Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Imamu Mtumwa Vuai (1 total)

MHE. IMAMU MTUMWA VUAI aliuliza:-

Je, upi mpango wa kuimarisha Idara ya Uhamiaji kutumia teknolojia za kisasa za utambuzi na udhibiti wa mipaka ili kuimarisha usalama?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Imamu Mtumwa Vuai, Mbunge wa Magomeni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuboresha huduma ya Uhamiaji kwa teknolojia ya kisasa kwa kuboresha mtandao na kujenga mifumo mipya na kuendelea kuimarisha mifumo iliyopo ambapo maboresho hayo yanajumuisha uanzishaji wa Mfumo wa Advance Passenger Information, Passenger Name Record, uboreshaji wa mfumo wa e-Border Management Control, Immigration Common Gateway Interface, pamoja na maboresho ya miundombinu ya vituo vya kuhifadhi mifumo ya Serikali ili kuongeza usalama, upatikanaji na mwendelezo wa huduma za Uhamiaji Mtandao.

Mheshimiwa Naibu Spika, uimarishaji wa matumizi ya mifumo ya kiteknolojia umerahisisha sana utolewaji wa huduma za kiuhamiaji sambamba na kuimarisha usalama wa nchi hasa katika utambuzi na udhibiti wa mipaka. Katika mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali ilitoa kiasi cha fedha shilingi 69,000,000,000 kwa ajili ya ununuzi na ufungaji wa vifaa vya mifumo ya Uhamiaji Mtandao, kukarabati miundombinu ya majengo ya vituo ili mifumo hiyo iweze kusimikwa, kuongeza uwezo wa vifaa vya kuhifadhi data na kuendesha mifumo katika kituo kikuu cha kuhifadhi mifumo na data zilizozalishwa (National Internet Data Centre) kilichoko Dar es Salaam na kituo cha kujikinga na majanga (Disaster Recovery site) kilichoko Mazizini, Zanzibar.