Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Happiness Daniel Ngwando (3 total)

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. HAPPINESS D. NGWANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote, napenda kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuwa mahali hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama kwenye Bunge lako Tukufu, ninapenda kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuniteua kuwa mwakilishi wa wanawake wa Mkoa wa Ruvuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee sana niwashukuru wanawake wa Mkoa wa Ruvuma kwa kunichagua kwa kura zao ili niweze kuwawakilisha katika Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Mheshimiwa Dkt. Emmanuel Nchimbi, Makamu wa Rais, kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi za kishindo Oktoba 29. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nipo hapa leo niseme mawili matatu ambayo Rais wetu ametufanyia. Kama inavyosemwa mara zote, moyo usio na shukrani hukausha mema. Sisi wanawake wa Mkoa wa Ruvuma, Mheshimiwa Rais ametufanyia mengi sana ndani ya miaka minne iliyopita toka aingie madarakani ametupa zahanati, vituo vya afya, kwenye sekta ya elimu, maji na hapa nitapenda niseme vichache tu ambavyo wajue kwamba Mheshimiwa Rais anafanya kazi sio tukisema tunasema hewani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ametupatia Halmashauri ya Mbinga Vijijini, hospitali ya wanawake yenye thamani ya shilingi bilioni 2.9; zahanati 17 zenye thamani ya shilingi bilioni 1.7; vituo vya afya vitano vyenye thamani ya shilingi bilioni 2.7; vituo vya afya kule Wilaya ya Tunduru; Kituo cha Malumba kinaendelea na kazi, Kituo cha Afya cha Kata ya Mbaa Wilaya ya Nyasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta ya maji ametupatia vitu vingi. Kwa kuwa mimi ni kiungo mchezeshaji namba sita nitataja wilaya zote ambazo amefanya vitu hivi kwa macho. Mheshimiwa Rais alitupa shilingi milioni 900 Hospitali ya Wilaya ya Mbinga ambayo kwa kweli ile hospitali ni kongwe alitupa tufanye ukarabati wa hospitali ile. Tuliweza kufanikisha kutengeneza OPD, emergency nzuri sana ipo pale, tulitengeneza theatre, tukatengeneza na maabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo alitoa fedha hospitali ya Wilaya ya Tunduru, shilingi milioni 900, tulitengeneza OPD nzuri sana, tukatengeneza theatre. Siku zote wanasema ukisema ahsante maana yake unaomba tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mazuri haya, bado niwakumbushe kwenye bajeti ambayo itakuja tunahitaji au tunaomba mtujengee wodi za akinamama (maternity ward) kwa kuwa hospitali hizi ni kongwe na zinapokea wamama wengi sana. Kwa mwezi wanajifungua wanawake takribani 400 - 500 kwa Tunduru, lakini pia wanajifungua akinamama 700 - 1,000 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye suala la maji. Ninamaanisha kwamba tunaposema uzalishaji na mpango wa ukuwaji wa uchumi kwa jamii, tunaangalia zaidi afya ya watu hawa. Jamii ikikosa afya, ikikosa huduma za jamii maana yake uchumi huu hautakua. Ndiyo maana nimempa hongera nyingi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukumbuka kuwa uchumi unaendana na afya ya jamii na mazingira mazuri. Tunasema ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Rais bado anajua unapotakiwa kuwa na uchumi mwanamke anatakiwa asikae bombani au asitafute maji masaa manne hadi matano ameendelea kutupatia maji Wilaya ya Mbinga shilingi bilioni 4.6. Pia amekwenda kutupatia mradi mkubwa wa maji Halmashauri ya Tunduru shilingi bilioni 3.4, tunasema ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hapa sasa ningeomba nijielekeze kwenye ushauri wa mpango na sera wa mwaka 2027/2028. Kwanza ninapenda kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri mwenye dhamana walipotuambia kuhusu suala la wanaopata kazi wasihame kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili ninapenda kuishauri Serikali, niseme kuwa kama Mheshimiwa Waziri Mkuu alivyosema kuwa inatakiwa watu wasihame, tunaomba iwekwe sheria ili kuilinda kauli za viongozi walizosema zitekelezwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano watu wakienda kuripoti kwenye vituo vyao, unakuta kuna wakati wanakuja na barua moja kwa moja wanasema wasainiwe ili wahame. Tunaomba, kuwalinda Wakurugenzi na watu wenye mamlaka husika basi waweke sheria ambayo ita-cement hii kauli ya kuwa watu wasihame ili watu wetu waendelee kupata huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaomba nishauri jambo lingine kwenye suala la elimu. Tunasema hawa watu wanaopelekwa kwenye vijiji mbalimbali, wanaokwenda kufanya kazi, ajira za vijijini, ningependa kushauri tuwape motivation, kwani kijijini kuna mazingira fulani ambayo sisi wote tunayafahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungetamani sana waajiriwa hawa wanaokwenda vijijini wapewe motisha. Kwa mfano, tuna ile Mei Mosi ambayo inasema, mtu Mei Mosi ndiyo anatambulika. Asitambulike Mei Mosi peke yake, kuwe na utaratibu, idara husika kama ni walimu, kama ni afya, waishi kule wakiwa wanajua wanajaliwa na wanapendwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mtu akifanya vizuri, labda tunasema anunuliwe bati, labda atakayefanya vizuri atanunuliwa hiki, itamfanya yule mtu aone kuwa inawezekana kubaki pale. Kama Mheshimiwa Rais alivyoanzisha kuanza kuwatengenezea nyumba zaidi ya 70 kwenye maeneo yao, na sisi kama watendaji na wataalam na Serikali, tuwape motivation hawa watu badala ya kuona tu kuwa wanakosea wapi? Kwa nini wanataka kuhama? Tuwatengenezee mazingira ya wao kupenda kukaa kwenye maeneo yao ya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikifika hapo, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. HAPPINESS D. NGWANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Pia nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunipa afya na uzima kusimama hapa siku ya leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee ninampongeza sana Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuendelea kututumikia Watanzania. Ninapenda pia kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa ziara yake nzuri ambayo ameshaifanya na nimkaribishe sana Mkoa wa Ruvuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nijikite moja kwa moja kwenye kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Nitaenda upande wa elimu, maji na kilimo kama muda utaniruhusu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niungane kwanza na Mheshimiwa Chenge aliyezungumzia kuhusu wanagenzi. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii. Tumekwenda kuona vyuo hivi kwenye mazingira yao. Kuna umuhimu mkubwa sana wa fedha hizi kurudi moja kwa moja kwenye Mfuko wa Ofisi ya Mahusiano, Kazi na Ajira, kwa sababu kwa kumwongezea hapo, hizi fedha zinakusanywa na TRA, lakini wakati zinapokusanywa, zinakwenda kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina, ambapo haziendi kugawiwa moja kwa moja kwenye Mfuko husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama tulivyoona hapa, inakusanywa shilingi bilioni 358. Walitakiwa wapewe shilingi bilioni 119, lakini wanapewa shilingi bilioni tisa au 10, hata robo ya ile fedha haijafikiwa. Sote tunafahamu kuwa vijana wetu ndio wa muhimu, wako wengi na wanahitaji ajira na kelele zimekuwa nyingi. Kumbe kama fedha hizi zingekwenda kwenye Wizara husika, wangeweza kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo nimpongeze Mheshimiwa Deus, amejitahidi sana kufanya kazi. Tumepita huko, anafanya kazi mno na kwa weledi mkubwa, lakini anakwamishwa pale ambapo fedha zinakuwa haziendi. Hivyo, tungeomba TRA zitoke moja kwa moja kwenda kwa wahusika badala ya kubaki na hizi fedha. Agawiwe vile ambavyo wao wanasema. Mara wanasema imekwenda Bodi ya Mikopo, mara imeenda huku. Tujue hicho kipengele fedha imekwama kwa ajili ya vijana wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende eneo la pili kwenye suala la elimu. Tunafahamu kuwa tuna shule zetu za kata. Kwenye hizi shule za kata watoto wa kike wanapata shida. Tunaomba sana kujengwe hata bweni. Wakati tunajiandaa kuelekea kwenye sekondari za vijiji, basi wawekewe mabweni. Angalau tuanze mchakato mdogo mdogo wa kuanzisha mabweni.

Mheshimiwa Naibu Spika, watoto wanapanga nyumba, wanafanya umama kabla ya wakati. Wanakuwa wana majukumu ya kimama, kwa hiyo, tunakuwa hatumwokoi mtoto, siyo tu wa kike, tena bora wa kike. Sasa hivi unakuta na mtoto wa kiume vishawishi ni vingi. Akitoka pale anapotokea alipopanga, mpaka afike shule mambo ni mengi. Boda boda naye anampa lifti na baadaye sasa inabidi alipe nauli kwa njia zisizo salama. At the end tunajikuta mtoto huyu hayuko tena salama na anaharibu ndoto zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee pia suala la chakula shuleni. Sisi sote tunafahamu kuwa ugali ni kazi kwenye baadhi ya familia. Ukisema hapa sasa hivi mtoto apewe gunia la mahindi aende nalo shule, mzazi unachanganyikiwa. Ningeomba sana Serikali, nitoe ushauri kwenye hili, kama kuna uwezekano itengwe bajeti kwa ajili ya chakula cha watoto shuleni. Hata kama hatutaweza leo, wafanye ubunifu wa chochote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu inalima, nchi yetu ina vitu vingi sana ambavyo tunaweza kuchangia chakula watoto hawa wakapata chakula shuleni. Mimi mwenyewe hapa ni mfano hai. Nilipokuwa mdogo, unaweza ukashinda siku nzima hamjala. Tusichukulie poa kwa sababu tayari tumeshiba. Tukumbuke, tutengeneze.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtoto gani ambaye utampeleka shule halafu anashinda na njaa? Kwanza tunatengeneza kizazi cha Taifa la kesho ambalo linaweza likawa na vidonda vya tumbo, badala ya kutufanyia kazi vizuri kwenye Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo niende kwenye Wizara ya Maji. Tuna suala la maji vijijini na mijini, lakini Wizara ya Maji mara nyingi tunapata nayo tabu. Kikubwa ni hiki, unatoka unaanzisha mradi kata fulani, mradi ule haujakwisha, unakwenda kata ya pili; mradi haujakwisha, unakwenda kata ya tatu. Kwa nini, fedha hii iliyoanzisha miradi midogo midogo isimalize mradi mmoja ili kero hii upande huu ikapungua wakati tunaendelea kutembea? Mheshimiwa Rais anajitahidi sana kuleta fedha kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niingie pia kwenye suala hili la miradi. Kwa mfano suala la miradi ambayo tunaipeleka kwenye maeneo yetu, usimamizi unakuwa mdogo. Fedha zinatoka zinakwenda site, lakini tukifika kule, baadhi ya wataalam wetu hawana uzalendo. Kwa mfano, tulipewa Miradi ya COVID 19, kila wilaya ilipewa fedha na tukapelekewa kwenye kata yakajengwa madarasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, madarasa yale Mheshimiwa Rais aliyapeleka nchi nzima, maana tayari ameshatoa fedha na imeshakwenda, lakini ukifika pale kwenye lile eneo la ujenzi unakuta engineer tu anakwamisha. Baada ya hapo, pakiharibika, engineer yule yule wanamtoa tena wanampeleka eneo lingine ili akaharibu tena. Ameharibu Madaba, unampeleka Mbinga. Kiukweli wanatuumiza sana, na wananchi wanateseka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hili nina ushahidi. Nimefika kukagua mradi nikiwa huko nyuma, tunakagua, unakuta mtoto anadeki, cement inatoka na alikuwepo engineer hilo eneo. Ukimwuliza, engineer, kwa nini iko hivi? Wanajibu wanasema; “huyu tumemhamisha kule ndiyo maana tumemleta huku.”

Mheshimiwa Naibu Spika, jamani, ninaiomba sana Serikali, mtu anayeharibu atoke. Kuna wengi wanaomba kazi. Tunawaumiza Watanzania. Fedha inaletwa mara moja. Mheshimiwa Rais ameshatuletea fedha mara moja, hadi tena mzunguko uje, ni leo! Hii fedha ina kazi nyingi. Leo tumejengewa darasa, kesho tena hela hiyo hiyo tujengewe darasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi tumeenda halmashauri moja tumekuta mwalimu wa pale amejenga hilo hilo darasa la bei hiyo hiyo amelimaliza na amejiongeza ameweka na madawati, unafika huku darasa hilo halijakwisha. TAMISEMI tunaomba sana, Watanzania ni wengi kuliko mtu mmoja. Watoto wa kimaskini wa Kitanzania Mheshimiwa Rais amewaletea kitu, mtu mmoja tu anaharibu labda kwa sababu zake binafsi. Ninaomba sana wachukue hatua kama ambavyo Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wengine wanavyokwenda huko. Hakuna kitu kibaya kama mtu mmoja aharibu watu 1,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaenda kwenye suala la kilimo. Hapa niongee na NFRA. Tunaomba sana, sisi Mkoa wa Ruvuma, wanawake na waume na watoto wetu ni wakulima. Tukifika tunaanza kulima. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais ametuletea pembejeo za kutosha, anatupa kwa muda muafaka, tunaenda shambani tunalima, tunaleta mazao yetu, haijatulipa toka mwaka jana mwezi Agosti mpaka leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huo mtoto mdogo mwenye miaka 10 kule Wilaya ya Mbinga ana shamba lake la hekari mbili, mama yake akamwambia lete tupeleke NFRA Serikali yetu inanunua vizuri. Anafika kule hajalipwa, mtoto huyu daftari za mwaka huu maana yake hawezi kupata kwa sababu pesa iko NFRA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana kama kuna uwezekano uwekwe utaratibu mzuri haya mazao yanunuliwe kwa wakati lakini wakati huo huo yalipwe kwa wakati. Tunateseka, tunashindwa kupata huduma zinazostahili. Ustawi wa jamii ni pamoja na mtu kunawiri na kupendeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pesa ndiyo kila kitu, nimelima nimepeleka mazao yangu, haya mengine mwananchi hataki kujua anachojua ameshapeleka mazao NFRA anataka kuona sasampa. Kikubwa ni pesa, watu hawa hawatuelewi tunavyokuja kule kama wawakilishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu jambo moja, ninakushukuru sana. Kikubwa ninaunga mkono hoja na ninashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. HAPPINESS D. NGWANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Nami nimshukuru Mungu kwa afya aliyonijalia jioni ya leo. Nimshukuru sana pia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutupambania wanawake katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitakuwa na mambo machache tu kuhusu sheria, nimesimama hapa kwa ajili ya wanawake wa Mkoa wa Ruvuma kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022, ni wanawake 953,000 ambao wako huko na wanatamani kuona nini juu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku ya leo nitakuwa kwenye mambo mawili au matatu. Awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria, kwa kazi nzuri anayoifanya hasa ile ya kusema na Waziri moja kwa moja, tunashukuru sana wakati akiwa anatatua kero. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana pia Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria na kumpongeza kwa kazi anayofanya hasa ile kazi ya Mama Samia Legal Aids ambayo inatufikia hata kwenye mkoa wetu na watu wetu wanawake wanaendelea kupata haki zao, wanaendelea kusikilizwa kero mbalimbali katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina sehemu mbili au tatu. Niko kwenye suala la sheria ya mwanamke au binti upande wa ndoa. Sehemu ya kwanza ni ile ambayo inamtaka mtoto wa kike mwenye miaka 14, ndiyo yeye anatakiwa kuolewa kwa mujibu wa mzazi, lakini mtoto wa kiume wa miaka 18 yeye ndiye atakuwa akifikisha miaka 18.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyoona sasa hivi elimu msingi inaanzia awali mpaka kidato cha nne, mtoto huyu mwenye miaka 14 sheria hii ikiendelea kubaki ikikaa silence haieleweki vizuri, mtoto huyu hatapata haki ya kusoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, mtoto mwenye miaka 14 bado katika uhalisia kwetu ni mtoto mdogo sana. Hapa nawaona wanangu wa darasa la saba sasa hivi wanapata mimba huko nyumbani leba akiingia mama unaanza kuchanganyikiwa nje. Si sahihi na tunaomba sana sheria hii isiwe na kigugumizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto hawa wenye miaka 14 tunaomba waingizwe kwenye miaka 18 kama watoto wa kiume kwa kuwa hata Katiba yetu inakataza ubaguzi kati ya mtoto wa kike na mtoto wa kiume. Sheria hii isiwe na kigugumizi tunaomba sana kama mwakilishi wa wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Sheria za Ndoa yanasemwa mengi na wenye sheria zetu huko na wataalam walioziandika sheria hizi. Kiuhalisia sheria hizi zimepitwa na wakati ukilinganisha na mfumo wa mwanamke sasa hivi ulivyo. Mwanamke sasa hivi ndiyo mchumi kwenye nyumba zetu na familia zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru wametuelimisha sana na somo limeeleweka, wanawake sasa hivi nyumbani wanamiliki pesa, wanamiliki kila kitu ambacho mwanaume anaweza kumiliki. Sheria bado inamtaka mwanamke, huyu hata hasa pale kwenye mirathi unakuta anaambiwa mwanaume akifariki yeye anapata moja ya tatu anagawiwa kidogo, lakini haitoshi mama huyu huyu akitokea anafariki, katika baadhi ya sehemu, anatolewa kwenye nyumba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapata meseji nyingi kama wawakilishi na hapa simwongelei mwanamke msomi, mwanamke mwenye lace wig. Mwanamke ninayemwongelea ni mwanamke wa kijijini, Mkoa wa Ruvuma kule ambaye haijui sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba uelewa kwenye hili; sheria inasemaje mwanamke huyu anapofiwa, kwa nini nyumba yake anayoishi na mume wake wa ujana iwe ndani ya mirathi? Kwa nini nimekaa na mume wangu ujana wote leo unaniambia ninatakiwa nitoke kwa sababu amefariki ile nyumba igawiwe?


Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi baba alienda sehemu kwa starehe zake akifika huko kule kuna watoto, sheria inasema mtoto si haramu baba ndiyo haramu, itabidi arudi huku kwa bibi mkubwa akachukue mali ambazo alichuma mama huyu na mume wake. Mume aliyemvumilia miaka 40 mpaka 50, anarudi saa nane usiku, kichwa cha nyumba kinarudi kimeyumba, mama amevumilia, ameishi vizuri, ametunza watoto, analima, anaenda kulima mikorosho yake, amechangia nyumbani vitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo anaambiwa yeye moja ya tatu tu, lakini watoto wote wenye jina la baba watapata mali hiyo. Hata hivyo, mali ya kule inaelezwa ni zawadi hadi ithibitike. Kwa nini mali ya baba huyu haijathibitika kule lakini watoto wamethibitishwa? Ni kitu gani kimethibitisha kuwa wale ni watoto wake ili hali hawakuthibitisha kama zile mali pia ni za mume wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kama ni hivyo sheria iseme mali ya huku na kule zirudi sehemu moja tugawane pamoja. Siyo shida; ila tugawane zote na tusiwe na kigugumizi kusema eti imekuwaje kwa sababu ile ina majina yake hakuna aliyeona hapana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtueleweshe hatuelewi tunagombana, tunapigana wanawake tunakuwa psychiatric tunatembea tunaongea peke yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta mama unamsalimia mama shikamoo anakwambia ona nimeachika talaka hii hapa, ameshapoteza akili. Mwanamke ni upendo kwenye jamii, leo Sheria ya Ndoa hii hii wanasema tumebadilisha na maneno yao, sheria ipo wazi, wanasema sheria iko wazi, wazi wapi? Mbona watu wetu hawaijui? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba uelewa iende huko kwenye vijiji. Wanasema sasa hivi kila mtu akiwa mwanaume na mwanamke wanachangiana wanaleta kitu pamoja; wewe unaonyesha ulichofanya na ulichochuma na mwenzako anaonyesha alichochuma, lakini unatakiwa uwe na ushahidi hata miamala.


Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mahusiano kuna wakati wa kuangalia na kutunza miamala? Muda huo mpo lele; miamala hii unaitunzaje? Tumefikia sehemu tunavyojenga nyumba nyumbani, kwanza mila za kiafrika mwanamke huwa ham-demote mwanaume, unacheza kikoba, unajinunulia mwenyewe marumaru unaweka kwenye nyumba.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa
muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante.

MHE. HAPPINESS D. NGWANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, unapoweka unamwambia fundi weka vizuri mume wangu amenituma. Kwa hiyo, tunaomba sheria hii imepinda...

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda.

MHE. HAPPINESS D. NGWANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika moja na wind up moja tu…

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. HAPPINESS D. NGWANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nyumba ya mrithi isiwekwe kwenye mirathi. (Makofi)