MHE. IMAMU MTUMWA VUAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi. Ni lini Serikali itakuja na mkakati madhubuti wa kulinda viwanda vya ndani dhidi ya ushindani wa bidhaa za bei nafuu kutoka nje?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nishukuru kwa swali zuri la Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na suala la kulinda viwanda vyetu vya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, tumeendelea kutengeneza sheria, lakini pia tumeendelea kutengeneza kanuni na kuboresha kanuni mbalimbali, lengo ni kulinda bidhaa za ndani, na pia kuchochea uwekezaji na kuendeleza uzalishaji wa bidhaa zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili, tunaweza kuona wiki iliyopita Waziri wa Viwanda na Biashara aliongoza zoezi la kukamata mali ambazo zimezalishwa kinyume na sheria ama zimeingizwa kinyume cha sheria ambazo zimeingizwa sokoni chini ya viwango ama kinyume cha taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kufanya hivi, ni kulinda viwanda vyetu vya ndani, kuongeza imani ya walaji, lakini pia kulinda mitaji ya Watanzania. Tutaendelea kufanya hivyo ili kuwavutia wawekezaji wapya, lakini pia kulinda wawekezaji na wazalishaji wa bidhaa za ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. IMAMU MTUMWA VUAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutumia teknolojia ya kisasa kama CCTV Camera na mifumo ya kidigitali katika kuboresha ulinzi nchini badala ya kutegemea vituo vya Polisi pekee?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninampongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Imamu Vuai, Mbunge wa Magomeni kwa swali lake la msingi na muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba, dunia kwa sasa imekua kwa kiasi kikubwa kwenye eneo la teknolojia. Kutokana na kukua huko, hata Dira yetu ya Maendeleo ya 2050 imeelekeza kwamba tutumie teknolojia katika kukuza uchumi na kuimarisha ufanisi. Hivyo nikubaliane na rai yake inayosema kwamba sasa Jeshi la Polisi au vyombo vya ulinzi na usalama vijielekeze zaidi kwenye teknolojia katika kuimarisha mifumo ya kiulinzi, na huko ndipo ambapo kwa sasa dunia ipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kujielekeza huko kuna faida nyingi, zikiwemo kupunguza idadi ya makosa (crime rates) kwenye maeneo mbalimbali, vilevile kuna kupatikana kwa usahihi wa taarifa za kiusalama au kwa wale wanaotenda makosa na bila ya kumwonea mtu kwa sababu tumetumia teknolojia. Aidha, tunaweza kupunguza matumizi makubwa ya rasilimali watu na kutumia mifumo na vifaa badala ya idadi kubwa ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jambo hili, na kwa kuona umuhimu huu, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeanza mchakato wa kuliangalia upya jambo hili. Kwa bahati nzuri, kwa upande wa Zanzibar jambo hili lilishaanza kwa muda kidogo. Tumeona katika eneo la Mji Mkongwe limeondoa au kupunguza kwa kiasi kikubwa sana crime rate kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeliangalia jambo hili katika maeneo makuu matatu. Kwa kuanzia, kwanza, Serikali inataka kwenda kwenye miji salama (safer city), na itaanza miji mikubwa; pili, tunataka kwenda kwenye barabara salama kuhakikisha kwamba tunapunguza ajali kwa kutumia mifumo; na tatu, katika ukaguzi wa magari kwa maana vehicle inspection, nalo hilo tuko katika mwelekeo wa kuelekea huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.