MHE. ESTER A. BULAYA K.n.y. MHE. PATRICK A. MWALUNENGE aliuliza: -
Je, lini Serikali itakamilisha Mradi mkubwa wa Maji kutoka chanzo cha Mto Kiwira ili kukomesha tatizo la maji Mbeya Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Patrick Mwalunenge, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kutoa maji Mto Kiwira kwenda Jijini Mbeya. Miongoni mwa kazi zinazotekelezwa kupitia mradi huo ni pamoja na ujenzi wa dakio (intake) na mtambo wa kutibu maji lita milioni 117 kwa siku, ujenzi wa matanki mawili yenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni 10 sambamba na ulazaji wa mabomba umbali wa kilometa 37.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa 48% na kwa mujibu wa mkataba unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba, 2026 ambapo utanufaisha zaidi ya wakazi 890,000 wa Jiji la Mbeya na Mji wa Mbalizi. (Makofi)
MHE. BARAKA A. U. MWAMENGO K.n.y. MHE. PATRICK A. MWALUNENGE aliuliza:-
Je, lini ujenzi wa Barabara ya TANZAM kutoka Igawa hadi Mbeya Mjini kuunganisha Mbeya Mjini hadi Tunduma, pamoja na Bypass utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Patrick Adkin Mwalunenge, Mbunge wa Mbeya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Barabara ya Igawa – Songwe – Tunduma, yenye urefu wa kilometa 218, pamoja na njia ya mchepuko ya Uyole – Songwe, yenye urefu wa kilometa 48.9 unatekelezwa kwa utaratibu wa ubia wa Serikali na Sekta Binafsi (PPP). Kwa sasa, mwekezaji wa mradi huo anaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu ambao unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Novemba, 2026.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi za ujenzi wa barabara hii zitaanza baada ya kukamilika majadiliano kati ya Serikali na mwekezaji. Aidha, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea na ujenzi wa barabara ya njia nne kuanzia Nsalanga – Ifisi, yenye urefu wa kilometa 29, ambayo ni sehemu ya barabara hiyo.