MHE. HIJA HASSAN HIJA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninaomba nimuulize swali moja la nyongeza. Mwezi Novemba, Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya ziara kwenye hospitali moja hapa Mjini Dodoma na wananchi, hususan wazazi, waliipongeza Serikali kwa huduma nzuri za matibabu na dawa, lakini walilalamikia ukosefu wa mabeseni na ndoo, kwa ajili ya wajawazito; Mheshimiwa Waziri Mkuu akaagiza jambo hili litatuliwe. Ninaomba kujua limefikia hatua gani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. RAJAB S. JAFAR): Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hija Hassan Hija. Tunakumbuka ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye kituo chetu, kile cha afya na akatoa maelekezo yale.
Mheshimiwa Spika, maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ndiyo maelekezo ya Serikali. Nami kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninawaelekeza Waganga Wakuu wote wa Mikoa, Waganga wote, ma-DMO wa Halmashauri na ma-MOI wetu waendelee kutekeleza majukumu hayo, waendelee kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa maana kwamba, sasa mambo ya kuwatoza hivyo vifaa kama mabeseni na ndoo visiwe vikwazo kwa mama zetu wanapokwenda kujifungua katika hospitali zetu
MHE. HIJA HASSAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize swali la nyongeza. Mheshimiwa Waziri, amethibitisha kwamba vijana 6,367 wamepata ajira nje ya nchi, na vijana wengi wamekuwa na utashi wa ajira hizi, lakini wanakwazwa na masuala ya lugha. Je, Serikali ina mpango gani wa kuandaa program maalum kwa ajili ya Watanzania ili wawe na lugha nzuri ambayo inakubalika nje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je,...
MWENYEKITI: Mheshimiwa, swali la nyongeza ni moja tu.
MHE. HIJA HASSAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA MAHUSIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sijasikia swali vizuri.
MWENYEKITI: Naibu Waziri, hajasikia vizuri, hebu uliza kwa ufasaha.
MHE. HIJA HASSAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba, Serikali imekiri kwamba vijana 6,367 wamepata ajira nje ya nchi. Vijana wengi wamekuwa na ari ya kufanya ajira hizo, lakini wanakwazwa na masuala ya lugha. Serikali ina mpango gani wa kuwaandaa vijana wetu ili wakidhi kigezo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA MAHUSIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, tunatoa mafunzo maalum mahususi kwa vijana wanaokwenda nje kwa ajili ya kufanya kazi. Naomba tupokee ushauri wa Mheshimiwa Mbunge, juu ya mafunzo ya lugha, tuongeze katika program yetu ya mafunzo ambayo vijana wanapewa kabla ya kwenda kufanya kazi nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)