Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Happiness Daniel Ngwando (4 total)

MHE. HAPPINESS D. NGWANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kuuliza swali la nyongeza. Serikali ina mpango gani wa kuweka network kwenye hospitali zetu ambazo zinatumia system, ili kupunguza mgonjwa kukaa muda mrefu kumsubiria daktari apate network. Kwa mfano, Hospitali ya Wilaya ya Nyasa na Nangombo, Tunduru, ili daktari apate network inabidi atoke nje kutafuta mnara. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka network haraka ili wananchi wetu wasipate usumbufu wa kusubiri majibu muda mrefu hususan wanawake wa Mkoa wa Ruvuma? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza kwamba tuna mkakati wa miaka mitano wa kupeleka mawasiliano ya simu na data katika maeneo yote nchini. Katika haya maeneo ya hospitali na maeneo mengine muhimu, tutayatekeleza katika awamu ya 11 ambapo Serikali ina mpango wa kupeleka mawasiliano ya internet na data katika maeneo ya mkakati yakiwemo haya ya miundombinu ya Serikali ikiwemo Reli ya TAZARA, SGR, MGR ikiwemo mbuga ya hifadhi za wanyama na maeneo mengine ya kimkakati kama hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba eneo hilo pia kama Serikali tunalifanyia kazi na lipo kwenye mkakati mahususi wa Wizara. Kwa hiyo, tutalifanyia kazi na maeneo yote hayo yatapata mawasiliano ya internet.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri.

WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na tumshukuru sana Mheshimiwa Happiness kwa maswali yake na kuweka msisitizo kuhakikisha kwamba Wilaya ya Nyasa na Tunduru zinapata mawasiliano ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Happiness, katika mradi wetu wa utekelezaji wa ujenzi wa minara 201, Wilaya ya Nyasa tutaweka minara miwili katika Kata ya Liuli pamoja na Mpepo. Vilevile kwa Wilaya ya Tunduru tutajenga mnara katika Kata ya Mchesi pamoja na Mlingoti Magharibi. Hivyo basi, niendelee kumhakikishia kwamba sasa hivi tunakamisha ujenzi wa minara 908 katika kata 730, na tutahakikisha kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivyoeleza katika makakati wetu, tuwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, ifikapo 2030 hakuna eneo ambalo litakuwa halina mawasiliano. Nashukuru kwa nafasi. (Makofi)
MHE. HAPPINESS D. NGWANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Kwa kuwa, mfumo huu umewaathiri sana wanawake wa Mkoa wa Ruvuma, ile kwenda na kurudi kwa ajili ya kufuatilia kupata mkopo huu, kiasi kwamba, wametumia gharama zao, na biashara zao zimefilisika kwa vile ni biashara ndogo ndogo kama mbogamboga au mama lishe. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wamama hawa kupata fedha kwa haraka? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuboresha mfumo wa mikopo hii ili kuanza kupunguza muda wa kusubiri, lakini pia, kuondoa gharama zisizokuwa na lazima na usumbufu kwa wajasiriamali wanaohitaji mikopo hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba, tunaendelea kuboresha. Moja ya mambo ambayo Serikali imetoa maelekezo, nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI kuwasisitiza Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini kwamba, vikundi vya wajasiriamali wanawake, vijana na watu wenye ulemavu mara baada ya kuwasilisha maombi yao, wapewe taarifa kwa njia ya simu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itawafanya wasilazimike kusafiri kwenda na kurudi mara kwa mara, ili kuepuka gharama za nauli na gharama kubwa katika kuomba mikopo. Mikopo inapokuwa tayari wapewe taarifa kwa utaratibu wa uwazi kwa njia ya simu na mbao za matangazo, ili wananchi waweze kupata mikopo hiyo kwa wakati, na pia, bila kutumia gharama kubwa.
MHE. HAPPINESS D. NGWANDO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa barabara hizi zimekuwa na umuhimu sana hasa kwa wananchi wanaoishi mipakani kiuchumi pamoja na ulinzi wao; kwa mfano, tukiongelea Dapoli - Mbinga, Mitomoni Songea, Magazini - Namtumbo kuelekea Wenje na Nalasi – Tunduru, je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka fedha kwa haraka ili kuzuia watu wabaya na wahalifu ambao hawaitakii mema nchi yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Barabara ya Mtwara - Pachani kuelekea Nalasi Lingusenguse imefanyiwa upembuzi yakinifu kuanzia mwaka 2022 na usanifu wa kina. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwenye barabara hiyo ukizingatia ni barabara ambayo wananchi wake wanalima ‘pesa’ nikimaanisha inalima korosho pamoja na ufuta, lakini kilometa 200 kutoka kwenye hospitali ya Kata moja mpaka kufika kwenye Wilaya ndiyo mama mjamzito anaweza kufika huko?

Mheshimiwa Spika, je, Serikali haioni umuhimu wa barabara hii kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma hususan Wilaya ya Namtumbo na Tunduru? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi, kipaumbele cha kwanza kwa barabara za mipakani ni kuhakikisha kwamba nchi yetu inakuwa salama, kwa maana ya kusaidia vyombo vya usalama kuweza kupita muda wote inapohitajika na ndiyo maana tunaziimarisha, pale ambapo hatujazifungua, tunahakikisha kwamba tunazifungua.

Mheshimiwa Spika, ninatambua pia zikishajengwa inakuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi ambao wanazitumia hizo barabara kwa shughuli zao za kawaida ikiwa ni pamoja na kiuchumi na za kijamii. Kwa hiyo, nimhakikishie Mbunge kwamba, Serikali kama tulivyosema, tutaendelea kuziimarisha na kuzifungua na kuhakikisha kwamba zinapitika muda wote.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, ni kweli kwamba tuna barabara hiyo ya Mtwara - Pachani - Nalasi kwenda Tunduru yenye urefu wa kilometa 300, barabara ambayo tumeshakamilisha usanifu, lakini imekuwa ikiombewa fedha, na kwa kuwa bajeti bado haijaruhusu kuijenga barabara yote, tunachofanya kwanza ni kuhakikisha inapitika muda wote na maeneo yote yale korofi, tunachokifanya sasa hivi ni kuhakikisha kwamba tunajitahidi kujenga ama zege, ama lami, ama kama kuna daraja ambalo limekwama, huo ndiyo mkakati ambao tunasema tuijenge ili iweze kupitika kwa muda wote, tukiwa tunatafuta fedha kuijenga barabara yote kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. HAPPINESS D. NGWANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa makuzi ya mtoto bora mwenye ubongo uliokomaa yanaanzia miaka sifuri mpaka miaka nane, wakati huo mama ndiye mlezi mkuu wa mtoto huyu, wakati anatoka kwenye familia yake anakuwa ameongozana na watoto hawa, je, Serikali haioni haja ya huu muda kuwa mrefu kwa kuwa mgogoro huu hadi unafika Mahakamani umetokea kwa Wajumbe wa nyumba kumi na Mabalozi? Kwa hiyo, mgogoro huu ulishawaka moto muda mrefu. Je, Serikali haioni huu muda wa mwaka mmoja mpaka miaka miwili ni mrefu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa mwanamke ana mchango mkubwa kwenye familia na nyumba zetu, lakini mama huyu pale unapotokea mgogoro anatoka yeye na rambo na watoto, hata alivyochangia kwenye ile familia anakuwa habebi, je, Serikali haioni haja kuepusha migogoro isiyo na lazima, wanandoa hawa wanapogombana kila mmoja aende kwa baba yake na mama yake, mlango ufungwe, ili haki itendeke? Ahsante. (Makofi/Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Happiness, kwa kweli anafanya kazi kubwa sana ya kuwasemea wanawake na watoto siyo tu wa Mkoa wa Ruvuma, lakini wa Tanzania nzima kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kwanza kwamba muda wa mpaka miaka miwili wa kesi za talaka ni muda mrefu na unaweza ukaleta athari ya mtoto na hasa mtoto wa chini ya miaka minane. Kama nilivyojibu kwenye majibu ya msingi, ni kwamba muda umewekwa mahususi kwa ajili ya kuhakikisha mashauri mbalimbali yanaisha katika Mahakama ikiwemo mashauri yanayohusiana na masuala ya talaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa muda wa kumaliza Shauri la Talaka katika ngazi ya Mahakama ya Mwanzo ni miezi sita. Ndani ya miezi sita lazima shauri hili liwe limekamilika na maamuzi yametoka, lakini katika ngazi za Mahakama za Wilaya na Mahakama ya Hakimu Mkazi, ni muda wa mwaka mmoja, na katika ngazi ya juu zaidi ambayo ni Mahakama Kuu, ni miaka miwili. Kwa hiyo, mara nyingi kesi za ndoa tunaona zinaisha katika ngazi ya Mahakama ya Mwanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, yapo mazingira mengine ambayo kesi hizi zinaenda katika ngazi ya juu, na ndiyo maana Mahakama imeweka Mwongozo wa kutaka kuharakisha kesi hizi zisikilizwe kwa wakati ili kuweza kutoa haki hizi kwa wakati na kulinda maslahi ya wanaohusika katika mashauri haya ikiwemo watoto wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake sasa la pili ambalo amegusia suala la mwananmke au mke kufukuzwa kwenye nyumba ya ndoa, pindi anapokuwa kwenye shauri linalohusiana na masuala ya talaka, Sheria za Tanzania zinatambua na hasa Sheria ya Ndoa Sura ya 29 hairuhusu mume kumfukuza mke kwenye nyumba ya ndoa. Nyumba ya ndoa imetambulika kabisa kisheria, ni ile nyumba ambayo mume na mke wanaishi. Nyumba hiyo ya ndoa inakuwa na umiliki wa pande zote kwa maana ya mume na mke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mume haruhusiwi kumfukuza mke kwenye nyumba ya ndoa pindi wanapoingia kwenye Shauri la Talaka. Huo ni msingi ambao umewekwa katika Kifungu cha 59 cha Sheria ya Ndoa, lakini tumeona maamuzi mbalimbali yanatolewa na Mahakama kufafanua na kusisitiza msingi huu uliowekwa kwenye Kifungu hiki cha 59. Mathalani kwenye Kesi ya Elizabeth Dikene dhidi ya John Dikene ambayo ni Shauri la Ndoa (Na. 5) la Mwaka 2004. Mahakama imesisitiza msingi wa kwamba mume haruhusiwi kumfukuza mke kwenye nyumba yao ya ndoa wakiwa wako kwenye Shauri la Talaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunafahamu kwenye jamii kunakuwa na changamoto mbalimbali ambazo zinahusisha wanawake kukutana na mazingira kama hayo. Kwa hiyo, wanawake wanapokutana na mazingira kama hayo, wanachoweza kufanya ni kuchukua taratibu za kisheria ambapo anaweza kuwasilisha maombi ya zuio, yaani mhusika, tuseme mke anaweza akaandaa maombi ya dharura Mahakamani (Chamber Summons) kwa ajili ya kuiomba Mahakama kuweka zuio la muda (Temporary Injunction) ili asifukuzwe. Azuie aidha, kufukuzwa kwenye ile nyumba yao ya ndoa au kuzuia pia nyumba kuuzwa, kwa sababu kuna wakati mwingine unaweza ukashaangaa mpo kwenye Shauri la Talaka, lakini nyumba mnayoishi, yaani nyumba ya ndoa ipo katika kuuzwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utaratibu umewekwa, unaweza ukaomba zuio hilo la muda ili Mahakama iweze kuingilia kati na kuzuia hatua za namna hiyo. Maombi haya yanafanyika kwenye Mahakama, ambapo inasikilizwa…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu yako nadhani ameyaelewa na umempa reference nzuri, aende afuatilie. Malizia.

NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa hiyo, kwa wale wanaohitaji Huduma ya Msaada wa Kisheria, katika kila halmashauri kuna dawati la kutoa Huduma ya Msaada wa Kisheria wafike ili waweze kupatiwa suluhu ya changamoto na hususan kama hii ambayo ameitaja Mheshimiwa Happiness.