowe lipate majibu ya kutosha na ya kina yanayowaridhisha Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)