Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Eng Ezra John Chiwelesa (1 total)

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi pia nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Biharamulo kuna miradi mikubwa ya maji inayoendelea katika Kata ya Nyakahura, Kata ya Rusahunge eneo la Nyakanazi na Kata ya Nyarubungo, ni miradi mikubwa, mingi zaidi ya shilingi bilioni moja. Mradi mmoja wa Nyarubungo ni 1.4, Nyakahura ni 1.4, lakini ule wa Nyakanazi ni 2.9 bilioni, kwa hiyo ni miradi mikubwa ya kimkakati kwa eneo la kwetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumejikuta kwamba ile miradi yote imekwama kwa sababu mtekelezaji wa ile miradi ni mmoja na amejitahidi sana kufanya kazi, lakini ana madai ya muda mrefu Wizarani hali ambayo imemsababisha amekuwa incapacitated kiasi kwamba hawezi tena kuendelea na ile miradi, na miradi imefikia katikati haiwezi kutoa maji kwa sababu ana madai yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninataka nisikie kauli ya Serikali, ni lini mtu huyo atalipwa ili nia njema ya Serikali ya kuwapelekea wananchi wa Biharamulo maji iweze kutimilika kwa vile anakwama kwa sababu ya malipo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra, Mbunge wa Biharamulo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana, kazi kubwa anayoifanya na hata hii miradi asingekuwa anaifuatilia kwa ukaribu isingeweza kuanza na sasa imeanza. Hiyo ni hatua moja kubwa ambayo ninampongeza sana na sisi Wizara ya Maji tutahakikisha kwamba tunampa ushirikiano wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, niendelee kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa kupitisha sheria ambayo imetufanya tuweze kupata fedha za tozo ya mafuta moja kwa moja zaidi ya 70%, ambayo sasa itatufanya tuweze kupangilia mambo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikujulishe kwamba kuanzia mwezi huu tayari tumeanza kupokea fedha na tayari tumeanza ku-disburse kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunalipa madeni katika miradi yote inayoendelea nchini. Tunafahamu kwamba burden ni kubwa, fedha inayokuja haiwezi kutosha kwa pamoja, nimtoe hofu kwamba tunaenda kumuweka kwenye vipaumbele kuhakikisha kwamba miradi yake na mkandarasi wake analipwa kwa wakati ili aende kutekeleza mradi huo na ukamilike kama ambavyo amekusudia Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana.