MHE. HAPPINESS D. NGWANDO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kutengeneza barabara za usalama mipakani ili kuwezesha vyombo vya ulinzi na usalama kufanya doria?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Happiness Daniel Ngwando, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara za usalama mipakani ni barabara zinazoambaa na mipaka ya nchi yetu kwa ajili ya kuwezesha vyombo vya usalama kuimarisha ulinzi na usalama mipakani. Kwa kutambua umuhimu wa barabara hizi, Serikali inaendelea kuzijenga kwa kiwango cha changarawe ili ziweze kutumika na vyombo vya usalama kufanya doria mipakani.
Mheshimiwa Spika, hadi sasa Serikali kupitia TANROADS imejenga jumla ya kilometa 1,759 kwa kiwango cha changarawe katika Mikoa ya mipakani. Aidha, Serikali inaendelea kujenga sehemu zilizobaki kwa awamu kwa kiwango cha changarawe kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. HAPPINESS D. NGWANDO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kurekebisha Sheria ya Ndoa pale wanandoa wanapotalikiana ili kumaliza kesi zao haraka?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha Tisa cha Sheria ya Ndoa, Sura 29 kinatafsiri ndoa kuwa ni muunganiko wa mwanamke na mwanume kwa lengo la kuishi pamoja maisha yao yote. Kwa msingi huo, Sheria ya Ndoa imeweka utaratibu wa kuanza kusikilizwa kwa mashauri ya ndoa katika Bodi za Usuluhishi wa Ndoa kabla ya kufikishwa Mahakamani kwa ajili ya maombi ya talaka, lengo likiwa kutafuta suluhu zaidi kuliko kuachana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika juhudi za kuhakikisha usikilizaji na umalizaji wa mashauri, Mahakama ya Tanzania imetoa Mwongozo wa muda wa usikilizaji kesi kulingana na Mahakama ilipofunguliwa. Kwa mujibu wa Mwongozo huo, kesi zinazosikilizwa na Mahakama ya Mwanzo, ukomo wake ni miezi sita; Mahakama ya Wilaya na Hakimu Mkazi ukomo wake ni mwaka mmoja; na Mahakama Kuu ukomo wake ni miaka miwili. Aidha, Mashauri ya Talaka, kwa mujibu wa taratibu yanaweza kusikilizwa na kuamuliwa na Mahakama za Mwanzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuimarisha taasisi ya ndoa na kuhakikisha migogoro ya ndoa inatatuliwa kwa njia ya usuluhishi, Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeanzisha programu ya kuwajengea uwezo Wajumbe wa Bodi za Usuluhishi wa Ndoa Nchini kote. Utekelezaji wa Programu hiyo ulianza rasmi tarehe 8 Aprili, 2026 katika Mkoa wa Kagera. Lengo ni kuhakikisha wanandoa wenye migogoro wanapata suluhu stahiki kabla ya kuwasilisha mashauri yao Mahakamani kwa ajili ya maombi ya talaka.