Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Patrick Adkin Mwalunenge (2 total)

Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. PATRICK A. MWALUNENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Mpango wa Maendeleo wa Taifa letu wa 2050, 2026 - 2031, na 2026/2027.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, ninampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushindi alioupata. Kwa kuwa hii ni mara ya kwanza kusimama hapa, niseme wazi kwamba, katika Uchaguzi Mkuu, hizi kura alizitafuta yeye mwenyewe baada ya kutekeleza miradi mikubwa ambayo iliachwa na mtangulizi wake. Mfano, mradi wa umeme, mradi wa SGR na Kigongo - Busisi, barabara na miradi mingi ya maji aliitekeleza katika kipindi chake. Kwa hiyo, ushindi alioupata alistahili. Kwa hiyo, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupewa dhamana na kuaminiwa kuwa Waziri Mkuu wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, nimpongeze Mheshimiwa Spika wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Naibu Spika kwa kutuongoza vyema. Vilevile, niwapongeze Wabunge wenzangu wote waliochaguliwa katika kipindi hiki 2025/2030 kuja kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumpongeza Waziri wa Mipango, Mheshimiwa Prof. Kitila kwa wasilisho zuri, Naibu Waziri na Watendaji wote kwenye Wizara hiyo. Pia, nimpongeze Waziri wa Fedha kwa wasilisho lake, Naibu Waziri na Watendaji wake wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliposikiliza huu mpango wa nchi, ukiufuatilia, na pia Waziri wa Fedha alivyowasilisha, kiukweli unaona kuna mwanga mkubwa sana kwa Watanzania na unaona ni Serikali imedhamiria kutatua changamoto za watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nina maoni, na hasa ninajikita kwenye sekta za uzalishaji. Wameongea wenzangu; ameongea Mheshimiwa Shangazi na mwenzangu aliyepita hapa na mimi nitapita mlemle.

Mheshimiwa Mwenyekiti, 75% au 80% ya watu wetu, wako kwenye kilimo, lakini tumekubaliana na mpango wa Wizara ya Kilimo kwamba 2030 kilimo kichangie 10% ya GDP ya nchi yetu. Hatuwezi kufika huko kama hatuna commitment. Mashaka yangu makubwa yapo kwenye utekelezaji wa mpango wenyewe, na Waziri wa Mipango ameongea kwamba kuandika mpango kwenye karatasi ni jambo moja, lakini kutekeleza mpango wenyewe ni jambo lingine. Hapo ndio kwenye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto kubwa la rasilimali watu. Nilidhani mpango huu pamoja na mambo yote mazuri yaliyoongelewa, lakini tungejikita pia kuangalia mpango huu unaendaje sambamba na kutengeneza rasilimali watu? Hilo ndilo tatizo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapanga hivi, lakini watu wanaotekeleza huko chini especially kwenye halmashauri zetu unakuta wanakuwa na matatizo makubwa sana, na huwa mara nyingi wanakuwa kama miungu watu na hawana zile fikra za kibiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiuangalia huu mpango kwa 100% ni kama biashara, na nina-declare interest, mimi ni mfanyabiashara. Mfanyabiashara kwanza anaulinda mtaji, anapunguza matumizi, lakini pia mfanyabiashara anataka kuona matokeo, na biashara yake ikue, na ukiuangalia huu mpango, malengo yake ni hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nitajikita zaidi kwenye kilimo. Sekta ya Kilimo ndiyo imeajiri watu wengi sana kwenye nchi yetu na ndiyo inaweza ikaleta jawabu la matatizo ya ajira kwenye nchi yetu kama tukijipanga sawasawa. Kwa nini, ninasema hivyo? Tunayo sisi mazao ya kimkakati. Tunalo zao la pamba, tunalo zao la korosho, tunayo kahawa, tunayo chai, tunayo kokoa na pia tunayo mazao ambayo yanaitwa cereals (alizeti, ufuta na mazao mengine) na yote haya yameundiwa bodi zake za zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia namna zile bodi zinavyofanya kazi, utaona kabisa kwamba mpango unasema hivi lakini ile dhamira ya dhati haipo, kwa sababu zile bodi zinasuasua, hazijatengewa bajeti ya kutosha ili ziweze kuzalisha kwa tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, unaona Bodi ya Pamba kwa miaka mitano mfululizo wanahangaika ili waweze kufikia angalau tani 500,000 za uzalishaji. Pamba hiyo ukiangalia watu wa huko kanda ya ziwa ni zaidi ya watu 15,000,000 wanategemea zao lile, lakini uzalishaji kila siku unasuasua. Kwa sababu gani? Bodi ya Pamba maana yake na sekta zima haina mtaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa takwimu, mimi siyo mtaalamu wa takwimu, lakini watu wa fedha watatusaidia, percentage ya dola zinazokwenda nje kwa ajili ya kuagiza nguo ni fedha nyingi sana zinakwenda China na Uturuki, lakini sisi tunalima pamba hapa. Ili kiwanda cha pamba kiweze kuanzishwa hapa, na kuzalisha kuanzia nyuzi mpaka nguo, angalau tuweze kuzalisha tani 1,000,000; lakini leo hii hatujawahi kufikisha tani 1,000,000 hata tani 500,000 hatujafikisha. Sasa utaona ni jinsi gani tunavyopishana. Mpango unasema hivi, lakini na kwenye utekelezaji ni tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, maoni yangu hapo, mpango na Wizara ya Fedha tuziwezeshe hizi bodi za mazao kwa kuzipa mitaji. Ninafurahi na ninaipongeza pia Kamati. Commitment yao kwamba lazima hawa Wakurugenzi wa Taasisi na Wakurugenzi wa Halmashauri wawe wanashindanishwa ili waweze kupatikana; maana yake ni nini? Kama ni Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba au Bodi ya Pareto au Bodi ya Chai ameshindanishwa kibiashara na amepewa mtaji. Maana yake lazima atazalisha kwa faida, na mwisho wa siku tutapata viwanda vya kuzalisha nguo hapa kuanzia nyuzi mpaka nguo, final product. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda kimoja cha nguo kikitengenezwa kinaweza kulisha watu wasiopungua 3,000. Sasa tukiwa na viwanda 10, maana yake uzalishaji utakuwa mkubwa lakini na watu wetu watapata ajira za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tunaishukuru Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa makusudi kupitia Wizara ya Kilimo waliwekeza kupeleka pembejeo kwenye zao la korosho na tija imeonekana. Uzalishaji umetoka tani 200,000, 150,000 ikawa inasuasua mpaka tani 500,000 na pesa zilizoenda kwa wakulima ni zaidi ya shilingi trilioni 1.5. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ile pesa imekwenda kwa wakulima na nyingine Serikali imepata kodi. Sasa tukiwekeza kwa makusudi kwenye sekta ya kilimo nina uhakika tutajibu matatizo mengi. Kwanza, tutajibu tatizo la bima ya afya kwa sababu haya mazao yote yapo kwenye mfumo wa ushirika. Tunaweza tukaamua hawa wakulima wote ambao wapo kwenye sekta ya korosho wakatiwe bima za afya kupitia zao lao na inawezekana kabisa kwa sababu wana mapato ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tazama wakulima wa zao la kahawa kule kwetu Mbeya na Songwe na wenyewe pia hivyo hivyo. Serikali ikiwezesha mitaji kule, maana yake watakatiwa bima na watapata mazao, lakini hata kujengewa nyumba za bei rahisi kwa sababu tayari wana mazao ya uhakika na uhakika wa kuvuna. Kwa hiyo, ninaiona sekta ya kilimo kwamba ndiyo solution ya matatizo kwenye nchi yetu na tunaweza kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tu iweke commitment hapa kwamba uwekezaji wote unaoenda kuzalisha basi, central bank, kwa maana ya Wizara ya Fedha iwe inatoa guarantee kwenye haya hizi sekta. Kwa mfano, hizi bodi za mazao siyo lazima wawape fedha cash. Wanatoa guarantee kwamba huu ni mradi unaoenda kuzalisha ajira za watu labda 10,000. Kwa hiyo, Serikali itoe guarantee pale ili hawa watu wanaoenda kukopa kwenye commercial bank wakope kwa ratio ambayo iko chini ya 10%, na nina uhakika tija kubwa sana itapatikana kwenye mazao yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, kuwe na mpango wa makusudi wa kutafuta masoko nje ya nchi. Tunao mabalozi wetu sisi kila mahali na wenyewe watusaidie au tutengeneze chombo maalum kinachoshirikiana na mabalozi wetu kwenye kutafuta masoko kwa sababu kuna masoko mengi sana nje ambayo hatujayafikia ili tuweze kuleta foreign currency (fedha za kigeni) ambazo mimi nina uhakika kama tukishirikiana vizuri na mabalozi wetu na tukaunda chombo maalum kwa ajili ya kutafuta masoko tija itakuwa ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano. Mimi nilipata order ya kupeleka machungwa Shanghai. Nilipopeleka sample ya machungwa yetu yaliyoko Tanga na Mbeya kule yakaonekana hayana vigezo. Kwa hiyo, mimi ninayatoa machungwa South Africa ninayapeleka Shanghai na China, wakati kumbe tungetengeneza mpango mzuri hapa kupitia Wizara ya Kilimo, wale watu wanaolima machungwa Mbeya na Tanga kule kwa wenzetu, yaka-meet zile standard, ni dola nyingi sana zingeingia, na nchi yetu ingetengeneza mapato na ajira zingepatikana. Kwa hiyo, iko mifano hai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kabisa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umekwisha.

MHE. PATRICK A. MWALUNENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kabisa ni uagizaji wa mafuta ya kupikia na ngano. Lazima tuamue kama nchi kwamba sasa tunakomesha uagizaji wa mafuta nje ya nchi kwa kulima alizeti na michikichi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. PATRICK A. MWALUNENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa fursa hii mchana na mimi niweze kuchangia bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu. Awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa uzima nikapata fursa hii leo ya kuweza kutoa mchango wangu na mawazo kwenye bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza ninamshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya, alishajipambanua wazi kupitia hotuba yake aliyolihutubia Bunge, maelezo aliyoyatoa na kazi kubwa anazozifanya kwenye nchi hii, Wabunge wengi wamezungumza, sitaki kurudia huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninampongeza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa bajeti nzuri aliyoleta na kazi anazoendelea kuzifanya kwenye nchi hii, kwa ziara anazozifanya kwenye mikoa na kutatua kero za wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaleta matumaini makubwa kwa wananchi wa Tanzania kwamba sasa Serikali yao ipo kazini. Ninasisitiza tu Wasaidizi wa Rais kwa maana ya Mawaziri, wasaidizi wa Waziri Mkuu sasa waige ile njia anayoifanya Waziri Mkuu kutatua kero za wananchi na hiyo ndiyo njia pekee ambayo wananchi wetu wanataka. Wananchi wa sasa wanataka kuona matokeo tumeshazungumza sana, tumeshaandika sana makaratasi, hasa vijana waliopo sasa wanataka kuona matokeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ni nzuri, mambo ni mengi yamezungumzwa, nijikite kwenye Jimbo langu la Mbeya Mjini, pia niendelee kumpongeza na Dada yangu aliyetangulia kuzungumza hapa Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo ametuwakilisha vizuri wananchi wa Mbeya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru wananchi wa Mbeya Mjini kwa kunipa imani hiyo ya kuwa mwakilishi wao hapa Bungeni. Wanambeya mjini pale shughuli zetu kubwa ni biashara, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa maana Waziri Mkuu na Watendaji wake Mipango, TAMISEMI watakubaliana nami kwamba, umefika wakati muafaka sasa kwenda kuweka shughuli za biashara kwa maana kongani za viwanda kwenye Jiji la Mbeya, kwa sababu Jiji la Mbeya ni jiji la biashara na Jiji la Mbeya, ni barabara inayopitisha magari mengi na ndiyo lango la SADC kuelekea nchi zote za Kusini mwa Afrika, lakini hatuna viwanda Mbeya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kujibu tatizo la ajira la vijana wetu kaka yangu Kitila atuletee kongani za viwanda Mbeya, atuletee uwekezaji Mbeya ili tunufaike na jiografia ya Mbeya ilivyo, kwa maana Mbeya ni lango la SADC, lakini kuna wakulima wengi wa mazao, basi tupate viwanda ambavyo vinatokana na uzalishaji wa mazao ya kule kama vile viazi, machungwa, ndizi, mpunga ili yale mazao tuweze kuyaongezea thamani na watu wetu waweze kupata ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameongea sana hapo dada yangu na mimi ninakazia kwenye suala la miundobinu. Mbeya tunao utalii mwingi sana lakini bado hatujautangaza vizuri kwa sababu ya hali ya miundombinu. Nikiongea specific Mbeya Mjini, barabara nyingi za Mbeya Mjini hazipitiki vizuri. Ikiwa wakati wa mvua mifereji inajaa na wakati mwingine inaziba, wakati wa jua vumbi kali. Sasa huwezi kuwa na Jiji la aina kama ya Mbeya lenye wafanyabiashara wengi ambao wanajituma, vijana wanaweza kufanya kazi halafu barabara hazipitiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ninaiomba Ofisi ya Waziri Mkuu watupatie barabara angalau hata kilometa 100 ya barabara za ndani ya Jiji la Mbeya, ninawahakikishia Mbeya itastawi na itashamiri na itavutia utalii na watu wa Mbeya ni wachapakazi wazuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasi tunajiongeza wakitupatia barabara hizo kilometa 100 tumeanza kuandika andiko hivi sasa kupitia viongozi wangu wa Mkoa kwa maana ya Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Jiji, tumeanza kuandika andiko ambalo kama watatukubalia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa maana ya TAMISEMI waturuhusu tukope pesa kwenye taasisi za fedha ili tujenge hizo kilometa 100, kwa sababu Jiji letu linalo uwezo wa kukusanya mapato ya kulipa. Kwa hiyo, tutaandika hilo andiko na tutaliwasilisha kwao walione kama linakidhi vigezo waturuhusu ili sisi tuondoe vumbi Mbeya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao uwezo kwa sababu mapato tunayo, tupate mkopo hata wa miaka 20 tunao uwezo wa kulipa, sisi Jiji letu la Mbeya tuisaidie Serikali yetu, wakati wanahangaika kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga miradi mingine ya barabara ya njia nne, barabara za ndani ya jiji tunao uwezo wa kuzijenga kupitia vyanzo vetu vya mapato. Hilo linakuja na nitaomba waliangalie ili tuweze kuiweka Mbeya yetu katika hali nzuri na barabara ziweze kupitika vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni ukarabati wa masoko. Mimi ninajikita sana huko kwa sababu watu wa Mbeya ni wafanyabiashara, masoko yetu mengi yana hali chakavu na tumesema tunataka watu wetu wakajiajiri na maeneo ya kujiajiri ni maeneo ya masoko, lakini masoko yetu mengi ya Jiji la Mbeya yana hali mbaya sana. Wakati wa mvua wafanyabiashara wananyeshewa mvua, wakati wa jua wanapigwa na jua. Kwa hiyo, tunaomba kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu watuwekee bajeti kwa ajili ya ukarabati wa masoko yote yaliyoko kwenye Jiji letu la Mbeya ili yafanane na hadhi ya Jiji la Mbeya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Mbeya ni lango la SADC, tunaomba pale na sisi siku moja tuje tu-host mikutano mikubwa kama wanavyo-host wenzetu wa Arusha mikutano – AICC, basi na sisi tuwe na ukumbi mmoja pale mkubwa utakaoweza ku-host mikutano ya SADC badala ya watu kutoka Nchi za Kusini mwa Afrika wanapita kwenye anga letu wanaenda kufanya mikutano Dar es Salaam. Tunaomba sana Wizara kwa maana Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI na Ofisi ya Mipango watusaidie jambo hilo ili siku moja nasi tuweze ku-host mikutano mikubwa na hiyo itakuwa njia pekee ya kuutangaza utalii wetu tulionao kwenye Mkoa wetu wa Mbeya na Mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini na Mbeya itakuwa ni center ya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo michango yangu itajikita sana kwenye biashara kwa sababu sisi pale Mbeya tunafanya biashara. Pia suala la mikopo kwa vijana, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais ametuundia mpaka Wizara ya Vijana na tunaye Waziri machachali kabisa sina mashaka na yeye, hofu yangu inanijia kwa wale watu watakaokuwa wanamsaidia kazi, je ni watu wabunifu? Kwa sababu vijana wanayo staili yao jinsi ya kuishi nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshapata Waziri mzuri, sawa Mheshimiwa Rais amefanya jambo jema ametuwekea pale bilioni 200 kianzio cha mtaji, lakini ninatamani ile bilioni 200 kuizalisha zaidi iwe mara tano ya ile bilioni 200, nayo inawezekana Wizara ya Vijana ijiongeze waweke vikao na hizi taasisi nyingine kwa maana hii Mifuko ya Hifadhi, ina pesa kule, lakini haiwekezi kwenye miradi ambayo itaongeza ajira kwa vijana wanawekeza kwenye kujenga majengo ambayo return yake ni ya muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninawaomba kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Vijana ikae na hii Mifuko ya Hifadhi, wana pesa nyingi kule wawekeze kwenye miradi itakayoleta matokeo kwa vijana kujenga mabwawa ya umwagiliaji ambako kule vijana wengi watahitaji kwenye kilimo, kujenga zile skimu za umwagiliaji na masuala ya ufugaji wa samaki, ufugaji wa ng'ombe kule ndiyo kwenye matokeo. Maana yake unakuta Mifuko ya Hifadhi inaenda kuwekeza kwenye majengo ambayo unakuta return yake ni ya miaka 100 na wakati mwingine pesa hiyo hairudi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuna hawa watu wa TFS na TANAPA imekuwa ni tatizo kubwa, ni mgogoro mkubwa sana kila mahali kwenye nchi hii, hii tu inatokana na kwamba wao TFS hawazalishi wao ni regulator ili kufanya udhibiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja nikawauliza watu wa TFS kwa nini ninyi mnawaambia wananchi waulinde msitu tu, wataulinda kwa miaka mingapi, badala ya ule msitu utumike kwenye kufuga nyuki, wale wananchi wa eneo husika wakafuga nyuki wakaulinda wao ule msitu, wakawa na chanzo kipya cha mapato badala ya kuwakataza kukata kuni, kukata mkaa lakini wakati huo hamuwapi njia mbadala ya kuzalisha lakini wakati huo TFS ataongeza mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana unaona juzi tu hapa niliongea na Waziri Mkuu, watu wa TANAPA, watu wetu wa Mbarali wamelima mpunga ekari karibu 2000, wanakwenda kuziteketeza wanasema wamelima maeneo yaliyotunzwa na ni eneo oevu. Sasa unajiuliza, yule mtu alipanda lini mpunga, wao walikuwa wako wapi? Tunamshukuru Waziri Mkuu aliliingilia kati akazuia, lakini wale watu walikuwa wamejiandaa, wanatumia fedha za Serikali kwenda kuteketeza mpunga ambao mwananchi anatakiwa avune baada ya miezi miwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona hili si jambo jema, tunaongea hapa watu wakajiajiri, tutengeneze ajira, watu wajiajiri kupitia kilimo, leo ekari 2000 zimelimwa, watu wanachukua pesa ya Serikali kwenda kuteketeza ule mpunga! Sasa hii ni namna ya kuichonganisha Serikali na wananchi na kuwachonganisha na Rais.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. PATRICK A. MWALUNENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)