Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Nassoro Rashid Nassoro (1 total)

MHE. NASSORO RASHID NASSORO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri aliyonipa, lakini katika eneo hilo la Makangale ambalo sasa hivi linaendelea kukua kiutalii na wageni wanaingia na kutoka, na wengine bila kuripoti katika Ofisi za Uhamiaji. Juzi tu kuna mgeni tulimkamata ana wiki mbili hajaripoti katika Ofisi za Uhamiaji na tukaweza kumpeleka katika Ofisi za Uhamiaji. Je, Waziri ana mpango gani kwa sasa hivi kuweza kuidhibiti hiyo hali au kuiondoa kabisa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kumshukuru Mheshimiwa Nassoro Rashid Nassoro, kwanza kwa uzalendo wa kujua na kuifanyia kazi Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususan kwa kuwa mlinzi wa eneo ambalo unatoka.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili naomba nikuhakikishie kuwa eneo hilo ni la kimkakati, ni kati ya shehia ambazo zipo kwenye eneo ambalo watalii wengi sana wanakuja. Nikuhakikishie kwamba nitaongeza idadi ya askari ambao watakuja kushirikiana na viongozi wote wa shehia ili kuweza kufanya doria na kuimarisha vipenyo vyote ambavyo kuna uwezekano wa hao wanaokuja kuingia na kutoka bila kufuata utaratibu.

Mheshimiwa Spika, pia tutaendelea kuwachukulia hatua wote ambao watapatikana kadri ya vile ambavyo itathibitika kuwa wameingia na kutoka bila kufuata utaratibu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.